Rayvanny na Nora Fatehi damu zimeendana
Muktasari:
- Toleo hili jipya, Oh Mama! Tetema (2025) linalotawala chati za muziki duniani kwa sasa, limeshirikisha mastaa wengine kutokea India kama Shreya Ghoshal, Vishal Mishra, Sanjoy na Bhushan K.
Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Fleva, Rayvanny bado anaendelea kuishika dunia na wimbo wake, Tetema (2019) uliotayarishwa na S2kizzy. Hiyo ni baada ya kuachia toleo lake la nne akishirikiana na Nora Fatehi ukiwa ni wimbo wa pili kufanya pamoja ndani ya miaka mitano.
Toleo hili jipya, Oh Mama! Tetema (2025) linalotawala chati za muziki duniani kwa sasa, limeshirikisha mastaa wengine kutokea India kama Shreya Ghoshal, Vishal Mishra, Sanjoy na Bhushan K.
Ikumbukwe toleo la kwanza la wimbo huu, Rayvanny alimshirikisha Diamond Platnumz, la pili, Tetema Remix (2019) akawa na Patoranking, Zlatan na Diamond tena, kisha la tatu, Mama Tetema (2021) akawa na Maluma kutokea Colombia.
Tangu Rayvanny ameanza kutoa matoleo mpya ya Tetema, yamesababisha wimbo huo kuzidi kuwa mkubwa na kuikuza chapa yake kimataifa kama ilivyokuwa kiu yake kwa miaka yote.
Mathalani toleo la Mama Tetema (2021) ndilo lilisababisha kupata nafasi ya kutumbuiza katika tuzo za MTV Europe Music Awards (MTV EMAs) na kuandika rekodi kama mwanamuziki wa kwanza kutokea Afrika kufanya hivyo.
Wimbo huo ulijumuishwa katika albamu ya Maluma, Don Juan (2023) ambayo aliwania tuzo ya Grammy katika kipengele cha Best Latin Pop Album 2024, kitu ambacho Rayvanny na S2kizzy hadi leo wanatamba nacho wakisisitiza hakuna mwanamuziki au mtayarishaji Bongo mwenye rekodi hiyo.
Bila shaka toleo hili la Oh Mama! Tetema (2025) litafanya maajabu sana duniani na tayari limeshaanza. Video yake ndani ya saa 24 tangu kuachiwa kwake ilitazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 7.4, na ndani ya siku 3 ikafikia milioni 10, ukiwa ni mradi wa kwanza wa Rayvanny na Bongofleva kwa ujumla kupiga namba hizo ndani ya muda huo.
Video hii imevuma (trend) katika chati za YouTube kwenye nchi takribani 60 duniani ikishika namba moja huku Rayvanny akisema alikuwa anafikirikia walau siku moja ashike namba 10 ila sasa yupo namba moja duniani.
"Haya yalikuwa mawazo yangu ya kila siku, siku nije kuwa trending ya dunia nzima acha hizi za nyumbani za kila siku. Nilikuwa nawaza hata nikishika namba 10 sio mbaya ila Mungu ni fundi sana, wimbo wetu upo namba moja duniani, hii inanipa nguvu kuamini kila kitu kinawezekana, historia imeandikwa na Oh Mama Tetema," amesema Rayvanny.
Hata hivyo, huwezi kuzungumza mafanikio makubwa ya wimbo huu bila kuitaja lebo ya T-Series ambayo ndio imesimamia mradi wote huo. Video hii imewekwa katika chaneli ya T-Series ambayo ina wafutiliaji (subscribers) zaidi ya milioni 300.
Hadi sasa YouTube chaneli ya T-Series iliyofunguliwa Machi 13, 2006 ikijikita huko India, ni ya pili duniani kwa kuwa na wafutiliaji wengi wa maudhui yake, hivyo kazi nyingi za filamu na muziki zinazopandishwa hapo mara zote hupata mamilioni ya watazamaji.
T-Series ni lebo ya muziki na kampuni ya utayarishaji wa filamu ya Kihindi iliyoanzishwa na Gulshan Kumar hapo Julai 11, 1983. Inajulikana zaidi kwa muziki wa filamu za Kihindi na muziki wa Indi-pop, huku maudhui yake YouTube yakiwa yameshatazamwa mara bilioni 307.8.
Hii ndio lebo kubwa zaidi ya muziki India, ikiwa imeshikilia hadi asilimia 35 ya soko la muziki wa India. Ingawa inajulikana zaidi kama lebo ya muziki, T-Series pia imetayarisha filamu zaidi ya 100, na kwa miaka mingi imejipambanua kama kampuni inayoongoza katika utayarishaji wa filamu za Kihindi.
Mnamo Februari 2019, T-Series walimsaini Nora Fatehi kama msanii wa kipekee ambaye atashirikishwa katika filamu zao zijazo, na tangu wakati huo ameendelea kuwa staa mwenye nguvu kubwa ya ushawishi duniani kutokana na umahiri wa kazi yake.
Katika wimbo wa 'Oh Mama Tetema', Nora ndiye anatajwa na kuzungumziwa zaidi na mashabiki wengi Bongo kutokana na umaarufu wake hasa upande wa filamu za Kihindi na alianza kazi yake ya uigizaji kupitia filamu, Roar: Tigers of the Sundarbans (2014).
Huu ni wimbo wa pili kwa Nora kushirikiana na Rayvanny baada ya hapo awali kutoa, Pepeta (2019). Ni ngoma ambayo video yake imeshatazamwa YouTube zaidi mara milioni 92, ikiwa ni ya pili kwa Nora kufanya vizuri zaidi katika mtandao baada ya kupitwa na ile aliyomshirikisha Jason Derulo kutokea Marekani, Snake (2025).
Pepeta ulikuwa wimbo wa kwanza wake Nora wa kimataifa kuiimba kwa lugha ya Kiingereza, na baadaye alichaguliwa kushiriki katika wimbo, Light The Sky (2022) kwa ajili ya Kombe la Dunia la FIFA 2022 nchini Qatar ambapo alishirikiana na wasanii wengine kama RedOne, Manal, Balqees na Rahma Riad.