CAG afukua madudu kibao

CAG afukua madudu kibao

Muktasari:

  • Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere jana ametekeleza agizo la kutoufanya ulimi wake kuwa na utata, akitoa ripoti inayofichua madudu kibao kwenye ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka 2019/2020.

Dodoma. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere jana ametekeleza agizo la kutoufanya ulimi wake kuwa na utata, akitoa ripoti inayofichua madudu kibao kwenye ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka 2019/2020.

Kichere ambaye Machi 28, 2021 aliambiwa na Rais Samia Suluhu Hassan asiufanye ulimi wake kuwa na utata, jana aliweka hadharani ripoti hiyo ya ukaguzi kwa kutumia saa 1:22 akifafanua kwa wananchi alichoita “taarifa fupi ya ukaguzi”.

Kichere katika ripoti yake alieleza matumizi mabaya ya fedha yaliyofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii, akitoa mfano wa shindano lililoitwa Kigwangalla Kili Challenge la mwaka 2019 lililolenga kuhamasisha watu kupanda Mlima Kilimanjaro.

Alisema alibaini shindano hilo lilitumia jumla ya Sh172 milioni huku Waziri wa Maliasili na Utalii, kupitia kwa kaimu katibu wake, akizielekeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Tanapa kufadhili shindano hilo wakati halikuwa kwenye bajeti yao.

Pia, alisema wizara hiyo ilikuwa na usimamizi usioridhisha wa Mfuko wa Tozo ya Maendeleo ya Utalii ambapo Sh6.875 bilioni zililipwa kutoka kwenye mfuko huo bila idhini ya ofisa masuuli kinyume na kanuni za fedha.

Mradi wa SGR

Kichere alisema kwenye mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), alibani kuwepo raia wa kigeni 1,538 walioajiriwa bila kuwa na vibali vya kazi na hivyo kuikosesha Serikali mapato ya dola za Marekani 1,538,000.

Alisema pia kuchelewa kumalizika kwa kipande cha kwanza cha SGR kama mkataba ulivyosema, kumesababisha Serikali kulipa riba ya dola za Marekani milioni 11.22.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere, CAG alisema ulikuwa na raia wa kigeni 46 ambao hawana vibali vya kufanya kazi nchini.

Alisema utekelezaji wa mradi huo haukufuata sheria inayotaka ufanyike upembuzi yakinifu na kwamba mradi huo unatumia upembuzi yakinifu uliofanywa katika miaka ya 1970 na 1972 na kampuni ya M/S Norconsult (ya Norway).

Alisema pamoja na kuhuisha vipengele vya taarifa ya upembuzi yakinifu miaka ya 1980, kuna ambavyo havikufanyiwa mapitio na kuhuishwa ambavyo ni utafiti wa kiuchumi na kifedha wa mradi, tafiti za kuwepo kwa maji na uendeshaji endelevu wa mradi.

Kampuni ya ndege

Kichere alisema ukaguzi wake kwenye Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) alibaini imetengeneza hasara kwa miaka mitano mfululizo na mwaka huu ilitengeneza hasara ya Sh60.246 bilioni. Kwa miaka mitano mfululizo imetengeneza hasara ya Sh153.542 bilioni.

Alisema alibaini kuwa Bodi ya Wakurugenzi haina mjumbe hata mmoja ambaye ana uzoefu kwenye masuala ya usafiri wa anga.

Kichere alisema wakati wa changamoto ya corona ndege nyingi zilikuwa zimesimama, lakini ATCL ilikuwa inatozwa gharama za ukodishaji bila kujali kwamba ndege zilikuwa hazifanyi kazi kutokana na corona.

Alisema ATCL imerithi madeni makubwa ambayo hutozwa riba, kwa mwaka wa fedha 2019/20 ATCL imetozwa riba ya Sh12.5 bilioni.

“Kutokana na madeni hayo, inakuwa vigumu kwa ndege za ATCL kusafiri kwenda nje ya nchi kwani zinaweza kukamatwa,” alisema.

Maeneo huru ya uwekezaji

Alisema mwenendo wa uwekezaji wa mitaji katika Kanda Maalumu za Uwekezaji (EPZA) alibaini kushuka kwa uwekezaji wa mitaji mipya katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2015/16 mpaka mwaka 2019/20.

Pia, alisema mwenendo wa uwekezaji katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) alibaini kushuka kwa idadi ya miradi inayosajiliwa na TIC katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015/16 mpaka mwaka 2019/20.

“Kwa mfano idadi ya miradi iliyosajiliwa na kituo mwaka 2015/16 ilikuwa ni 420, wakati katika kipindi cha mwaka 2019/20 ilikuwa ni 219, hivyo idadi hiyo ya miradi katika miaka hii imepungua kwa asilimia 48,” alisema.

Asilimia 15 ya bodi ya mikopo

Kichere alibaini katika mamlaka 35 za Serikali za mitaa kuna watumishi 3,038 waliokuwa wakipokea chini ya theluthi ya mishahara kutokana na ulipaji wa Mikopo ya Elimu ya Juu ambapo mnufaika hukatwa asilimia 15 ya mshahara.