CBT yamwaga neema kwa wabanguaji korosho Mtwara

Baadhi ya wabanguaji wadogo wakipewa mashine za kubangulia korosho na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanal Ahmed Abbas (wapili kulia) katika msimu wa pili wa korosho marathon. Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

  • Wabanguaji wadogo wapatiwa mashine 100 za kubangulia korosho ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha kuongeza ubanguaji nchini ambao kwa sasa  upo chini kwa asilimia 10.

Mtwara. Bodi ya korosho Tanzania (CBT) imetoa zaidi ya mashine 100 kwa vikundi 25 vya wabanguaji wadogo wa korosho ikiwa ni moja ya mikakati ya kuongeza ubanguaji wa korosho nchini ili kuweza kufikia asilima 60 ifikapo 2026.

Akizungumza wakati akikabidhi mashine hizo Mkurugenzi wa CBT, Francis Alfred alisema Serikali ina nia ya kuongeza ubanguaji hadi kufika asilimia 60 ifikapo 2026 na kuwanufaisha wabanguaji wengi.

“Tunafanya kampeni za kuhamasisha ubanguaji wa korosho kwa wananchi, wakulima na wabanguaji wadogo tatizo linalowakabili wengi ni kutokuwa na mashine za kubangulia na badala yake wanatumia mawe na vigongo,”amesema.

"ili kuwaboreshea vifaa ndio maana tulifanya marathon mwaka jana na tulipata Sh80 milioni ambazo tumenunua mashine za  kubangua korosho na za kufungashia  kwakuwa tulibaini kuwa wabanguaji wengi wanashindwa kutunza muda mrefu kutokana ukosekanaji wa mashine ,”aliongeza.

Alfred alisema Kwasasa asilimia 10 tu za korosho ndio zinaweza kubanguliwa kwa kuzingatia takwimu za mwaka ambapo tani 14,000 ya korosho kati ya tani 240,000 zilibanguliwa huku mwaka huu kukiwa na matumaini ya kufikia asilimia 20 ya korosho zote.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanal Ahmed Abbas alisema utolewaji wa mashine hizo ni chachu kwa vijana kwakuwa zimetengenezwa hapa hapa nchini hii inaweza kuwa ishara nzuri kwa mkoa wetu katika viwanda vya ubanguaji.

“Huyu mbunifu anafanya kazi kubwa ya kutengeneza mashine za ubanguaji niungane na Taasisi ya Jakaya Kikwete kwakuibua na kumtangaza niliona kwenye runinga, nikamtafuta nikapata nafasi ya kuonana nae ameonyesha furaha yake baada ya kuibuliwa na kutangazwa” alisema Kanal Abbas.