Wakulima wadogo wanavyoubeba mkonge kwa kuongeza uzalishaji

Dar es Salaam. Haba na haba hujaza kibaba, methali hii inatosha kuelezea vyema namna wakulima wadogo wa mkonge walivyoongeza uzalishaji wa zao hilo karibia nusu ya uzalishaji wote wa kipindi cha nusu mwaka.

Hali hii ni tofauti na miaka ya nyuma ambayo wakulima wadogo huchangia kiwango kidogo kwenye uzalishaji, mfano; 2019 walichangia asilimia 24, 2020 walichngia asilimia 30, 2021 asilimia 24 kabla ya kupanda hadi asilimia 45 kwa nusu mwaka wa 2022.

Ripoti ya Nusu Mwaka ya Bodi ya Mkonge (TSB) inaonyesha wakulima wadogo (smallholders) wameongezeka kwa asilimia 53.6 kutoka wakulima 6,726 mwaka 2021 hadi 10,337 June, 2022.

Mchango wa wakulima wadogo kwenye zao hilo pia, umeongezeka mara mbili Zaidi kwa kipindi cha miezi sita ambapo tani 22,990 zilizalishwa kati ya hizo tani 10,337 zilizalishwa na wakulima wadogo ikiwa ni sawa na asilimia 45.

Wakati huo 2021 kati ya tani 39,484 za mkonge zilizozalishwa wakulima wadogo walihusika kuzalisha tani 9,434 sawa na asilimia 24.

Mwenendo huu wa kuongezeka kwa tija ya wakulima wadogo kwenye zao la mkonge ambapo awali takwimu zao zilikuwa chini, inalifanya gazeti hili lipate shauku ya kujua hali hii inasababishwa na nini.


Wakulima wadogo wafunguka

Jarufu Mbuma, Mkulima mdogo wa Mkonge anasema sababu iliyosaidia kundi lao kuongeza uzalishaji wa mkonge ni pamoja na mazingira wezeshi ya serikali hasa kwenye kukodishiwa mashamba ya zao hilo.

“Unajua zamani kilimo cha mkonge kilikuwa kinafanywa na matajiri tu, lakini sasa hivi kutokana na uwezeshwaji unaofanywa na serikali kupitia bodi ya mkonge wanaokodisha mashamba kwa muda wa miaka mitatu mitatu inatuwezesha hata sisi tusio na fedha kulima,”alisema.

Mbuma alisema uzalishaji wa zao hilo kwa wakulima wadogo umezidi kuongezeka kutokana na idadi ya wakulima hao kuongezeka mwaka huu ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Mwaka huu wakulima wadogo tumeongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma, wengi tumeingia kwasababu ya uhakika wa soko la zao hili ndani nan je ya nchi,” alisema.

Verediana Kambangwa, Mkulima wa mkonge mkoani Morogoro alisema uzalishaji umekuwa mkubwa kutokana na kufuata kanuni za kitaalamu za kuhudumia zao hilo ambazo amepewa na wataalamu.

“Wataalamu wanakuja huku shambani kutueleza jinsi ya kulima na hili linasababisha mavuno yetu wakulima wadogo yaongezeke. Mwaka huu natarajia kuvuna Zaidi yam waka jana naomba tu bei iwe nzuri,” alisema

Aidha, Verediana alisema changamoto kubwa inayowakabili ni mitaji finyu kwa wakulima wadogo.

“Tatizo letu la miaka yote, tunakosa fedha ya kutosha kwa ajili ya kupanua mashamba yetu ili na sisi tuwe na maeneo makubwa na uzalishaji uongezeke Zaidi,”alisema.


Bodi ya Mkonge

Gazeti hili lilifanya mahojiano na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona aliyesema sababu zinazoongeza tija ya wakulima wadogo kwenye zao hilo ni uwezeshwaji wa kifedha na zana za kilimo kwa wakulima hao.

