Malembo: Huhitaji eneo kubwa kulima

Wakati ikielezwa kuwa zaidi ya vijana milioni moja huingia kwenye soko la ajira kila mwaka nchini kutoka shule za msingi, sekondari na vyuo, uwezekano wa vijana hao kuajiriwa kimekuwa kitendawili kikubwa.

Hata hivyo, wapo walioziona fursa na kujiajiri mijini.

Hivi karibuni, mwandishi wetu amezungumza na mmoja wa vijana aliyeona fursa za kilimo akiwa mjini.

Huyo si mwingine bali ni Lucas Malembo, aliyeanzisha kampuni ya Malembo Farm inayotoa ushauri wa kilimo na huduma za kiufundi katika sekta hiyo.

Swali: Ni changamoto gani wanazokabiliana na vijana hadi washindwe kujiajiri katika kilimo.

Jibu: Kwanza niseme, Serikali imekuwa na mikakati ya kuwahusisha vijana katika kilimo, ukiwemo mpango wa Building Better Tomorrow unaolenga kutatua changamoto, ikiwa pamoja na kuwapatia huduma za kijamii, utaalamu, mitaji na masoko.

Sasa tukija kwenye vikwazo, kwanza vijana wengi wanakosa maarifa na taarifa ya namna ya kufanya kilimo biashara. Katika eneo hili, kijana atajua jinsi ya kuendesha kilimo, taarifa za kisayansi, hali ya hewa na hata masoko.

Licha ya Tanzania kuwa na watumiaji wengi wa intaneti, lakini mtu akitaka kujua bei za mazao lazima aende sokoni kuangalia, wakati mtu anaweza kupata taarifa zote kupitia simu yake ya mkononi.

Leo hii ukimtumia dalali unalima nyanya, atakwambia leo hakuna bidhaa yoyote sokoni, labda mkulima yuko Tabora, yupo Kigoma, mwingine yupo Mtwara. Mara mnakutana wote sokoni kwa pamoja, na huko mlikotoka mmeacha mahitaji.

Lakini kungekuwa na taarifa kupitia mitandao ya jamii watu wangejua.

Pili, kuna tatizo la upatikanaji wa mitaji. Leo ili ufanye kilimo chenye matokeo, lazima uwe na mtaji wa kuwekeza, katika kupata maarifa na taarifa za uzalishaji, masoko.

Ukiangalia taasisi zetu za fedha hazina urafiki na wakulima wadogo wanaoanza. Wakati Serikali inasema kipaumbele ni kilimo, bado hakuna kipaumbele cha kuwawezesha vijana kufanikiwa kilimo.

Jambo la tatu, ni kwamba wakati Serikali inawataka vijana wajiajiri, kwenye uhalisia haipo hivyo.

Kuna changamoto pia ya masoko. Bado hatujafungamanisha mlaji, mzalishaji na masoko.

Hapa nashauri kuwasajili madalali ili watambulike kisheria na kuwawekea kiwango cha kuchukua cha juu kulingana na mazao aliyouza ili asimlalie mkulima.

Swali: Kwa hiyo kijana atawezaje kujiajiri katika kilimo licha ya changamoto zote hizi?

Jibu: Kwanza siyo lazima kijana awe na eneo kubwa ndio ajiajiri kwenye kilimo. Huku huku mijini walipokimbilia pia wanaweza kujiajiri kwenye kilimo.

Unahitaji eneo dogo tu na mtaji mdogo wa kuanzia ili uweze kufanya kilimo cha biashara.

Kwa mfano, mimi niko hapa Mwananyamala hapa nafuga kuku wa kienyeji zaidi ya 200, tumetengeneza mabanda ya ghorofa, tunafuga sungura hapa, mkojo wake ni biashara, tunafuga pia panya wanaotumika kwenye majaribio shuleni kwa wanafunzi wanapsoma masomo ya sayansi.

