Airtel yawatoa hofu wateja bei ya vocha za kukwangua

Muktasari:

  • Baadhi ya maeneo vocha zinauzwa Sh700 kutoka Sh500, na Sh1,500 kwa zile za Sh1,000.  

Dar es Salaam. Wakati bei za vocha za kukwangua zikipanda katika baadhi ya maeneo nchini, Kampuni ya Airtel Tanzania imezindua kampeni ya ‘Usilipe zaidi’ ikieleza wateja wake huduma hiyo haijapanda.

Kwa baadhi ya maeneo vocha za Sh500 zinauzwa Sh700 na zile za Sh1,000 zikiuzwa Sh1,500. 

Taarifa iliyotolewa na kampui hiyo Juni 6, 2024 imewaeleza wateja na umma kwa ujumla kuwa bei ya vocha zake za kukwangua hazijabadilika bei, hivyo wasilipe zaidi.

“Baadhi ya wateja wameripoti bei zimekuwa zikiongezwa tofauti na ile elekezi iliyoandikwa kwenye vocha, za Sh500 zimekuwa zikiuzwa kati ya Sh5,50 hadi Sh700, huku za Sh1,000 zinauzwa kati ya Sh1,100 hadi Sh1,500,” imeeleza taarifa hiyo.

Imeeleza bei hizo hazijaidhinishwa na Kampuni ya Airtel Tanzania au Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Mkurugenzi wa Masoko wa Airtel, Timea Chogo amesema ongezeko hilo ni kinyume cha mipango na taratibu zao.

“Tunathamini wateja wetu kupitia huduma na bidhaa tunazowapatia, ndiyo sababu leo hii tunawatangazia ‘Usilipe zaidi’ lengo letu ni kuwajengea uelewa kuwa ni haki yako kupatiwa huduma sawa na thamani ya pesa anayolipa,” amesema.

Kampuni hiyo imewataka kutoa taarifa kwa timu ya huduma kwa wateja haraka au kuwasilisha malalamiko kwa kutumia fomu ya malalamiko inayopatikana kwenye tovuti wanapouziwa bei kubwa.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi hivi karibuni akijibu swali bungeni kuhusu suala hilo alisema wameiagiza TCRA kuhakikisha watoa huduma hawapandishi bei kiholela, lazima wafuate utaratibu.

Alikuwa akijibu swali la nyongeza Mei 29, 2024 la mbunge wa Viti Maalumu, Tunza Malapo aliyehoji ni nini kauli ya Serikali kuhusu kupanda kwa bei ya vocha za kukwangua.