BoT, TADB wazindua mafunzo kuboresha ukopeshaji

Naibu Gavana Uthibiti na Ustawi, Sauda Msemo (katikati) akizindua kitabu cha programu ya udhibiti wa wataalamu katika ukopeshaji sekta ya kilimo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege na Naibu Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu (BOT Academy), Dk Ephraim Mwasanguti. Picha na Michael Matemanga.

Muktasari:

  • Mafunzo hayo yanatarajia kuongeza upatikanaji wa wataalamu wa ukopeshaji ambao wanahitajika kwa ajili ya kusaidia kuleta muunganiko wenye tija kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, wakopeshaji na wadau wengine katika sekta.

Dar es Salaam. Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na Chuo cha Benki Kuu (BoT Academy) wamezindua programu ya udhibiti wa wataalamu katika ukopeshaji sekta ya kilimo.

 Lengo la programu hiyo ya mafunzo, ni kuchochea upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kupitia ukopeshaji wenye tija.

Programu hiyo inatarajia pia kuongeza upatikanaji wa wataalamu wa ukopeshaji ambao wanahitajika kwa ajili ya kusaidia kuleta muunganiko wenye tija kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, wakopeshaji na wadau wengine katika sekta.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Naibu Gavana Uthibiti na Ustawi, Sauda Msemo, amesema benki na taasisi za fedha ni wadau muhimu wa mfuko wa dhamana kwa wakulima wadogo unaoendeshwa na TADB.

“Ukosefu wa utaalamu kwenye kubuni huduma, utoaji wa mikopo na kuvielewa viashiria hatari kwenye kufadhili miradi ya kilimo, vinaweza kuendelea kuwa kikwazo katika kutoa mikopo kwa miradi ya kilimo.

“Kujengewa uwezo kwa wataalamu wa fedha ili waweze kuwa na uwelewa mpana wa kilimo umeonekana kuwa ni jambo muhimu,” amesema Msemo.

Amesema katika kufanyia kazi suala hilo, BoT Academy kwa kushirikiana na TADB wamebuni programu hiyo ya mafunzo kwa ajili ya benki na taasisi za fedha zinazokopesha miradi ya kilimo.


“Hii itawawezesha kuwasaidia wakulima wadogo, vyama vya ushirika pamoja na wadau wengine wanaofanya kazi katika myororo mzima wa thamani wa kilimo,” ameongeza.

Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza wataalamu wabunifu, wavumbuzi na wenye uelewa mpana katika suala la ukopeshaji kwenye sekta ya kilimo.

Nyabundege amefafanua kuwa mafunzo yataongeza wataalamu kwenye taasisi za kifedha katika sekta ya kilimo, kubuni bidhaa na huduma rafiki kwa wakulima kwa kuzingatia vihatarishi vilivyopo kwenye ukopeshaji kwenye sekta hiyo.


Amesema kwa kufanya hivyo itasaidia pia kuleta uwekezaji zaidi kwa wakulima wadogo na wa kati.

“Programu hii ni hatua muhimu katika kuongeza utaalamu wa kiufundi na ubunifu kwa benki washirika wetu na taasisi nyingine za kifedha katika kukopesha sekta ya kilimo,” amesema na kuongeza…

“Mchango muhimu wa mafunzo haya ni kusaidia kuongeza uelewa wa utofauti wa mahitaji na mazingira ya ukopeshaji kwenye sekta yakilimo,” amesema.