Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Huu hapa upande wa pili wa Dida usioufahamu

Muktasari:

  • Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa aliyekuwa mtangazaji wa Wasafi Media aliyekuwa akifanya kipindi cha Mashamsham marehemu Khadija Shaibu ‘Dida’ ambaye kabla ya kuingia kwenye ulimwengu wa Taarab alipenda muziki wa hip-hop na nyimbo za Kiingereza zilizopo kwenye mahadhi ya R&B

Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa habari, mara nyingi mashabiki hufikiri watangazaji hufanya kazi katika vipindi wanavyovipenda tu. Lakini, ukweli ni kwamba wapo ambao vipaji vyao hukuzwa na kuzalishiwa ndoto mpya licha ya awali kutamani kuwasilisha maudhui ya aina fulani.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa aliyekuwa mtangazaji wa Wasafi Media aliyekuwa akifanya kipindi cha Mashamsham marehemu Khadija Shaibu ‘Dida’ ambaye kabla ya kuingia kwenye ulimwengu wa Taarab alipenda muziki wa hip-hop na nyimbo za Kiingereza zilizopo kwenye mahadhi ya R&B.

Akizungumza na Mwananchi aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi ‘Radio Times’ Aman Misana amesema Dida ambaye awali alianza kufanya kazi Times Fm kabla ya Wasafi Media, uchangamfu wake ndiyo ulifanya apate kazi kwenye kituo hicho cha redio na kupewa kipindi cha Taarab kilichoitwa Mitikisiko ya Pwani.

“Inaweza kuwa 2003, Dida alikuja Times kama mwanafunzi wa ‘field’ alikuwa anasoma DSJ, akaripoti kwa Taji Liundi halafu akakabidhiwa kwangu  kumuelekeza kazi kwa hiyo nikawa nipo naye sasa kutokana na uchangamfu wake tukaamua kumchukua moja kwa moja.

“Lakini hakuwa mtu wa Taarab kabisa alikuwa anapenda sana Umarekani alikuwa anaimba nyimbo za huko na hata studio alikuwa hapigi Taarab alipiga za Marekani zile R&B za zamani na Hip-hop,”amesema Misana.

Licha ya hayo amesema kipindi hicho redio nyingi Dar es Salaam mchana zilikuwa zikipiga R&B na Hip-hop, hivyo alitoa wazo la kuanzisha kipindi cha Taarab kwa ajili ya akina mama.

“ Nilitoa wazo la kuanzisha kipindi cha Taarab, Taji alikubali tulianza kwa muziki mtupu kwa muda wa saa zima tukaenda kama mwezi baada ya hapo tukafanya tafiti tukaona mtaani kila nyumba wanasikiliza, tukaanza kujiuliza nani awe mtangazaji.

Huu hapa upande wa pili wa Didah usioufahamu

“Taji akapendekeza jila la Dida wakati huo yeye ndiye alikuwa msimamizi wa vipindi  akamwambia Dida anafaa, Dida akasema yeye na Taarab wapi na wapi, mimi nikamwambia yeye ni mtu wa Tanga najua watu wa huko hawawezi kushindwa kwa sababu Taarab ina mirindimo ya pwani, basi akasema atajaribu,” ameeleza Misana.

Amesema kutokana na ugeni katika kutangaza alilazimika kumsimamia Dida na kumfundisha hadi alipofahamu vizuri.

“Baada ya muda mfupi kile kipindi kikashika kasi, saa moja likawa halitoshi kampuni za simu zikadhamini tukaongeza muda, wakati huo kilikuwa saa 6 hadi 7 mchana tukaongeza hadi 8,  zikafanyika tafiti na kampuni iliyoitwa Steadman Tanzania Ltd iliyokuwa inahusika na tafiti za vipindi vya redio.

“Kipindi cha Dida kikaonekana kipo juu ikabidi tuongeze muda tena  hadi saa 9, tuliongeza tena hadi kipindi kikawa na jumla ya saa nne,” amesema.

Hata hivyo, amesema mwaka 2006 na 2007 kampuni iliyoitwa George Inc Ltd iliyokuwa ikitoa tuzo kwa Watangazaji na Vipindi Bora ilimtunuku Dida tuzo kwa miaka hiyo miwili kama Mtangazaji Bora wa Kike na Mitikisiko ya Pwani kikawa Kipindi Bora cha Burudani.

“Baada ya 2006 Taarab bado ikawa juu sana  Mzee Yusuph akawa anatamba, Dida alikuwa na desturi moja hawezi kupiga wimbo wa Taarab kama ni mbaya hata umpe hela akawa anachukua muda mrefu kupiga nyimbo za Mzee Yusuph, vikundi vingine vya Taarab vikaanza kulalamika kwamba anampendelea.

“Kipindi hicho mimi nimekuwa msimamizi wa vipindi nikamwita Dida tukaitisha kikao na vikundi vya Taarab tukawapa changamoto ikabidi watengeneze nyimbo nzuri hiyo ni moja ya mafanikio ambayo alifanya kuwahamasisha watoe nyimbo nzuri,”amesema Misana

Aidha aliongezea kuwa kutokana na tamasha la Mtaa kwa Mtaa ambalo lilikuwa linafanywa na Dida kutokana na kipindi chake cha Mitikisiko ya Pwani ndipo kipaji cha mtangazaji Dokta Kumbuka kilizaliwa.

“Baada ya Dida kumsikia Kumbuka kwenye tamasha alinifuata akaniambia bosi kuna mtu nimemuona tumchukue awe msaidizi wangu.

“Dida alivyokuwa anasikika kwenye redio ndivyo alivyo mcheshi sana, anapenda maendeleo, jasiri siyo muoga huwa haogopi ni mtu wa kujaribu na ndiyo maana hata alipoanza kipindi kilifanikiwa na hapo ndipo hata redio nyingine wakaamua kuweka vipindi vya Taarab,” amesema Misana

Utakumbuka kuwa Dida alifariki dunia Oktoba 4, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Mwili wake ulizikwa Oktoba 5  katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Awali alifanya kazi kwenye Redio Times na kisha miaka mitano iliyopita alihamia Wasafi Media ambako alikuwa akifanya kipindi kiitwacho Mashamsham