Wadau wataja mbinu 5 kukabiliana na mfumuko wa bei za vyakula

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikikabiliwa na kupanda kwa bei za vyakula, wadau wamependekeza hatua tano muhimu zinazopaswa kuchukuliwa kunusuru hali hiyo.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji visivyo na kilevi ulikua kwa asilimia 9.7 katika mwaka unaoishia Desemba 2022 ukilinganisha na ilivyokuwa Desemba 2021.

Ongezeko hilo ni kubwa zaidi ukilinganisha na mfumuko wa asilimia 4.9 mwaka mmoja kabla. Mfumuko huu wa bei unachangiwa zaidi na ongezeko la bei ya vyakula kwa sababu asilimia 28.2 ya bidhaa zinazotumika kuandaa mfumuko wa bei ni vyakula na ndio bidhaa zinazochukua nafasi kubwa zaidi.

Kwa mujibu wa NBS, mfumuko wa bei wa jumla ulikua asilimia 4.3 mwaka 2022 ukilinganisha na asilimia 3.7 mwaka 2021 na asilimia 3.3 mwaka 2020.

Ongezeko hilo lilisababisha haja ya Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd kuratibu mjadala kwa njia ya Twitter (Twitter Space) uliohusu ‘Nini kifanyike kudhibiti kupanda kwa bei za vyakula nchini’ ulioibua mbinu tano kuikabili hali hiyo.

Maoni hayo ya wadau yanakuja wakati ambao kuna ongezeko la bei za vyakula.Mathalan, gunia la kilo 100 la mchele linauzwa kwa wastani wa Sh312,921 ukilinganisha na Sh202,353 mwaka jana.

Gunia la maharage limefikia Sh318,947, ongezeko la asilimia 55 ya ile ya mwaka jana iliyokuwa Sh203,118 kwa mujibu wa ripoti ya bei za vyakula ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.


Mbinu tano

Akichangia mjadala huo uliofanyika juzi, mkulima ambaye pia ni Mkurugenzi wa Malembo Farms, Lucas Malembo alipendekeza mabadiliko katika sekta ya kilimo, akitaka kijikite kwenye teknolojia za kisasa.

Alisema pamoja na kwamba idadi kubwa ya wananchi ni wakulima, lakini asilimia 60 kati yao hutumia jembe la mkono, huku asilimia 10 hadi 12 ndiyo hutumia trekta na asilimia 24 wakitumia mkokoteni wa ng’ombe.

“Lazima tuangalie mbegu bora, afya ya udongo, mbolea na maji, kanuni bora za kilimo ikiwemo udhibiti wa magonjwa na wadudu.

“Mahindi tunatumia hekta milioni 6.07 kuzalisha lakini bado mahitaji ya mbegu bora na upatikanaji ni changamoto. Mahitaji ya mbegu bora ni tani 151,999 lakini usambazaji ni tani 41,000, pia wakulima watembelewe na maofisa ugani,” alisema.

Kutengenezwa kwa sheria rafiki za uwekezaji ni jambo lingine alilopendekeza, akisema zitashawishi uwekezaji wa viwanda na hatimaye nchi itazalisha zaidi, kuuza nje na kupata fedha za kigeni.

Kilimo cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua, alikitaja kuwa turufu nyingine itakayowezesha upatikanaji wa mazao ya kutosha na hivyo kukabili mfumuko wa bei za vyakula.

Ukame ni changamoto nyingine inayosababisha uchache wa mavuno, katika hilo alitaka mazao yanayostahimili hali hiyo yalimwe zaidi, vikiwemo viazi.

Alishauri ngazi ya familia iukabili mfumuko wa bei ya bidhaa za vyakula kwa kuwa na utaratibu wa kuweka akiba na kuepuka matumizi ya anasa.

“Mimi natoka kanda ya ziwa, chakula cha watu saba anapikiwa mtu mmoja, tunahitaji kubadilika,” alisema Malembo.

Maoni ya Malembo hayakutofautiana sana na Mkurugenzi wa Jukwaa la Wadau wa Kilimo (ANSAF), Audax Rukonge aliyependekeza kuimarishwa kwa teknolojia ya uvunaji wa maji ya mvua ili yatumike katika kilimo.

