Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ndani ya Boksi: Oktoba 29, wasanii kujenga jamii mpya 

Muktasari:

  • Kwa hisia za chuki, taharuki na kugawanyika hovyo miongoni mwa raia wa taifa moja. Lakini zaidi ya yote ni kipimo cha utu, umoja na nafasi ya kila mmoja wetu. Hasa wale wenye ushawishi mkubwa katika jamii

Dar es Salaam. Oktoba 29 imebaki kama alama ya uchungu katika kumbukumbu za Watanzania. Ni siku iliyoacha majeraha ya kijamii, hofu, na maswali mengi yasiyo na majibu.  Siku ambayo amani ya kawaida ilitikiswa. 

Kwa hisia za chuki, taharuki na kugawanyika hovyo miongoni mwa raia wa taifa moja. Lakini zaidi ya yote ni kipimo cha utu, umoja na nafasi ya kila mmoja wetu. Hasa wale wenye ushawishi mkubwa katika jamii.

Zaidi ya tukio, ni fundisho

Siyo tukio la kisiasa tu, ni jeraha la kijamii. Matokeo ya maneno, propaganda, misukumo uliokosa uangalizi. Waliopoteza maisha, waliojeruhiwa, familia zilibaki na huzuni, nchi ikashuhudia hofu ikisambaa haraka kuliko ukweli.

Matukio kama haya huonyesha jinsi jamii inavyoweza kupasuka kirahisi. Pale sauti zenye busara zinaponyamaza kimyaa, na hisia zinapopewa nafasi ya kuongoza fikra. Hakika hakuna somo gumu kwetu kama la Oktoba 29.


Wanamuziki na wasanii

Wanamuziki na wasanii wa filamu ni zaidi ya waburudishaji. Wao ni walimu wa kihisia, watafsiri wa jamii, viongozi wa kiutamaduni. Wanapozungumza husikiliza na vijana. Wanapochukua msimamo, maelfu kwa maelfu huwaiga.

Katika kipindi kama kile cha Oktoba 29, walipaswa kuwa nguzo za utulivu. Kwa kupaza sauti za amani, busara na umoja badala ya kujiweka pembeni. Ama kwa wengine kuendeleza misimamo ya chuki kupitia mitandao.

Wasanii walipaswa kutumia majukwaa yao kufundisha watu, kutofautisha kati ya haki na hasira, kati ya hoja na matusi.

Kwa bahati mbaya, baadhi yao waliamua kukaa kimya, huku wengine wachache wakitumia majina yao makubwa kuchochea moto wa taharuki.


Wasanii wafanye nini sasa?

Baada ya maumivu ya Oktoba 29, jamii inahitaji ujenzi mpya wa kisaikolojia. Na wasanii wana nafasi kubwa katika mchakato huo. Kwa sababu wao ni sauti inayofika haraka katika masikio ya Gen Z kuliko hata viongozi wa kiroho.

1. Kurejesha matumaini:
Waandae nyimbo, filamu na maudhui yanayohusu amani, msamaha na umoja. Sanaa iwe tiba, si chachu ya hasira. Sanaa iwe elimu siyo chachandu ya kisasi.

2. Kuwa sauti za maridhiano:
Waimbe na kuigiza simulizi zinazohamasisha watu kukaa meza moja na kuzungumza. Kwa maana sanaa ina nguvu ya kugusa mioyo kuliko siasa. Sanaa inawafikia haraka kuliko siasa.

3. Kujenga uelewa wa kizazi kipya: 
Watumie ushawishi wao kuelekeza vijana, kwenye njia za kujitambua na kushiriki katika ujenzi wa nchi kwa amani. Kataa ubinafsi maana jamii ikiyumba na wao watayumba.

4. Kujiepusha na uhasama wa kisiasa:
Msanii anapopoteza usawa, hupoteza nguvu yake ya kuunganisha. Busara ni kuwa na maoni bila kugeuka kuwa chombo cha mgawanyiko. Na hili litazamwe kwa jicho elekezi.

Mitandao ya Kijamii: 
Oktoba 29 ilionesha upande wa giza wa mitandao ya kijamii.
Twitter (X), Instagram, TikTok, na Facebook ziliwaka moto kwa habari zisizothibitishwa, picha zilizopotoshwa na maneno ya kuchochea. 

Watu walitenda kwa hisia badala ya ukweli. Mitandao ni chombo chenye nguvu kinaweza kuokoa taifa au kukiharibu kabisa ndani ya dakika chache. Tatizo siyo ile teknolojia, bali ni yale matumizi yake ndio tatizo lilipo.


Nini kifanyike?

1. Elimu ya kidijitali (Digital Literacy):
Jamii inahitaji kuelimishwa kutambua taarifa sahihi, kuepuka “forward” zisizo na chanzo, na kujifunza kuthibitisha kabla ya kushiriki. Jamii ijue mitandao ni shetani au malaika kwa namna utumiavyo.

2. Wasanii kama walinzi wa taarifa:
Watu maarufu wapewe mafunzo au miongozo, kuhusu namna bora ya kutumia majukwaa yao bila kuongeza taharuki. Kwani wasanii na watu maarufu walio wengi hili suala la matumizi sahihi ya hii mitandao limewapita kushoto.

3. Kampeni za amani mtandaoni:
Redio, televisheni, na serikali zishirikiane kuanzisha kampeni kama #SambazaAmani, #TumiaMitandaoKibinadamu n.k., ambazo zinahamasisha uwajibikaji wa watumiaji. Na hii iwe ni suala la lazima.

4. ‘Iinfluencers’ na ujenzi wa maadili:
Badala ya kutumia umaarufu kwa utani na vijembe, wapewe nafasi za kuelimisha jamii kwa ubunifu. Kupitia video fupi, nyimbo, au mashairi. Hawa wana vijiji vyao mitandaoni na wanafuatiliwa sana, wanahitajika.

Vyombo vya Habari
Redio hasa zina nafasi ya kipekee zinawafikia watu wa kawaida, hata wale wasiokuwa na intaneti.

Zikitumia muda wake vizuri, zinaweza kuwa mabalozi wa amani kwa kuandaa vipindi vya mijadala. Kama vile vikao vya vijana na kuibua simulizi za matumaini baada ya majeraha ya kijamii.

Vipindi kama “Sauti ya Mtaa,” “Amani Yetu,” au “Vijana na Taifa” vijikite kuelimisha, kuunganisha na kutibu mitazamo iliyovunjika.

Wakati wa Kuwasha Taa Mpya
Oktoba 29 ilikuwa giza. Lakini kila giza linafundisha thamani ya mwanga. Leo, tunapaswa kujifunza kwamba amani haijengwi na wanasiasa pekee, bali na kila mmoja mwenye ushawishi katika jamii.

Wanamuziki, waigizaji, watangazaji, wanablogu, na watu maarufu. Wote ni walimu wa kizazi kipya. Wana uwezo wa kuibadilisha jamii kupitia sauti, picha na maneno yao. Wasitumie majukwaa yao kulalamika, bali kwa kujenga.

Mitandao yetu isiwe silaha ya chuki, bali daraja la kuelewana. Na kila mmoja wetu, kwa nafasi yake, awe staa wa amani, sio staa wa taharuki. Awe staa wa upendo siyo chuki. Staa wa maelewano siyo migongano.