Prime
Bandari Dar yaandika rekodi mpya ongezeko la mizigo
Dar es Salaam. Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kushuhudia ongezeko kubwa la shehena ya mizigo, likiongozwa na magari, makontena na mizigo mingine inayohudumiwa, hali inayoakisi kuimarika kwa biashara na uwekezaji katika miundombinu ya bandari nchini.
Takwimu za utendaji za mwaka 2026 zinaonyesha kiasi cha mizigo kikiongezeka sambamba na idadi ya meli zinazoingia bandarini, hatua inayozidi kuimarisha nafasi ya Bandari ya Dar es Salaam kama lango kuu la biashara kwa Afrika Mashariki na nchi jirani.
Katika mizigo isiyo ya makontena inayohusisha usafirishaji wa magari, idadi iliyohudumiwa iliongezeka kwa asilimia 88 na kufikia 30,442 Mei, 2026 kutoka magari 16,177 katika kipindi kama hicho mwaka 2025. Idadi hiyo pia ni zaidi ya mara mbili ya magari 14,645 yaliyoshushwa Mei, 2024.
Sambamba na ongezeko hilo, meli za RoRo ziliongezeka hadi 20 mwaka huu kutoka 13 mwaka 2025 na tisa mwaka 2024, hali inayoonyesha kuongezeka kwa shughuli za uagizaji wa magari na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi.
Sekta ya makontena nayo imeendelea kuimarika. DP World imehudumia makontena 44,001 hadi Mei, 2026 ikilinganishwa na Makontena 27,953, mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 57.
Inaelezwa kuwa kiwango hicho ni zaidi ya mara tatu ya makontena 13,779 yaliyopokewa mwaka 2024.
Idadi ya meli za makontena pia imeongezeka hadi kufikia 20 kutoka 13 za mwaka 2025 na saba za mwaka 2024, jambo linaloonyesha kuongezeka kwa mzunguko wa biashara bandarini.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa amesema ongezeko hilo linaonyesha kuimarika kwa shughuli za biashara na hitaji la kuendelea kuboresha mfumo wa usafirishaji wa mizigo.
“Ukuaji wa RoRo, makontena na mizigo ya wingi unaonyesha kuongezeka kwa mzunguko wa mizigo katika mfumo wa bandari. Sasa tunalenga kuhakikisha kasi hii inaendana na uondoaji wa haraka wa mizigo pamoja na kuimarisha uhusiano wa bandari na maeneo ya ndani ya nchi,” amesema Mbossa.
Kwa upande wa mizigo ya wingi (dry bulk), amesema kiasi kiliongezeka kwa asilimia 27 na kufikia tani 267,560, Mei, 2026 kutoka tani 210,488 mwaka uliopita.
“Kiwango hiki ni zaidi ya mara tatu ikilinganishwa na mwaka 2024. Meli za mizigo hiyo ziliongezeka hadi nane kutoka sita za mwaka 2025 na tatu mwaka 2024,” amesema Mbossa.
Hata hivyo, amesema mizigo ya kawaida ilipungua kwa asilimia mbili hadi tani 204,978 kutoka tani 210,079 mwaka uliopita, ingawa bado ni kubwa zaidi ya tani 113,699 zilizoshughulikiwa mwaka 2024.
Amesema katika Kituo cha East Africa Gateway Terminal (EAGTL), makontena yameongezeka kwa asilimia moja na kufikia 85,243 kutoka makontena 84,127 ya mwaka 2025.
Kufuatia ufanisi huo, wadau wa sekta ya usafirishaji wanasema ongezeko hilo limetokana na uwekezaji mkubwa wa miundombinu, maboresho ya mifumo ya uendeshaji na ushiriki wa sekta binafsi.
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Meli Tanzania, Daniel Malongo amesema ushiriki wa waendeshaji binafsi umeongeza ufanisi wa huduma na kuimarisha imani ya wateja.
“Ushiriki huu umekuwa kichocheo kikubwa cha ongezeko la mizigo ambalo tumeendelea kulishuhudia katika miaka ya hivi karibuni,” amesema.
Amesema mipango ya Serikali ya kuongeza gati tatu mpya pamoja na kupanua maeneo ya kuhifadhi mizigo itaongeza uwezo wa bandari kuhudumia mizigo mingi zaidi na kuimarisha ushindani wake kikanda.
Katibu Mtendaji wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Liston Goodluck kwa upande wake amesema uwekezaji katika miundombinu ya bandari pamoja na ushiriki wa DP World na EAGTL umeboresha kwa kiasi kikubwa ufanisi wa huduma na kupunguza muda wa utoaji wa mizigo.
“Kadiri ufanisi unavyoongezeka, ndivyo wamiliki wengi wa mizigo wanavyoendelea kuchagua Bandari ya Dar es Salaam kwa sababu inatoa njia ya haraka na yenye uhakika ya kufikia masoko ya kikanda,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Bandari Kavu Tanzania (CIDAT), Meleck Shange amesema ongezeko hilo limechangiwa na maboresho ya miundombinu, ikiwamo uchimbaji wa kina cha bandari na uwekezaji katika vifaa vya kisasa vya kuhudumia mizigo.
Ametaja pia mfumo wa kidijitali wa TanESWS kuwa miongoni mwa sababu zilizorahisisha utoaji wa mizigo kwa kuunganisha wadau mbalimbali wa biashara.
Kwa mujibu wake, maboresho hayo yanaifanya Bandari ya Dar es Salaam kuendelea kuwa kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji wa mizigo katika Afrika Mashariki na Kati, huku matarajio yakiwa ni kuendelea kushuhudia ongezeko la mizigo na meli katika miaka ijayo.