“Tuboreshe zaidi uvunaji wa maji ya mvua inayoendelea kunyesha kwa kuwa asilimia 90 inapotea haitumiki. Haya maji tuliyoyaona yatapotea, kuna haja ya kuboresha teknolojia. Tuvune maji ili tuyatumie kumwagilia,” alisema.

Sambamba na uvunaji maji, alitaka kuongezwa thamani ya mazao yanayozalishwa, jambo ambalo alisema litafanikiwa iwapo sekta binafsi itaimarishwa.

“Tuhamasishe vichocheo vya kikodi, huduma kama umeme, barabara vinawavutia kuwekeza kuhakikisha vyakula vinapatikana kwa wakati na kwa bei rahisi,” alisema.

Matumizi ya miundombinu ya kisasa ni hoja iliyoibuliwa na mdau wa kilimo, Mwaura Robert kama mwarobaini wa kupanda kwa bei ya bidhaa za chakula.

“Wakulima wadogo wanalima na roho zao wakiomba Mungu mvua inyeshe, wakulima wakubwa wanalima kwa umwagiliaji na kisasa zaidi. Wakulima wa Afrika Kusini wanatumia mbegu za kisasa na kilimo cha umwagiliaji tofauti na sisi, watu wawekeze katika kilimo kikubwa na tukiwa na mbegu za kisasa chakula kitaongezeka,” alisema Robert.

Mdau mwingine wa kilimo, Josephat Masanja alisema kuna haja kwa kila kaya kuzalisha chakula kwa kujitosheleza ili kupunguza mfumuko huo.

“Ili kaya iwe na utoshelevu inatakiwa kuzalisha chakula kwa asilimia 100 kwa mwaka mmoja hadi mwingine. Kaya itakayozalisha asilimia 0 hadi 99 haina utoshelevu,” alisema.

Alishauri maofisa kilimo wasiishie kwenye uzalishaji chakula, bali waingie pia kwenye matumizi ya kumwelewesha mkulima na kumsaidia katika familia yake.


Nini kimesababisha?

Mratibu wa kitaifa wa Mtandao wa Wadau wa Mazao ya Mikunde Tanzania (TPN), Zirack Andrew alihusisha kupanda kwa bei ya vyakula na vita vya Urusi na Ukraine.

Alifafanua mataifa hayo yanafanya biashara ya mazao ikiwemo ngano, hivyo kupungua kwake kunasababisha baadhi ya bidhaa, zikiwemo chapati kuongezeka bei.

“Lakini pia hizi nchi ni wazalishaji wa mafuta hivyo gharama zikipanda uzalishaji pia unapanda. Inachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la gharama, tangu vita ilipoanza wataalamu walishatabiri kwamba itachangia mfumuko wa bei kwa asilimia 17,” alisema Zirack.

Mtaalamu wa Lishe, Aneth Sisya alisema kupanda kwa bei ya chakula kunachagizwa na tabia za baadhi ya Watanzania kufungia bidhaa hizo ndani wakisubiri mfumuko.


Hifadhi ya chakula

Akizungumzia kuhusu hifadhi ya chakula, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Milton Lupa alisema, hifadhi iliyopo ina uwezo wa kuhudumia mwaka huu na hata mwakani.

Kulingana na mahitaji yaliyopo, Lupa alisema zaidi ya halmashauri 100 zinahudumiwa na wakala huo kwa sasa na kati ya Januari na Februari, idadi inatarajiwa kuongezeka.

“Tuna stock (hifadhi) kubwa sana, tunaweza kuhudumia mwaka huu na hata mwakani, wananchi wasiwe na wasiwasi. Tulianza na halmashauri chache lakini sasa zimefika zaidi ya 100,” alisema.

Kanda ya Kati, Ziwa Victoria, Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro aliitaja kuwa na mahitaji zaidi kwa sasa, huku Serengeti ikiwa na ahueni kwa kuwa mazao yameanza kukomaa.

Tofauti na ilivyokuwa awali, alieleza kwa sasa wakala huo unapeleka wenyewe chakula katika halmashauri kama ilivyoelekezwa na Serikali badala ya kuwapa wafanyabiashara.