Kamati ya Bunge yaitaka Ewura kumlinda mteja kwenye bei za gesi, mafuta na maji

Muktasari:

  • Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaj na Mitaji ya Umma (PIC), imeagiza ujenzi wa barabara ya Ngorongo huku Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetakiwa kuhakikisha inamlinda mlaji kwenye bei za gesi, mafuta na wanaobambikiwa bili za maji.

Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), imeiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kuhakikisha inamlinda mlaji kwenye bei za gesi, mafuta na wanaobambikiwa bili za maji
Pia, PIC imeagiza Serikali kujenga barabara kwenye Hifadhi ya Ngorongoro yenye urefu wa kilometa 83 ili kukuza utalii.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jerry Silaa ameyasema hayo leo Jumatano Januari 24, 2023 baada ya kuchambua ripoti za Msajili wa Hazina kuhusu Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Ewura kwa kushauri mambo kadhaa ili kuboresha utendaji wa taasisi hizo.
Silaa amesema kamati yake imeiagiza Ewura kuhakikisha inamlinda mlaji kwenye bei za gesi, mafuta na maji.
Pia, kamati hiyo imewataka Ewura kuongeza nguvu kwenye elimu kwa sababu  wako wananchi wengi wanaolalamikia kubambikiwa bili za maji, lakini wanatakiwa kujua kuwa Mahakama ya bili za maji ni Ewura.
“Watoe elimu kwa wananchi ili wawasilishe malalamiko yao na wajue kitendo cha kusoma mita kisiwe siri bali wananchi washirikishwe,” amesema.
Hali kadhalika, kamati hiyo imeipongeza Ewura kwa kuibuka kuwa taasisi ya mfano barani Afrika kwa ufanisi.
Kuhusu Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Silaa amesema taasisi hiyo ni miongoni mwa taasisi zilizokumbwa na athari za Uviko-19, ambapo mwaka 2018/19 walikusanya Sh142.5 bilioni lakini mwaka 2021 mapato yalishuka hadi Sh99.5 biiloni.
“Filamu ya Royal Tour imesaidia kwa kiwango kikubwa kwani kwa mwaka 2022/23 wamekusanya Sh98 bilioni huku lengo likiwa ni Sh148 bilioni hivyo watavuka lengo,” amesema.
Hata hivyo, amesema kamati yake imewataka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuandaa mazingira rafiki ya utalii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya kilomita 83, waliyopatiwa kibali cha ujenzi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) cha kuijenga kwa kiwango cha zege.
Amesema kibali hicho cha Unesco kinamaliza muda wake Desemba 2023 na hivyo wanaishauri Serikali na Ngorongoro kwa kuwa barabara hiyo ni chanzo kikubwa cha mapato ijengwe. Gharama za ujenzi ni Sh160 bilioni.