Taasisi za fedha, sekta binafsi zatakiwa kushirikiana

Thursday October 22 2020
taasis pic

Dar es Salaam. Taasisi za fedha zimetakiwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi ili kukuza mitaji yao na kuongeza ushindani wa kibiashara dhidi ya wenzao kutoka nje.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alitoa rai hiyo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa sekta binafsi waliohudhuria Mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) jijini Dar es Salaam.

Lengo la mkutano huo lilikuwa kumpongeza Rais John Magufuli kwa kuboresha sekta hiyo.

“Pamoja na ubora wa sera zinazoongoza sekta binafsi, bado Serikali tunaamini weledi kwenye utoaji wa huduma za fedha nchini ni nguzo muhimu katika kufanikisha ustawi wa sekta ya binafsi. Niomba benki zetu tusaidiane kwenye hili,’’ alisema mama Samia.

Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula alizipongeza taasisi za fedha nchini kwa namna zinavyoshirikiana na sekta binafsi katika kukuza mitaji ya wadau hao.

“Baadhi ya taasisi hizi zimekuwa haziishii katika kutoa mikopo tu, bali zimekuwa zikitusaidia kufanikisha mikakati yetu ikiwamo mikutano muhimu inayolenga kujadili fursa na mipango muhimu kwa ustawi wetum,’’alisema Ngalula.

Advertisement

Mkurugenzi mtendaji wa NBC, Theobald Sabi alisema benki hiyo imejipanga kushirikiana na sekta binafsi na Serikali ili kusukuma maendeleo.

Alisema Serikali imefanya kwa jitihada kwa kubuni sera ambazo zimeiwezesha sekta ya benki nchini kuwa imara zaidi licha ya changamoto za kiuchumi zilizotokana na athari za ugonjwa wa Covid-19, hatua ambayo imeziwezesha taasisi hizo kuendelea kutoa huduma kikamilifu bila kutetereka.

Subi alisema ustawi wa sekta binafsi nchini unategemea huduma bora za kifedha zinazoendana na mahitaji halisi ya wadau hao.

“Ndio maana Benki ya NBC tumekuwa karibu sana na wadau wa sekta binafsi si tu katika kutoa huduma bali kushirikiana nao kufanikisha mikakati yao mbalimbali kwa kuwa tunaamini kupitia ushirikiano na ukaribu huu; tunaweza kufahamu zaidi mahitaji yao hatua inayotuwezesha kubuni huduma zinazoenda sambamba na mahitaji yao,’’ alisema Sabi.

Advertisement