Dijitali inavyobadili sekta ya bima nchini, fursa na changamoto zake
“Nikitaka kusafiri nakata bima kupitia simu, hiyo inanilinda muda wote wa safari, natumia simu sina haja ya kwenda kwa wakala wala ofisi ya bima,” anasema Joel Gize, mmoja kati ya watumiaji wa huduma za bima.
Anachokielezea Gize ni maisha ya wengi, hivi sasa ulipaji wa bima za vyombo vya moto, mali, maisha na afya umebadilika kwa kiasi kikubwa kuanzia namna na soko kwa ujumla.
Katika ulimwengu wa sasa teknolojia ya dijitali imefanya mapinduzi katika nyanja na sekta tofauti, imeendelea kutoa mchango mkubwa kwa kuongeza tija na ufanisi.
Kamishina wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), Dk Baghayo Saqware anasema ili kukumbatia fursa za kidijitali, mwaka 2022 walitoa mwongozo wa namna ambavyo wawekezaji, wafanyabiashara au wataalamu wa biashara wanaweza kutengeneza majukwaa ya bima kidijitali yatakayotumika kuuza au kununua bima kwa njia ya mtandao.
Anasema baada ya urasimishwaji kufanyika walijitokeza watu na sasa wanazidi kuongezeka, jambo ambalo anasema litasaidia mwitikio wa wananchi kutumia huduma za bima kutokana na urahisi wa kutumia na kupata huduma unaowekwa.
“Japokuwa bado njia zote za upataji bima zinatumika, ikiwemo kupitia mawakala au watu kwenda kwa kampuni ya bima, lakini mfumo wa dijitali umeongeza watumiaji ambao zamani walikuwa wanaona uzito kwenda ofisini au kwa mawakala,” anasema Saqware na kuongeza kuwa hata uelewa wa wananchi kuhusu huduma za bima umeongezeka.
Bosi huyo wa sekta ya bima nchini anasema hivi sasa watu wanapata huduma za bima kupitia vifaa vyao vya kidijitali, lakini pia imetoa nafasi kwa Tira kufuatilia kwa karibu shughuli za sekta na kutafutia suluhu changamoto zinazojitokeza.
“Lakini tunaona ni kitu kitakachokuza soko la bima, hii itaongeza ujumuishwaji katika sekta kwa sababu inagusa watu wote, wafanyabiashara, walimu, watu wa aina mbalimbali,” anasema Saqware.
Anasema uwepo wa majukwaa na huduma za bima kidijitali unaweka urahisi katika dhamira ya Serikali ya bima ya afya kwa wote ambayo inamtaka kila mtu awe na bima ya afya kwa kuanzia kabla ya kwenda katika bima nyingine kama ya maisha, mitambo.
“Hii ni moja ya namna ya urahisishaji wa upatikanaji wa bima ya afya kwa wote, baadaye majukwaa haya tutayatumia na kuomba wananchi wayatumie kupata bima,”
Miongoni mwa majukwaa ya bima yaliyosajiliwa mwaka 2022 ni M-Pesa Limited inayomilikiwa na kampuni ya Teknolojia ya Vodacom, wao wanasema ndani ya miaka miwili wamewafikia Watanzania takribani 400,000 ambao wanatumia huduma za bima, kama bima ya vyombo vya moto, bima za maisha na bima ya afya.
Meneja wa huduma za bima wa M-Pesa, Melchizedek Nyau anasema matokeo chanya yaliyoshuhudiwa ni kwa sababu ya urahisi wa kuwafikia Watanzania ambao wana uhitaji wa bima, lakini wanakwamishwa na changamoto ambazo majukwaa ya dijitali yamezitatua.
“Moja ya changamoto zinazotajwa katika ripoti mbalimbali ni urahisi wa upatikanaji wa huduma za bima. Kwa kawaida, inamlazimu mtu afike kwenye ofisi ya mtoa huduma kwa ajili ya kujisajili na kufanya malipo, ndipo aweze kupata huduma yoyote ya kibima, lakini kupitia teknolojia ya kidijitali ina nafasi kubwa katika kurahisisha upatikanaji wa huduma hizi,” anasema.
Anasema kutokana na changamoto za umbali, urasimu wa kupata nyaraka zinazohitajika pamoja na muda, wengi wamekuwa wakishindwa kufika na kufanya usajili huu, lakini sasa wengi zaidi watafikiwa kwa urahisi na haraka.
“Imani yetu kubwa ni kwamba mfumo huu wa upatikanaji wa huduma kidijitali utatatua changamoto hii kubwa na kuwezesha Watanzania wengi kupata huduma hii ya bima,” anasema.
Anasema changamoto kubwa ya bima za kidijitali iliyobakia sasa ni elimu na kuhakikisha kwamba wateja wako tayari kuziamini kuwa watalipwa madai yao sawa na aliyenunua kwa njia za kawaida zilizozoeleka.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude anaunga mkono kuwa uwepo wa bima ya kidijitali unarahisisha ufikiaji wa watu na kuondoa ulazima wa wao kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika ofisi za bima husika.
Lakini pia anataja uwepo wa bima hizo kuwa unasaidia kuondoa upigaji ambao ulikuwa ukifanywa na baadhi ya mawakala ambao walikuwa wakitumia mfumo wa zamani wa makaratasi kujipatia fedha kutoka kwa baadhi ya wateja.
