Biashara holela ya mahindi yawavuruga wafanyabiashara Holili

What you need to know:

Wafanyabiashara wa nafaka kutoka Tanzania kwenda nchi jirani ya Kenya, kupitia mpaka wa Holili, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, wamelalamikiwa kukiuka utaratibu wa kufanya biashara ya mazao hayo katika soko la kimataifa la nafaka la Holili.

Rombo. Wafanyabiashara wa nafaka kutoka Tanzania kwenda nchi jirani ya Kenya, kupitia mpaka wa Holili, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, wamelalamikiwa kukiuka utaratibu wa kufanya biashara ya mazao hayo katika soko la kimataifa la nafaka la Holili.

Imeelezwa kwamba badala yake huyaingiza na kufanya biashara moja kwa moja nchi jirani, hali ambayo inafifisha ajira na kuikosesha Serikali mapato. 

Utaratibu wa kufanya biashara katika soko la nafaka la Holili, ulitoa fursa kwa wafanyabiashara kutoka Kenya kuingia kununua mahindi katika soko hilo, hatua ambayo iliwezesha upatikanaji wa ajira na kuingiza pato la Serikali.

Wakizungumza leo Alhamisi Juni 8, 2023 kwa nyakati tofauti baadhi ya vijana wanaofanya biashara ndogondogo na ubebaji wa mizigo katika soko hilo, wamesema kwa sasa mawakala wa mahindi wanavusha mahindi moja kwa moja kwenda kufanya biashara upande wa Kenya.

Gustaph Joseph amesema hatua ya biashara ya mahindi kutoka Tanzania kufanyika Kenya  badala ya kufanyika katika soko la nafaka Holili, kunakosesha watu ajira na kuinyima Serikali mapato yanayotokana na magari ya Kenya kuingia.

"Kwa sasa gari za Kenya haziingii sokoni Holili kununua mahindi na badala yake kwa sasa soko limehamia Kenya, yaani magari ya Tanzania yanapita moja kwa moja kwenda Kenya, hii changamoto inasababisha watu kukosa ajira na Serikali kukosa mapato," amesema.

Priscus Moshi amesema, "Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) alishakuja hapa sokoni akatueleza hili ni soko la kimataifa na mahindi yaje hapa na wafanyabiashara wa Kenya wafike kununua hapa. Hata hivyo mawakala wamehamishia soko Kenya mahindi hayaingii sokoni kama ilivyokuwa maelekezo ya mwanzo," amesema.

Akizungumza Wakala wa Mahindi katika Soko hilo, Jabiri Mbaga amesema tatizo lililopo kwa sasa ni kupandishwa kwa gharama za ushuru unaotozwa na mawakala wa Clearance wa kuvusha mahindi kwenda Kenya kutoka Sh150,000 hadi Sh300,000 kwa gari ndogo huku gari kubwa ikifika Sh600,000.

"Hatujui tatizo ni nini maana hii inatuumiza mawakala na wafanyabiashara na imeshusha bei yetu ya mahindi, maana tulikuwa tunauza Sh1,050 kwa kilo lakini yameshuka hadi Sh1,010 kwa sababu ushuru kwenda nje umeongezeka hivyo wale wa Kenya wanapunguza bei ili kufidia ya kulipa ushuru," amesema.

Mfanyabiashara kutoka Kenya, Jackson Kasukumbandi amesema changamoto kubwa katika soko hilo ni kupandishwa kwa gharama za Clearence kwa upande wa Tanzania na kuomba hilo liangaliwe.

Akizungimzia malalamiko hayo Mkurugenzi wa Halmashari ya Rombo, Godwin Chacha amesema soko hilo huingiza Sh22 milioni kwa mwezi na kwamba halmashauri itakutana kwa dharura na wafanyabiashara pamoja na mawakala wanaohusika na uvushaji wa mahindi kwenda Kenya ili kushughulikia changamoto hizo na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka

"Tutakutana kwa dharura kushughulikia jambo hili kwa haraka kwani tunahitaji soko la Holili liendelee kuwa bora kwa wafanyabiashara na Taifa," amesema.