Ukweli kuhusu ndoa ya Mc Pilipili

Muktasari:

  • Ndoa yake iliwashangaza wengi na kuacha maswali kutokana na namna ambavyo Pilipili alikula kiapo chake mbele ya mchungaji kuwa tofauti na wengi walivyo tegemea.

Juni 29, 2019, mitandao ya kijamii na vyombo vya habari nchini vilitikisa kwa taarifa za mchekeshaji Emmanuel Mathias maarufu kwa jina la Mc Pilipili, alipoamua kuukacha ubachela na kusogeza jiko karibu kwa kufunga ndoa na mwanadada Philomena Thadey (Qute Mena).

Ndoa yake iliwashangaza wengi na kuacha maswali kutokana na namna ambavyo Pilipili alikula kiapo chake mbele ya mchungaji kuwa tofauti na wengi walivyo tegemea.

Kama ilivyo kawaida ya taratibu za kufungiswa ndoa kanisani, Pilipili aliulizwa kama anampokea Philomena Thadey  kuwa mkewe kwenye shida, raha na magonjwa lakini cha kushangaza mkali huyu kwake ilikuwa tofauti, alikubaliana na baadhi ya vipengele alivyoulizwa isipokuwa njaa, shida na magonjwa.

Kiapo hiki cha namna yake alichokula Pilipili miaka mitano iliyopita wengi wamekikumbuka hivi karibuni baada ya kuibuka tetesi za ndoa hiyo kuvunjika, huku baadhi ya mashabiki kwenye mitandao ya kijamii wakiwa hawaelewi ukweli kuhusiana na jambo hilo.

Mc Pilipili amezugumza na Mwananchi Digital na kueleza hali halisi ya ndoa yake kwa sasa, ambapo amekanusha kuwahi kutengana na mkewe na kueleza kuwa wiki chache zilizopita walikuwa na matatizo kwenye ndoa yao lakini hayakufikia ukubwa wa mkewe kuondoka nyumbani kama wengi wanavyodai.

“Sisi tumeingia kwenye ndoa tukiwa vijana, changamoto zipo mimi na mke wangu kweli tulikua na changamoto lakini zimeisha, tulipopata changamoto sisi wenyewe tulikaa tukaongea yakaisha.

“Ambapo hatukufikia muafaka tulitafuta marafiki na watu wa karibu tukawaeleza wakatupa ushauri mzuri wa hekima, kwa sababu mtu unayeenda kumwambia kuhusu masuala yako ya uhusiano lazima awe na hekima na uelewa mkubwa.

“Tulipokuwa kwenye changamoto nilimtafuta Anthony Mavunde ambaye ni  Waziri wa Madini, Mc Luvanda, Mc Gara B na Masanja  Mkandamizaji nikawaelezea, wote hao ni ndugu zangu na tayari wapo kwenye ndoa,” alisema.

Pilipili anasema mgogoro wao kwenye ndoa ulidumu kwa muda wa wiki moja tu tofauti na tetesi zilivyokuwa zinasema, hivyo mkewe hakuwahi kuondoka nyumbani hadi pale ambapo waliweka sawa mambo yao.

Hata hivyo, baada ya kutokea kwa maneno ya kuvunjia kwa ndoa hiyo, zilisambaa video kwenye mitandao ya kijamii zikimuonesha kijana aliyejitambulisha kwa jina la Damson, akidai alikuwa akifanyishwa kazi nyumbani kwa Pilipili, hadi za kumfulia nguo za ndani lakini alikuwa akinyimwa chakula.

Kutokana na tuhuma za kijana huyo Pilipili, amesema kweli anamfahamu lakini kijana huyo alikuwa ni muumini wake kanisani.

 “Yule ni kijana ambaye alikuwa anakuja kanisani nilimkaribisha akaja hadi Dar es Salaam,  hakuwa na sehemu ya kukaa mimi nilikuwa na nyumba ya upendo ambayo nilikuwa nasaidia watu wasiyojiweza.
 
“Nikamuweka akakaa ameishi huko kwa muda mrefu, nikawa nimechukua nyumba nyingine Goba akawa anakaa huko, mimi nalipa kodi nanunua chakula na kila kitu, ni mtu ambaye alikuwa anakuja pia kwangu anasaidia kazi mbili tatu na siyo kufanyishwa kazi kama alivyoeleza.

”Hata anapokaa sasa hivi, kila kitu cha kwangu kwa hivyo yule ni picha ya wanadamu mimi sina ubaya naye nataka nikakae naye nimuulize nini ambacho kimetokea ,”alisema Pilipili.

Usikose kufuatilia muendelezo wa makala hii