Tunafuga samaki kwenye eneo hili hili, tunaotesha miche ya mazao ya mbogamboga, kama nyanya, pilipili, michaichai, Sukuma wiki ambazo huvunwa hata kwa miezi mitatu.

Kwa hiyo kijana anaweza kujiajiri katika kilimo bila hata ya kuwa na ardhi kubwa.

Swali: Eleza jinsi kijana atakavyoanza na mtaji wake kununua vifaa hadi apate faida.

Jibu: Kwa mfano hiki chungu cha mmea kinauzwa Sh1,000 vikiwa 100 ni Sh100,000. Kwa hiyo unaweka udongo na mbolea unapanda mmea wako. Tayari hilo ni shamba baada ya siku kadhaa utakuwa unavuna mboga na unauza.

Fungu la sukuma wiki kwa Dar es Saalaam ni kati ya Sh400 hadi 500 na mahitaji yake ni makubwa, unaweza kuvuna na kuuza hata kwa miezi mitatu kabla ya kupanda tena.

Unaweza pia kununua mboga na matunda masokoni na kuuza mitaani.

Kijana pia anaweza kufanya biashara ya kusindika mazao ya kilimo kwa kutumia mashine ndogo. Kwa mfano kuna mashine za kutwanga kisamvu unafungasha kwenye vikasha na kuuza mitaani.

Kuna mashine zinazotengenezwa na Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) kama vile za kumenyea viazi vya chipsi na nyinginezo. Hizo zinaweza kutumia kujiingizia kipato.

Kwa wale vijana waliosomea kilimo na biashara na wamekosa ajira, wanaweza kujiajiri kwenye kutoa ushauri wa kilimo kwa kusajili kampuni, kwa sababu wakulima wengi wanaishi mijini na wanahitaji ushauri wa kilimo.

Mimi nimekuwa nikitoa elimu ya biashara ya kilimo kwa wafanyakazi wanaostaafu.

Swali: Kwenye ufugaji pia inaelezwa kuwepo gharama kubwa, je huko nako vijana wanaweza kuingia kirahisi?

Jibu: Ni rahisi tu kama kijana atakuwa na nia na malengo.

Kwa mfano kama kijana ataanza bata 100 kwa kununua bata mmoja Sh5,000, baada ya miezi sita ukiwauza kwa Sh15,000 kila mmoja atapata faida kubwa.

Unaweza pia kuuza nyama ya bata kwa kununua bata na kuwapaki kwenye vifungashio.

Kijana pia anaweza kujiajiri kutengeneza chakula cha mifugo hasa kuku na bata, kwa sababu vyakula vya nafaka ni bei ghali.

Kuna zalishaji wa magugu maji aina ya Azolla na majani ya fodder yanayozalishwa kwa mbegu za ngano, shayiri, mtama yanapunguza gharama kwa asilimia 50.

Kwa hiyo badala ya kununua vyakula vya mifugo kwa bei kubwa, unatumia mazao hayo na unapata faida mapema.

Swali: Majani ya fodder yanazalishwaje?

Jibu: Kilo moja ya ngano ni Sh1,300, ukiiloweka kwenye karai lenye mkojo wa sungura, inazalisha majani ya kilo sita hadi saba. Majani hayo yanaliwa na mifugo na yanaongeza unene na uzito.

Kuna magugu maji ya azolla, hayo ukipata mbegu unaiweka kwenye maji inaendelea kujiotea kwa miaka mingi. Ni chakula kizuri kwa kuku au bata na kinapunguza gharama ya kununua chakula kwa bei kubwa.

Unaweza pia kuzalisha chakula mwenyewe na kuuza. Nunua pumba, uduvi, damu na mifupa iliyosagwa na kuchanganya mwenyewe kisha unalisha mifugo au unauza kwa wafugaji.

Kuna kutengeza funza ambao wanaongeza protini kwa mifugo.

Hizo ni sehemu ya fursa za ajira ambazo kijana anaweza kuingia kwa mitaji midogo, eneo dogo na kujikuta anapata faida kubwa.