Ukitaka kujua maendeleo ya biashara ndogo, anzia viwanda

Maendeleo ya viwanda vidogo nchini yanatoa picha ya namna wafanyabiashara wadogo sana, wadogo na wa kati wanavyoendelea katika utekelezaji wa mipango yao.

Hii inatokana na ukweli kwamba viwanda vidogo sana, vidogo na vya kati vimepewa kipaumbele kikubwa na watunga sera miaka ya hivi karibuni ambayo Serikali inahamasisha na kusisitiza kuimarisha uchumi hasa kupitia sekta ya viwanda.

Hamasa inayotolewa miaka ya hivi karibuni ni ya aina yake tangu Tanzania ipate uhuru ikidhamiria kukuza uchumi ambao tayari umeingia daraja la kati pamoja na kuimarisha uzalishaji w andani ili kupunguza utegemezi kutoka nje.

Biashara ndogo sana, ndogo na za kati zinapatikana katika sekta zote na kuunda zaidi ya asilimia 90 ya biashara zilizopo nchini, katika sekta rasmi hata isiyo rasmi.

Msisitizo wa Serikali kwenye eneo hili umekuwa mkubwa kutokana na historia iliyohamasisha kutungwa kwa sera ya viwanda vidogo na vya kati, mahsusi kwa ajili ya kuisimamia na kuiwezesha sekta hii. Sera hiyo iliyoanza kuandaliwa tangu mwaka 2003 ipo kwenye hatua za mwisho za kupitia ili kuiboresha.

Ilianza kwa kuanzisha Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) mwaka 1973 ili kuviboresha viwanda vidogo nchini kuvifanya vya kisasa na vitakavyozalisha kwa tija kwa kuachana na teknolojia za kizamani katika uzalishaji wao.

Shirika hilo lina ofisi katika kila mkoa na ni mwamvuli wa kutegemewa katika sekta ya viwanda nchini. Wachambuzi wanasema Sido imefanikisha kuanzishwa kwa zaidi ya viwanda 100,000 vilivyotoa takriban ajira milioni moja kwa kuviwezesha kupata teknolojia bora na kuvilea kwa ujuzi na masoko.

Kuanzishwa kwa Sido na mpangilio wa majukumu yake kulifanyika mapema ili kujenga msingi wa viwanda nchini muda mfupi baada ya kuanzishwa kwa Azimio la Arusha lililosisitiza ujamaa na kujitegemea. Azimio hilo lilisema Tanzania haiwezi kuwa na viwanda iwapo vile vidogo sana, vidogo na vya kati havitoendelezwa.

Kufanikiwa na malengo kadhaa yaliyomo kwenye majukumu ya Sido kunajidhihirisha kwa namna tofauti, kulingana na utafiti uliowahi kufanywa. Lakini ukweli kwamba Tanzania inategemea kwa kiasi kikubwa bidhaa kutoka nje ya mipaka yake, mafanikio haya yanaweza yasionekane ila yapo. Ni kama vitani tu ambako jeshi linaweza kushinda mapigano lakini ikapoteza vita mwishoni mwa mapambano.

Sababu za kutoimarika kwa viwanda licha ya maendeleo yaliyopigwa katika sekta hiyo, yamewekwa kwenye kumbukumbu za wasomi na watafiti hata kuripotiwa kwenye Makala zilizoandikwa na kuchapishwa magazetini kwa miaka mingi.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba Tanzania isingekuwa nyuma kiviwanda iwapo viwanda vyake vidogo sana, vidogo na vya kati vingekuwa vinakua kadri miaka inavyokwenda. Kwa utaratibu huo sasa hivi vingekuwa vikubwa hivyo kukidhi mahitaji ya bidhaa ambazo Taifa linazihitaji hata kuiwezesha kuwa msafirishaji muhimu mwenye ushindani kwenye soko la kimataifa.

Licha ya msisitizo na hamasa inayotolewa na viongozi, ukweli ni kwamba viwanda hivi vidogo vimedumaa, shughuli zake hazikui katika namna yoyote inayoweza kuelezewa. Ukweli huo unazifanya biashar anyingine ndogo zilizopokwenye sekta ambazo hazipewi kipaumbele na Serikali kwa kutungiwa au kuboreshewa kuwa katika hali mbaya zaidi.

Mjadala wowote wa kuangalia namna biashara ndigi zinavyokua nchini au mapendekezo ya nini kifanyike kuweka mazingira mazuri kwa wajasiriamali wadogo yanapaswa kuangalia hatua zilizopigwa na wafanyabiashara wadogo na wa kati waliopo kwenye sekta ya viwanda ambayo inaangaliwa kwa jicho la ziada.

Hoja kuu katika mijadala hiyo inapaswa kuwa kushindikana kwa maendeleo ya viwanda vidogo nchini kuchochea ukuaji wa sekta nyingine hivyo kukuza uchumi kama ilivyotarajiwa. Mafanikio ya sekta hiyo bado hayajajidhihirisha vyema kwenye kilimo, kinachozalisha malighafi na kuajiri wananchi wengi zaidi nchini, na kukifanya kikue hivyo kuboresha maisha ya Watanzania. Kushindwa kuchangamana kwa sekta tofauti za uchumi ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo. Iwapo fumbo hilo litajibiwa, itafungua zaidi fursa ya wajasiriamali wadogo na wa kati kuchangia kwenye uchumi wa Taifa. Kwa sasa, mafanikio ya sekta moja hayajawa na mchangio mkubwa kwenye uchumi wa Taifa na wananchi kwa ujumla.

Hili linaonekana kwenye sekta ya huduma pia kama ilivyo kwenye madini na utalii hata mawasiliano na sekta ya biashara nayo.


Shughuli za Sido

Katika mwaka wa fedha 2021/22, Sido ilianza kujenga vizimba kwa ajili ya viwanda vidogo vya kusindika pamba, korosho na mafuta ya kula. Ujenzi wa vizimba hivyo, hotuba ya bajeti ya Wizara ya uwekezaji, Viwanda na Biashara inasema upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.Sido pia imeendelea kutoa teknolojia ya kisasa na kuwawezesha wajasiriamali kupitia vituo vyake vya uendelezaji teknolojia nchini kote. Shirika hilo limeviboresha vituo vyake vya teknolojia mkoani Kilimanjaro na Mbeya. Vituo vyake saba vilivyopo katika mikoa ya Kigoma, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha, Iringa, Shinyanga na Lindi vimefanikisha utengenezaji wa mashine 313 na vipuri 1,014 vilivyouzwa kwa wajasiriamali.

Vituo hivyo pia vinaendelea utekelezaji wa majukumu yake mengine hasa ya kukuza teknolojia na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wamiliki wa viwanda vidogo sana, vidogo na vya kati kote, mjini na vijijini katika utekelezaji wa mkakati wa kila wilaya kuwa na bidhaa yake pamoja na kuzibainisha na kuzitumia fursa nyingine zozote zinazojitokeza.