Rayvanny ndani ya Kombe la Dunia
Muktasari:
- Tamasha hilo la kimataifa linatarajiwa kufanyika Juni 11, 2026 na litahusisha maonesho ya moja kwa moja kutoka miji mitatu ya wenyeji wa mashindano hayo ambayo ni Mexico City, Toronto na Los Angeles.
Dar es Salaam. Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Rayvanny, ameendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa baada ya kutangazwa kuwa miongoni mwa wasanii watakaotumbuiza katika Tamasha la Kombe la Dunia la FIFA 2026.
Tamasha hilo la kimataifa linatarajiwa kufanyika Juni 11, 2026 na litahusisha maonesho ya moja kwa moja kutoka miji mitatu ya wenyeji wa mashindano hayo ambayo ni Mexico City, Toronto na Los Angeles.
Ushiriki wa Rayvanny katika tukio hilo unaonekana kuwa hatua kubwa kwa muziki wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, huku ukiendelea kuthibitisha kuwa wasanii kutoka ukanda huo wanaweza kushindana na kupata nafasi kwenye majukwaa makubwa duniani.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na waandaaji, Rayvanny anatarajiwa kutumbuiza katika jiji la Toronto, Canada, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea ufunguzi wa michuano ya Kombe la Dunia 2026.
Iwapo ataonekana jukwaani kama ilivyopangwa, Rayvanny atakuwa miongoni mwa Watanzania wa kwanza kupata nafasi ya kutumbuiza katika matukio rasmi yanayohusiana na Kombe la Dunia, jambo ambalo litakuwa historia muhimu kwa tasnia ya muziki nchini.
Inaelezwa kuwa nafasi hiyo imekuja kupitia ushirikiano wake wa kimuziki na mwanamuziki na mwigizaji maarufu kutoka India, Nora Fatehi, ambaye aliwahi kufanya kazi na nyota huyo wa Tanzania wimbo uitwao ‘Oh Mama! Tetema’ uliyotoka miezi tisa iliyopita ukiwa umetazamwa mara milioni 107 katika mtandao wa YouTube.
Katika miaka ya karibuni, Rayvanny amekuwa mmoja wa wasanii wa Tanzania waliofanikiwa kupanua soko lao nje ya Afrika Mashariki kupitia ushirikiano na wasanii kutoka Afrika, Asia, Ulaya na Amerika, hatua iliyomjengea umaarufu mkubwa kwenye majukwaa ya kimataifa.
Tangazo la ushiriki wake katika tamasha hilo limepokelewa kwa furaha na mashabiki wengi wa muziki nchini Tanzania, ambao wanaamini kuwa ni ishara ya ukuaji wa muziki wa Bongo Fleva katika soko la dunia.
Kwa sasa macho ya wengi yataelekezwa Toronto kusubiri kuona kama nyota huyo wa "Tetema" atatumia jukwaa hilo kubwa kuendelea kuiandika historia ya muziki wa Tanzania mbele ya mamilioni ya watazamaji.