Siri nguli wa hip-hop Bongo kumkubali Dizasta
Muktasari:
- Muundo wa mashairi yake unajumuisha usimulizi wa matukio na hadithi za maisha halisi ya jamii anayotokea, tungo zake zinasifika kwa kuelimisha na kugusa masuala ya kijamii kama vile malezi, siasa, umasikini, dini, haki na usawa, na masuala mengine ndani na ulimwengu mzima kwa ujumla
Dar es Salaam.Kwa wafuatiliaji wa muziki wa Hip-hop jina la Dizasta Vinna sio geni masikioni mwao, kutokana na umaarufu aliopata kwenye kiwanda cha burudani nchini. Edger Vicent 'Dizasta Vinna' mzaliwa wa Iringa, ambaye pia ni mwanzilishi wa kundi la panorama Authentik, ni miongoni mwa wasanii wa Hip-hop wachache Bongo wanaofuata misingi ya muziki huo.
Muundo wa mashairi yake unajumuisha usimulizi wa matukio na hadithi za maisha halisi ya jamii anayotokea, tungo zake zinasifika kwa kuelimisha na kugusa masuala ya kijamii kama vile malezi, siasa, umasikini, dini, haki na usawa, na masuala mengine ndani na ulimwengu mzima kwa ujumla
Dizasta Vinna amekubalika kwa mashabiki kuanzia miaka ya 2012 alipoanza kwa kutoa wimbo wake wa kwanza unaofahamika kama “Harder” uliotengenezwa na Mocco na Laheel Paps, umahiri wake kwenye kuandaa maudhui ya kufikirisha ni kati ya vitu vinavyofanya ajizolee mashabiki ikiwemo wasanii wenzake.
Novemba 29, 2023 msanii nguli wa muziki wa Hip-hop nchini Farid Quband 'Fid Q' alipokuwa akijibu swali la mwandishi kuhusu wasanii wa rap anaowakubali kutokea Tanzania alimtaja Dizasta kama msanii namba moja.
“Namba moja yangu mimi ni Dizasta Vinna kwa sababu mimi napenda mtu anayeandika sana, Dizasta anazingatia peni zaidi” alisema Fid Q
Lakini sio Fid Q pekee amewahi kuonesha kukubali kipaji cha Dizasta, rapa kama Professor Jay na Mr Blue pia wamewahi kumzungumzia Dizasta kuwa ni miongoni mwa rapa wanaowakubali
“Lunya anafanya vizuri kwa sasa lakini huyu Dizasta ni mwisho,” alisema Mr Blue.
"Huwezi kuamini mambo ambayo ubongo una-solve have been tested couple na time madokta wanahofu linapotajwa jina langu marapa wanatokwa na povu mi ni ndovu ameshaprove ngosha na Proff,” alijibu Dizasta kupitia wimbo wake wa Nobody is safe 5 baada ya kupokea sifa kedekede kutoka kwa manguli wa rap nchini
Mapokeo ya Dizasta kwa sifa anapata kutoka kwa mashabiki na manguli wa Hip-hop bado ni kitu ambacho kinawashangaza watu wengi, licha ya kupata sifa kedekede bado amekuwa akiendelea na kusimamia misingi yake binafsi, kuwa yeye sio msanii anayependa umaarufu wa mitandaoni.
Hata hivyo, ukali wake kwenye uandishi unatajwa kutokana na tabia yake ya kupenda kusoma vitabu kwa ajili ya kujiongeze maarifa.
“Natazamwa kama mgongo wa kuegemewa kama chombo nikitegemewa na watoto lakin kwa ndani mimi ni mtoto pia, mtoto wa katikati njia panda kati ya ukweli na uongo ukubwa na udogo ” alizungumza Dizasta kupitia Intro ya album yake ya A FATHERS FIGURE
Aidha watu wengi hujiuliza msanii huyo anawezaje kuendesha maisha yake kwa kutegemea muziki wakati nyimbo zake adimu kupigwa kwenye vyombo vya habari, hana usimamizi (management), hafanyi shoo.
“Nina mashabiki ambao wananisapoti sana nikitoa album nawauzia kwanza kwa njia ya hard copy kisha nawawekea nyimbo kwenye majukwaa na mitandao mbalimbali ya kijamii napata stream za kutosha” alisema Dizasta kupitia mahojiano yake na Clouds Fm
Mpaka sasa Dizasta ana album tatu ikiwemo The Verteler, Jesusta, na A FATHER Figure na ndiye msanii pekee Tanzania mwenye sequels zaidi ya moja ambazo ni (HATIA, COMFESSIONM NA NOBODY IS SAFE) yote hayo ameyafanya kabla ya kufikisha miaka 30, bila kuwa na usimamizi, bila msaada na bila kuwa na mkataba kwenye studio ya kurekodia.