Bei ya korosho yaongezeka sokoni

Muktasari:

Bei za korosho zimepanda sokoni ambapo katika mnada wa Chama Kikuu cha Ushirika (Tanecu) wakulima wameuza korosho hizo kwa bei ya juu Sh2,012 na bei ya chini Sh2,002 ikilinganishwa na bei ya mnada wa tatu ambayo ilikuwa bei ya juu ni Sh1,910 na bei ya chini Sh1,900.


Mtwara. Bei za korosho zimepanda sokoni ambapo Chama Kikuu cha Ushirika (Tanecu) kimeeleza korosho hizo kuuzwa kwa bei ya juu Sh2,012 na bei ya chini Sh2,002 tofauti na bei ya mnada wa tatu ambayo ilikuwa bei ya juu ni Sh1,910 na bei ya chini Sh1,900.

Oktoba 21 mwaka huu wakulima hao walikataa kuuza korosho zao katika mnada wa kwanza bei ya juu Sh2,011 na bei ya chini Sh1,630 huku mnada wa pili ukifanyika Oktoba 28 wa tatu kwa bei za juu Sh2,200 huku bei ya chini ikiwa ni Sh1,800 katika mnada wa nne bei ya juu Sh1,910 na bei ya chini Sh1,900 ambapo leo bei zimepanda Sh2,012 hadi Sh2,002.

Akizungumza baada ya wakulima hao kuuza korosho hizo Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Tanecu, Karim Chipola amesema kuwa katika mnada wa nne uliofanyikia wilayani Newala.

“Hizi bei hatufurahishwi kulingana na bei ya korosho lakini mazingira ya soko la dunia inatulazimisha kuuza. Bidhaa hii ina tabia ya kupanda na kushuka, tupeleke korosho kwenye ghala zetu,” amesema.

“Bodi imetuambia kuwa soko la dunia haikuwa sawa kama kungekuwa na ubabaishaji bodi wasingetuongopea. Tunajua mazingira sio mazuri katika uzalishaji na bei pia ili maisha yaendelee lazima tufanya maamuzi ya kupeleka korosho zetu kwenye vyama vya msingi,” amefafanua.

Mwakilishi wa Meneja Mkuu  wa Chama Kikuu cha Tanecu Sababu Juma  alisema kuwa chama hicho kilipeleka sokoni korosho tani 2,882 kwa bei ya juu Sh2,012 na bei ya chini Sh2,002.

Alisema kuwa chama hicho kiliuza korosho katika mnada uliopita ambapo tani 3,575  ziliingia sokoni zikiwa na thamani ya zaidi ya Sh6 bilioni.

Kwa upande wake Meneja wa Chama Kikuu cha Masasi & Mtwara Cooperative Union MAMCU, Biadia Matipa alisema kuwa leo wameuza korosho katika mnada wa nne  tani 8,900 kwa bei ya juu Sh2,010 na bei ya chini Sh1,850.