“Kwa sasa ni rahisi mtu kujua kama bima aliyolipia ina uhalali, ukiingiza namba zako za bima utaonyeshwa umelipa kiasi gani kwa muda gani, hiyo inakupa urahisi hata wa wewe kuhoji ikiwa taarifa zimekuja tofauti,” anasema Mkude.
Anasema hiyo ni tofauti na zamani ambayo ilikuwa ngumu kwa mtu kujua kama alicholipia kipo kama alivyokusudia.
“Hofu kubwa ilikuwa kwenye mfumo wa zamani, unaweza kuuziwa bima ikawa ‘fake’, kuna siku nililipia bima kwa wakala imeandikwa vizuri, lakini nikiangalia katika mfumo sioni kama nimekata, uzuri nilikuwa palepale nilimuuliza akawa anasema labda afanye mawasiliano, Sh118,000 ilienda bure,” anasema Mkude.
Anasema karatasi zinaweza kuwa bandia kuliko dijitali, jambo ambalo linafanya mifumo hiyo kuwa na uhalali mkubwa na kumpa mtumiaji uhakika wa kile anachokitumia.
Hata hivyo, alitoa angalizo kuwa ni vyema watumiaji wa bima wakawa makini katika kusoma vigezo na masharti vinavyowekwa na kampuni ili wajue endapo majanga yatatokea watasaidiwa vipi.
Mkurugenzi na Mshauri wa Utafiti na Uhusiano wa Kimataifa (ACISP), Dk Anselmi Ancellimi alisema majukwaa ya bima ya kidijitali yana uwezo mkubwa wa kuchochea fursa na ukuaji wa sekta hiyo.
“Dijitali inaongeza upatikanaji huduma za bima. Mfano mtu anaweza kununua bima hata mwisho wa wiki au siku za mapumziko ya kitaifa ambazo kwa kawaida ofisi za kampuni na mashirika ya bima zinakuwa zimefungwa,” anasema Ancellimi, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya bima.
Anasema dijitali katika bima imeongeza ufikiaji wa wananchi walio pembezoni na maeneo yasiyo na mawakala kama vijijini na kuongeza matumizi ya huduma mbalimbali, ambapo mwananchi anaona bidhaa tofauti za bima kupitia simu yake.
Ancellimi anasema fursa nyingine zinazopatikana ni kuongeza ajira kwa vijana wanaoshiriki katika kutengeneza na ku 'maintain' mifumo inayotumika na katika mifumo ya kidijitali.
“Kuongeza ufanisi wa utendaji, ikiwemo kulipa madai haraka, kupungua gharama za kupata (acqusition), kuhudumia (servicing) na kutunza (retaining) wateja. Kupunguza hasara, ikiwemo wizi na ubadhirifu (fraud) kwenye bima,” anasema.
Kuhusu kufanikisha malengo ya Serikali ya bima ya afya kwa wote, Dk Ancellimi anasema kwa kuwa inalenga kuwahudumia wananchi wote, hilo linawezekana endapo watawekeza kwenye mifumo ya teknolojia na dijitali katika mnyororo wa thamani (value chain) ya bima.
“Kuwapa wananchi uthibitisho rahisi wa bima kama kadi ya kidijitali, QR codes, tokeni, na kuhakikisha matumizi sahihi ya bima za afya kwenye vituo vya kutoa huduma za afya kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za rufaa,” anasema.
Kwa nini bima za kidijitali sasa
Akizungumzia suala hilo, Mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora anasema kukua kwa majukwaa hayo kunatokana na kuwapo sera nzuri na msukumo mkubwa wa bima uliowekwa siku za hivi karibuni ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita.
“Dijitali inafanya kazi vizuri sehemu ambayo sera ni nzuri na zinaiwezesha bima kufanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa. Serikali iingie na sekta nyingine na ifanye kama kilichofanyika katika bima ili kuleta ushindani,” anasema Profesa Kamuzora.
Mtaalamu wa Uchumi na Kodi, Dk Balozi Morwa ambaye ni mmoja wa watumiaji wakubwa wa bima mtandaoni, anasema ukuaji wa majukwaa hayo unachangiwa na uharaka wao katika kuwakumbusha wateja ikiwa bima zao zinakaribia kwisha, tofauti na zamani ambapo hakuna mtu alikuwa anamkumbushwa mwenzake.
“Ikibaki mwezi mmoja tu unapigiwa simu kukumbushwa kuwa bima yako inakaribia kwisha, ikiisha huna haja ya kwenda, unalipia mtandaoni na hata ukitaka uletewe nyumbani unaletewa tofauti na zamani, hawa wanajali sana wateja,” anasema Dk Morwa.
Anasema pia uwepo wao kidijitali unaweka ugumu katika ukwepaji wa kodi, jambo ambalo linafanya Serikali kuwa na uhakika wa kukusanya mapato kutoka kwao na mfuko kutuna.
“Ningependekeza bima zote zikatwe kidijitali, hii itasaidia kuongeza mapato ya Serikali na kuondoa ukwepaji wa kodi, itolewe tamko maalumu kuwa kuanzia tarehe fulani bima zote zitakuwa kidijitali, ikiwemo ya maisha, biashara, makazi,” anasema Dk Morwa.