Kapinga aitaka FCC kuharakisha utafiti wa biashara ya kidijitali
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga akizungumza na wadau wa biashara wakati akifunga rasmi maadhimisho ya Siku ya Haki za Mlaji Duniani hafla Iliyofanyika Dar es Salaam leo.
Muktasari:
- Utafiti huo mahususi kwa soko la biashara ya mtandao unaolenga pia wazalishaji, matokeo yake yatasaidia kuimarisha ulinzi wa mlaji kupitia uamuzi wa kisera, kisheria na kitaasisi kwa kuzingatia haki za pande zote.
Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameiagiza Tume ya Ushindani (FCC) kuharakisha na kukamilisha utafiti wa soko la biashara ya kidijitali nchini ili kusaidia maamuzi ya kisera na kisheria.
Akizungumza Dar es Salaam leo Alhamisi Aprili 2, 2026 wakati wa kufunga maadhimisho ya Siku ya Haki ya Mlaji Duniani ambayo kitaifa yamefanyika jijini humo, Waziri Kapinga amesema kukamilika kwa utafiti huo kwa wakati kutaisaidia Serikali kuandaa sera zinazoendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa.
Amesema utafiti huo unaofanywa na FCC katika soko la biashara ya mtandaoni, ikiwemo sekta ya wazalishaji, utachangia kuimarisha ulinzi wa mlaji kupitia mifumo ya kisera, kisheria na kitaasisi.
Kapinga amebainisha kuwa licha ya juhudi zinazoendelea za udhibiti, uelimishaji na tafiti mbalimbali pamoja na uchunguzi wa huduma za vifurushi vya intaneti, bado kuna haja ya kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya bidhaa bandia sokoni.
“Kulinda masilahi ya watumiaji kunahitaji uwazi wa bei, ubora wa huduma na ushindani wa haki. Ni lazima mjipange upya na kutekeleza majukumu haya kwa ufanisi zaidi,” amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, taasisi hiyo ilitoa elimu kwa umma kuhusu haki za walaji na kushughulikia changamoto mbalimbali, ikiwemo mikopo ya huduma za kifedha maarufu ‘kausha damu’.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga akizungumza na wadau wa biashara wakati akifunga rasmi maadhimisho ya Siku ya Haki za Mlaji Duniani hafla Iliyofanyika Dar es Salaam leo.
Amesema FCC inaendelea kupitia mikataba ya mikopo hiyo, ikiwemo viwango vya riba na masharti yake, ili kuhakikisha haki za walaji zinalindwa kisheria.
“Hatua kama hizi pia zinachukuliwa katika sekta ya bima ili kuhakikisha usawa kati ya watoa huduma na watumiaji,” amesema.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Mbwasi, amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kuimarisha taasisi na kukuza ushindani wa haki.
“Tutaendelea kusimamia utekelezaji wa sera na sheria ili kuhakikisha bidhaa ni salama na kuimarisha mapambano dhidi ya bidhaa bandia,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa FCC, Dk Aggrey Kalimwage, amesema maboresho ya sheria yameipa Tume hiyo nguvu zaidi ya kulinda haki za walaji.
Amesema kila mwananchi ana haki ya kupata bidhaa salama na kuahidi kuwa FCC itaendelea kusimamia uwajibikaji katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kimazingira.