VIDEO: Mbowe asimulia alivyokamatwa, kupewa kesi ya ugaidi

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiagana na makada na wanachama wa chama hicho waliomsindikiza nje ya hoteli aliyofikia katikati ya jiji la Mwanza. Mpigapicha Wetu.

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe leo amefichua namna alivyotolewa Mwanza kupelekwa Dar es Salaam kisha kutuhumiwa kuhusika na ugaidi alipokuwa akizungumza na wanachama na wananchi waliofika kwenye uzinduzi wa mikutano ya hadhara ya chama hicho jijini Mwanza.

Mwanza. Leo Jumamosi, Januari 21, 2023 Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amewasimulia wakazi wa Mkoa wa Mwanza na mikoa jirani waliohudhuria ufunguzi wa mikutano ya hadhara ya chama hicho uliofanyika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza namna alivyochulkuliwa ‘kinyemela’, kutoka Mwanza hadi kufikishwa Dar es Salaam kisha kufunguliwa mashtaka ya ugaidi.

Akiwaadhithia wananchi hao Mbowe amesema akiwa msibani kwa kaka yake Kilimanjaro Julai, 2021 alisikia Dk Azaveli Lwaitama na Mzee Sylivester Masinde mmoja kati ya waasisi wa chama hicho kuwa wameshikiliwa na jeshi la polisi mkoani Mwanza na kulazimika kuondoka msibani (Kilimanjaro) na kuja hadi Mwanza kwaajili ya kuwatoa mahabusu.

Chadema yakiwasha Mwanza, Mbowe achukizwa 'kulamba asali'

“Nilivyotua Mwanza kuwatoa rumande, siku ya kwanza, siku ya pili nikakamatwa mimi nikafungwa vitambaa machoni, nikafungwa pingu miguuni, nikafungwa pingu mikononi, nikasafirishwa mazingira nisiyoyajua napelekwa wapi? (alijiuliza), nikapelekwa Dar es Salam na ndio kesi yangu ya ugaidi ikaanzia hapo,”amesimulia.

“Ndugu zangu wa Mwanza nazungumza mambo haya mnaweza kuyaona kama mambo mepesi lakini mimi kama Mwenyekiti wenu kesi ile ikapelekwa miezi nane, asanteni ndugu zangu wa Mwanza na dunia inasikiliza kwa sababu wote mlisikiliza na mkasimama mkasema ‘Mbowe sio gaidi’,”amesema

Hatahivyo, Mbowe na wenzake watatu walifutiwa mashtaka yote yaliyokuwa yakiwakabili katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Machi 4, 2022 baada ya upande wa Jamuhuri kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo.