Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vichwa vya Mondi, Nandy vyaongeza utamu bongoflevani

Muktasari:

  •  Yammi akiwa wa kwanza kusainiwa na lebo hiyo, ujio wake uliambatana na EP, ‘Three Hearts’ (2023) yenye nyimbo tatu ambazo hakumshirikisha msanii yeyote.

Waimbaji wa Bongofleva, Nandy na Diamond Platnumz ndani ya mwaka huu wamewatambulisha  wasanii wawili wapya ambao wamepokelewa vizuri.

Nandy kupitia The African Princess Label kamtambulisha Yammi, huku Diamond kupitia WCB Wasafi akimtambulisha D Voice, vichwa hivi vipya ndani ya Bongofleva kwa mwaka 2023 hadi sasa hakuna ubishi kuwa vimeupiga mwingi.

Utakumbuka Nandy na Diamond hawajawahi kushirikiana kimzuki, ila wamewahi kuwa na ukaribu, Nandy ndiye alifanya 'jingle' ya Wasafi Records, yaani kile kisauti cha kike kinachosikika mwanzoni mwa nyimbo zinazotoka chini ya Wasafi Records, ni cha Nandy.

Lakini vichwa hivi vipya walivyovitambulisha vimefanya yapi katika muziki kwa mwaka huu? Mashabiki wamewapokeaje? Kwa nini wao na sio wengine? Tunaenda kuangazia hilo kwa undani zaidi. 

1. Yammi & Nandy
Januari 20, 2023, The African Princess Label ilimtambulisha  Yammi akiwa wa kwanza kusainiwa na lebo hiyo, ujio wake uliambatana na EP, ‘Three Hearts’ (2023) yenye nyimbo tatu ambazo hakumshirikisha msanii yeyote.

Nandy alimuona Yammi akiwa anaimba nyimbo za wasanii mbalimbali katika mtandao wa TikTok na kuvutiwa na kipaji chake na kumchukua.

Nandy alikuwa na wazo la kufungua lebo tangu alipoachia albamu yake ya kwanza, ‘The African Princess’ (2018) chini ya Epic Records inayomilikiwa na Sony Music Entertainment, kampuni tanzu ya Sony Corporation of America.

Awali lebo hiyo ilikuwa inasimamia kazi za Nandy pekee na kumfanya kuwa msanii mkubwa akiwa namba kubwa kwenye majukwaa ya kidijitali, akishirikiana na wasanii wakubwa kama Koffi Olomide, kuanzisha tamasha lake na kushinda tuzo kibao za ndani na nje.

Baada ya kumtambulisha Yammi, ilimchukua Nandy zaidi ya miezi mitano bila kutoa wimbo wowote ili kuhakikisha nyota huyo  anafanya vizuri kimuziki.

Hadi sasa nyimbo za Yammi zilizofanya vizuri zaidi ni 'Namchukia', Tiririka' na 'Tunapendezana', huku video zake zikipata 'views' zaidi ya milioni 8.7 katika mtandao wa YouTube, na 'streams' zaidi milioni 17.5 Boomplay Music.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka kutoka Boomplay, Yammi ni msanii wa tatu wa kike Bongo kusikilizwa zaidi katika jukwaa hilo kwa mwaka huu akitanguliwa na Zuchu na Nandy.

2023  Yammi alipata fursa ya kujiunga na kampuni kubwa ya usambazaji muziki barani Afrika na India, ZiikiMedia ambayo ina ushirikiano na kampuni kubwa ya muziki duniani, Warner Music Group.

Kinachosubiriwa sasa ni kolabo ya mtu na bosi wake, pengine itakuwa mwakani baada ya mwaka huu Nandy kufanya kolabo na wasanii wenzake wawili wa kike, Mimi Mars (Pole) na Lulu Diva (Mtaalamu). 

Hata hivyo, Yammi kusaniwa The African Princess Label, haitoi uhakika wa kufanya kolabo na Nandy, mbona Mimi Mars alisainiwa katika lebo tena ya dada yake, Mdee Music lakini hadi Vanessa anatangaza kuachana na muziki hawakuwahi kushirikiana. 


2. D Voice & Diamond Platnumz

Novemba 15, 2023, WCB Wasafi ilimtambulisha msanii mpya, D Voice ambaye awali alifanya vizuri na wimbo wake wa singeli, Kuachana Shingapi (2021) aliyokuja kuwashirikisha Barnaba, Platform na Lody Music katika remix yake. 

Kabla ya D Voice, msanii wa mwisho kutambulishwa na WCB Wasafi alikuwa ni Zuchu hapo Aprili 2020 na ujio wake uliambatana na EP, ‘I AM Zuchu’ (2020) akiwashirikisha Mbosso na Khadija Kopa ambaye ni mama yake mzazi.

D Voice anakuwa msanii wa nane kutambulishwa na WCB Wasafi baada ya Harmonize (2015), Rayvanny (2016), Queen Darleen (2016), Rich Mavoko (2016), Lala Lava (2017), Mbosso (2018) na Zuchu (2020).

Kati ya hao, watatu tayari wamejitoa katika lebo hiyo ambao ni Rich Mavoko, Harmonize na Rayvanny, hawa nao wamekwenda kuanzisha lebo zao, Billionea Kid, Konde Music Worldwide na Next Level Music (NLM). 

Ikumbukwe WCB Wasafi ilianza kusaini wasanii mwaka 2015 huku Harmonize akiwa wa kwanza, alifanya vizuri na kushinda tuzo mbili kutoka African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) na African Entertainment Awards USA 2016 kama Msanii Bora Chipukizi. 

Utambulisho huo wa D Voice ndani ya WCB Wasafi uliambataba na albamu yake mpya, ‘Swahili Kid’ (2023) yenye nyimbo 10, huyu anakuwa msanii wa kwanza katika historia ya lebo hiyo kutambulishwa na albamu. 

D Voice amewashirikisha wasanii kutoka WCB Wasafi pekee ambao ni Diamond Platnumz, Lava Lava, Mbosso na Zuchu aliyesikika katika nyimbo mbili, ‘BamBam’ na ‘Nimezama’.

Nyota huyo baada ya kuachia video ya wimbo 'BamBam' akiwa na Zuchu, ndani ya wiki tatu tu imepata 'views' zaidi ya milioni 3.6 na kuifanya kuwa video yake ya pekee iliyotazamwa zaidi YouTube kwa muda wote.

Hadi sasa albamu yake, Swahili Kid (2023) imefikisha 'streams' zaidi ya milioni 8.8 Boomplay na Audiomack ikiwa na milioni 4.7, huku wimbo 'BamBam' aliomshirikisha Zuchu ukishika namba moja chati za Boomplay Top 100 Africa.
Nyota huyo  anatazamiwa kuja kufanya vizuri kama Zuchu hasa upande wa mauzo mtandaoni.

Ikumbukwe Zuchu alikuwa msanii wa kwanza Afrika Mashariki kupata wafuasi (subscribers) milioni 1 YouTube kwa mwaka mmoja, msanii wa kwanza wa kike Tanzania kupata 'views' milioni 100 YouTube na kwanza wa kike kufikisha 'streams' milioni 100 Boomplay.

Na hadi sasa Zuchu ukanda wa kusini mwa jangwa la Sahara, ni msanii wa kike namba moja kwa kuwa na wafuasi wengi YouTube.
Anashika namba tatu kwa kutazamwa zaidi katika mtandao huo, namba moja Afrika Mashariki kwa kusikilizwa zaidi Boomplay Music.