‘Msitumie Mwezi wa Ramadhani kujinufaisha’

‘Msitumie Mwezi wa Ramadhani kujinufaisha’

Muktasari:

  • Wafanyabiashara  mkoani Lindi ,wametakiwa kutokutumia mwezi mtukufu wa Ramadhani ulioanza leo, kupandisha bei kwa lengo la kutaka kupata faida kubwa kwakuwa kwa kufanya hivyo ni kuwaumiza wafungaji.

Lindi. Wafanyabiashara  mkoani Lindi ,wametakiwa kutokutumia mwezi mtukufu wa Ramadhani ulioanza leo, kupandisha bei kwa lengo la kutaka kupata faida kubwa kwakuwa kwa kufanya hivyo ni kuwaumiza wafungaji.

Rai hiyo imetolewa leo Jumatano, Aprili 14 na Mkuu wa Mkoa wa lindi, Godfrey Zambi  wakati akizungumza na wakazi wa Mji mdogo wa Masoko,kijiji cha Nanjirinji,wilaya ya Kilwa na Lindi, alipokuwa anazungumza na wananchi wa maeneo husika..

Amesema kitendo cha kuutumia mwezi mtukufu wa Ramadhan kupandisha bei ya vyakula kwa lengo la kujipatia faida kubwa ni dhambi na kinamchukiza Mwenyezi-Mungu.

“Wapo baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa na tabia potofu, ifikapo mwezi mtukufu wanapandisha bei ili mradi wapate faida kubwa,acheni mnamchukiza Mwenyezi-Mungu”Alisisitiza Zambi.

Zambi amesema kutokana na tabia hiyo ya kupandisha vyakula bei hata kama watakuwa wanaingia misikitini kuswali swala zote tano inakuwa ni kazi bure, kwani hawatakuwa wamepata thwawabu,

Zambi amewaagiza Wakuu wa Wilaya kulisimamia agizo hilo na wafanyabiashara watakaokwenda kinyume na agizo hilo hatosita kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kufunga biashara zao.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Soko kuu la mji mdogo masoko, Said Salum Litou, ameomba waboreshewa mazingira ya Soko lao ikiwemo kuondoa vibanda vilivyojengwa kwa miti na kuezekwa kwa plastiki  na waongezewe majengo ya matofali.

Naye Zambi akijibu malalamiko hayo amemuagiza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa,Renatus Mchau,kutekeleza malalamiko hayo mara moja,ili kuweka mmazingira ya Soko katika hali mzuri.