“Bodi ya Mkonge inawawezesha wakulima wadogo Kwa kuwapatia utaalamu (elimu ya kilimo bora Cha Mkonge), kuwapatia mbegu bure na pia kuwakutanisha wakulima wadogo na mabenki na taasisi za Fedha ili kupata elimu ya fursa za uwezeshwaji kifedha,” alisema.

“Bodi imeanza kutenga Fedha kuanzia bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/2023 ili kununua mitambo ya kuchakata Mkonge wa wakulima wadogo (Makorona) ili tija na ubora uongezeke Zaidi kwa wakulima wadogo,”aliongeza.

Kambona alisema sababu nyingine iliyosababisha kuongezeka kwa idadi ya wakulima wadogo hasa vijana kwenye zao hilo ni pamoja na hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kuyagawa mashamba pori kwa bodi.

“Hivi karibuni Rais Samia alifuta hati za mashamba pori na kuelekeza kuwa baadhi ya mashamba hayo yawe chini ya Bodi ya Mkonge Tanzania ili yagawiwe Kwa wakulima wadogo kipaumbele kikiwa ni wanawake, vijana na wenye ulemavu,”alisema

Kuhusu mgawanyo wa mashamba pori hayo Kambona alisema “mpaka sasa zaidi ya ekari 6,000 zimegawanywa Kwa wakulima wadogo na Kati ya hao takribani ekari 3,000 zimegawanywa Kwa makundi ya vijana na nakadiriwa kuwa karibia vijana 6,000 wanajishughulisha na kilimo cha mkonge nchini,”

Licha ya kuwepo kwa soko zuri la dunia la mkonge, bado uhaba upo mkubwa huku takwimu za mtandao wa ‘Cognitive Market research’ zikionyesha kuna upungufu wa tani 300,000 Kwa Mwaka kwenye soko la dunia

Kwa mantiki hiyo, Tanzania ambayo inazalisha wastani wa tani 43,000 za mkonge inahitaji Zaidi ya tani 200,000 ili kuweza kukidhi mahitaji ya soko la dunia.

Ripoti ya mwisho wa mwaka ya Bodi ya Mkonge nchini ya 2021/2022 inaonyesha China inaongoza kununua mkonge wa Tanzania kwa asilimia 33.9 ikifuatiwa na Saudi Arabia kwa asilimia 17.2 na Nigeria ikinunua kwa asilimia 12.7

Umoja wa nchi za Kiarabu (UAE) wananunua asilimia 8.4 ya mkonge, Ghana asilimia saba, Morocco asilimia 6.5 na Hispania asilimia 3.8.


Wadau wa Kilimo

Mkurugenzi mtendaji wa Jukwaa huru la kilimo (Ansaf), Audax Rukonge alisema ongezeko la uzalishaji wa wakulima wadogo mara nyingi husababishwa na kuwepo kwa mashamba mapya yaliyoanza kuzalisha.

“Kuongezeka kwa uzalishaji wa wakulima wadogo kwenye zao lolote hii inaitwa ‘green field’ ambayo inaweza kusababishwa na kuongezeka kwa mashamba mapya ya zao husika,”alisema

“Mazao kama Mkonge, Korosho na Kahawa ni rahisi mkulima kuacha kuyalima kama bei hazivutii lakini endapo ukiona kuna ongezeko kubwa kama hilo (karibia nusu ya uzalishaji wote) labda bei inavutia wakulima,”aliongeza

Hata hivyo, Rukonge alishauri kuwa ni wakati wa kuacha kuuza mkonge na badala yake nguvu iwekezwe kwenye kuuza bidhaa za mkonge kwa ajili ya manufaa ya mkulima

Hata hivyo, ripoti ya ‘Tanzania in figures 2021’ inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha mauzo ya mkonge nje ya nchi yameongezeka kwa asilimia 15 mwaka 2021 ikilinganishwa na 2022.