CRDB yaweka rekodi ya tuzo za taarifa

Muktasari:

 Kwa mara ya tatu mfululizo, Benki ya CRDB imetunukiwa tuzo ya uwasilishaji wa taarifa bora za fedha kwa upande wa taasisi za fedha kwa mwaka 2021 na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA), kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.


Dar es Salaam. Kwa mara ya tatu mfululizo, Benki ya CRDB imetunukiwa tuzo ya uwasilishaji wa taarifa bora za fedha kwa upande wa taasisi za fedha kwa mwaka 2021 na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA), kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa NBAA ulioambatana na maadhimisha ya miaka 50 ya taasisi hiyo.

Hafla hiyo ilifanyika Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na wataalamu na wabobezi wa masuala ya uhasibu kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi.

Akikabidhi tuzo hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu- Zanzibar, Jamal Kassim Ali aliipongeza CRDB kwa kuendelea kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa katika utayarishaji wa taarifa zake za kifedha, jambo ambalo limepelekea benki hiyo kuendelea kuibuka kinara.

Waziri Ali alisema kuandaa ripoti za mwaka za mashirika na taasisi za umma kwa viwango vya kimataifa kunazipatia mamlaka za usimamizi, pamoja na wawekezaji na wananchi fursa na uwezo wa kupima ufanisi wa utendaji kazi wa taasisi husika, kuona namna gani yanawajibika ipasavyo katika kusimamia rasilimali na mikakati ya uendeshaji.

Ofisa Mkuu wa Fedha CRDB, Fredrick Nsekanabo alisema benki hiyo inatambua umuhimu wa kuandaa taarifa za fedha kupitia mifumo inayozingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.

Alisema kitendo cha kupata tuzo hiyo kwa mara ya tatu mfululizo kunaifanya benki hiyo kuendelea kuongeza jitihada ili kuhakikisha inatoa taarifa zilizobora zaidi.

Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, Pius Maneno alisema CRDB imeibuka kinara baada ya kukidhi vigezo vyote vilivyowekwa na taasisi hiyo kwa zaidi ya asilimia 90.