Wakosoaji walivyoibeba bendi ya TANCUT
Muktasari:
- Mashindano hayo yalikuwa makubwa sana na mpaka leo hayajawahi kufanyika mashindano ya bendi yenye ukubwa ule. Mashindano haya yalitayarishwa kwa ushirikiano wa CHAMUDATA, Radio Tanzania na Umoja wa Vijana wa CCM.
Dar es Salaam, Mwaka 1988 yalianza kufanyika mashindano ya bendi yaliyoitwa Top Ten Show, mashindano hayo yalifanyika mara ya pili mwaka 1989 na kilele kikawa mwaka 1990, bahati mbaya mashindano ya aina hiyo hayakuendelea tena.
Mashindano hayo yalikuwa makubwa sana na mpaka leo hayajawahi kufanyika mashindano ya bendi yenye ukubwa ule. Mashindano haya yalitayarishwa kwa ushirikiano wa CHAMUDATA, Radio Tanzania na Umoja wa Vijana wa CCM.
Radio Tanzania ilizunguka katika mikoa mbalimbali na bendi za huko zilifanya maonesho ambayo yalirushwa ‘live’ kila Jumamosi usiku kuanzia saa nne na hivyo kuwapa wasikilizaji nchi nzima nafasi ya kusikiliza na kufuatilia mashindano hayo katika hatua zote.
Miaka yote miwili nilishiriki mashindano haya wakati nikiwa mmoja wa wanamuziki wa bendi ya TANCUT Almasi Orchestra iliyokuwa na masikani yake mjini Iringa.
Mwaka 1989, masharti yalikuwa ni kila bendi ijitayarishe kwa nyimbo tatu, wimbo mmoja utungwe ukiwa na maudhui ya kuililia Afrika, ambao uliitwa Nakulilia Afrika, wimbo wa pili ulikuwa lazima utokane na wimbo asili wa kabila mojawapo la Tanzania na wimbo wa tatu uwe chaguo la bendi inayoshiriki mashindano.
Tulianza kufanya mazoezi makali ya nyimbo hizo. Marehemu Kasaloo Kyanga na pacha wake Kyanga Songa wakaja na tungo yao ya wimbo Afrika Nakulilia na mimi nikatoa mchango wa wimbo wa asili ya Kihehe ulioitwa Lung’ulye.
Baada ya mazoezi makali tulifanya onesho lisilo la kiingilio na kuwakaribisha wapenzi wa muziki wa dansi pale Iringa kuja kutoa maoni yao kuhusu matayarisho yetu. Mkuu wa Mkoa wa Iringa wakati huo Mama Chipungahelo alikuwa mgeni rasmi wa onyesho hilo.
Kilichofanyika pale siku ile kilikuwa si kitu ambacho naona kitawezekana kwa urahisi katika zama hizi. Baada ya kupiga nyimbo zetu tatu za mashindano, tuliruhusu wapenzi wa bendi yetu waliokuwepo kukosoa lolote lile ili waliloliona si sahihi kuhusu nyimbo zile, hakika kulikuweko maneno makali ambayo sidhani wasanii wengi siku hizi wangekubali kukosolewa vile.
Wapenzi walikosoa kuanzia mavazi, uchezaji na hata tungo zenyewe. Tungo ya Afrika Nakulilia iliyotungwa na akina Kasaloo ilikataliwa kwani ilionekana ilitokana na wimbo wa Pepe Kalle, hivyo muimbaji na mtunzi mwingine Kalala Mbwebwe na mpiga gitaa la solo Kawele Mutimwana wakaleta tungo nyingine ambayo ndiyo ilikuja kuwa moja ya kete zetu katika mashindano yale.
Baada ya kuvuka kigingi cha wapenzi wetu wa Iringa, tulikuja Dar es Salaam na tulikuwa tumepangiwa katika kituo cha ukumbi wa Silent Inn uliokuwa eneo la Mpakani Dar es Salaam.
Katika onesho hilo, bendi iliyotoka Sumbawanga iliyoitwa Rukwa International nayo pia ilitupa kete zake siku hiyo, Tancut tukaibuka kuwa katika bendi kumi bora na kuja kushiriki fainali za onesho lile zilizofanyika Uwanja wa Taifa.
Baadhi ya bendi zilizokuweko siku hiyo zilikuwa, Tancut Almasi, Super Matimila, MK Group, Salna Brothers, Varda Arts, Bima Lee, Kilimanjaro Band, Vijana Jazz Band, Mwenge Jazz Band na Maquis.
Siku ya fainali mwanzoni mwa mwaka 1990, nilikuwa nimekwishahamia Vijana Jazz Band, lakini kwa siku hiyo nilirudi bendi yangu ya zamani ya Tancut Almasi Orchestra kwani wakati wa mashindano nilishiriki katika bendi hiyo.
Wakosoaji walivyoibeba bendi ya TANCUT
Uwanja wa Taifa ulijaa wanamuziki wengi sana na kwa kuwa bendi zilikuwa na ustaarabu wa kuvaa sare, basi sare za aina mbalimbali zilitawala siku hiyo. Matokeo yalitangazwa na kila wimbo ulikuwa na mshindi wa kwanza mpaka wa kumi, washindi watatu wa kwanza wakipata zawadi mbalimbali.
Wimbo wangu wa asili ya Kihehe, ulishinda zawadi ya kwanza na washiriki wote tulipewa ‘radio cassette’ kutoka Ubalozi wa Uholanzi. Wimbo Afrika Nakulilia ulishika nafasi ya pili na wimbo uliokuwa chaguo la bendi ulikuwa Ngoma za Kwetu uliokuwa utunzi wa Kalala Mbwebwe ulichukua nafasi ya nne katika kundi lake, kwa ujumla matokeo yalikuwa mazuri sana kwa bendi ya TANCUT Almasi.
Katika nchi ambazo sanaa imekuwa, huwa kuna watu wanaoitwa ‘art critics’, hawa kwa kweli ni mabingwa katika fani za sanaa wanazo shughulikia na wao kazi yao moja kubwa ni kukosoa kazi mbalimbali za sanaa na hatimaye kuzipa grade.
Kwa mtizamo wa haraka haraka utaweza kudhani kuwa kukosoa kwao kunaweza kuharibu soko la sanaa husika, lakini kwa kuwa hawa watu huwa wakweli na wenye uzoefu.
Kupasishwa na watu hawa hupandisha thamani ya sanaa husika. Wakosoaji hawa pia huwafanya wasanii wawe makini katika kazi zao na hivyo ubora wa sanaa nzima unapanda. Kitendo cha bendi ya TANCUT kuruhusu kukosolewa kabla ya kuingia katika mashindano ilikuwa sababu moja wapo ya bendi kupata ushindi mnono katika mashindano yale.