Kampuni tano mbioni kuwekeza sekta ya madini

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeanza majadiliano na kampuni tano mpya kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ya madini.

Endapo majadiliano hayo yatafanikiwa, Tanzania itakuwa na jumla ya Kampuni 16 zenye mitaji mikubwa, zikiwamo tisa ambazo zimewekeza katika sekta hiyo ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Tayari majadiliano yameshaanza na kampuni hizo tano, lakini nisingependa kueleza hatua zozote katika majadiliano hayo,” amesema Waziri wa Madini, Dotto Biteko leo Mei 23, 2023.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelekea Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini, Oktoba 25-26 mwaka huu likihusisha mataifa 25.

Aidha, Biteko amesema makongamano hayo yamekuwa na manufaa kwa taifa ikiwamo ushawishi wa kampuni tatu zilizoingia mkataba hivi karibuni na Serikali katika uchimbaji wa madini mkakati.

Kampuni hizo kutoka Australia zilisainia miradi yenye thamani ya dola milioni 667 ni Evolution Energy Mineral, EcoGraf Limited na Peak Rare Earths, ambazo zinasaidia pia katika juhudi za kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.