Usher ataka kolabo na Nandy

Muktasari:

  • Jana Feb 7, 2024 Nandy kupitia ukurasa wake wa Instagram ameweka wazi kuwa msanii huyo wa Marekani naye anataka kufanya ‘kolabo’ ya wimbo wa 'Dah'.

Baada ya mwanamuziki wa Bongo Fleva Nandy, kufanya kolabo na Alikiba ya wimbo wake mpya unaotamba wa 'Dah', hatimaye wimbo huo umemfikia mwanamuziki wa Marekani Usher.

Jana Jumatano Februari 7, 2024 Nandy kupitia ukurasa wake wa Instagram ameweka wazi kuwa msanii huyo wa Marekani naye anataka kufanya ‘kolabo’ ya wimbo hupo.

Nandy 'ameshea' mazungumzo yake ya njia ya meseji za Instagram (DM) na Usher, yakionesha msanii huyo akieleza kuukubali wimbo huo, hivyo basi anahitaji kuweka verse yake katika ngoma hiyo.

Remix ya kwanza ya wimbo wa ‘Dah’ambayo Nandy alimshirikisha Alikiba bado inaendelea kushika namba moja kupitia mtandao wa YouTube, huku ukiwa na zaidi ya watazamaji milioni 2 ndani ya siku sita tangu kuachiwa kwake. Hivyo basi Usher akiingiza Verse zake kwenye ngoma hiyo itakuwa ni remix ya pili.

'Dah' ni wimbo ambao Nandy aliuandaa maalumu kwa ajili ya kuutumbuiza kwenye sherehe ya Haji Manara ya kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa na kumvisha pete ya uchumba, mke wake Zaylissa.

Kwa mara ya kwanza ulitumbuizwa Januari 18, kwenye sherehe hiyo ambayo ilihudhuriwa na watu mbalimbali maarufu.