Majani ya karafuu kuzalisha mafuta tani 100 Zanzibar

Monday April 05 2021
karafuu pc
By Jesse Mikofu

Unguja. Imeelezwa kuwa huenda Zanzibar ikawa inazalisha tani 100 za mafuta ya karafuu kwa mwaka baada ya Kampuni ya Indesso kutoka Indonesia kubaini uwezo wa visiwa hivyo.

Akizungumza wakati wa kufungua ofisi ya kampuni hiyo mjini Unguja, Mkurugenzi wa Indesso Tanzania, Feri Agustian Soleh alisema kutokana na ushirikiano uliopo, Zanzibar itapiga hatua kubwa.

“Tumeanza kuthibitisha hii kwa uzalishaji wa CLO (mafuta) wa mwaka wa kwanza wa tani 3.2 zenye thamani ya zaidi ya Sh51.7 milioni,” alisema Soleh.Alisema wakati wanaanza shughuli hiyo, walilenga kuzalisha tani tatu kwa mwaka kwa kutumia kinu (kiwanda) kimoja, lakini wamevuka lengo hilo na kufikia tani 3.2 tangu kuanza uzalishaji huo mwaka jana Mgelema kisiwani Pemba.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Dk Islem Amed alisema Serikali itaendelea kutengeneza sera na mazingira mazuri kuhakikisha inawavutia wawekezaji wengi na kufikia ndoto za uchumi wa bluu.

Pia, alisema kuanzishwa kwa uzalishaji huo ni jambo la kushirikiana maana linamgusa kila mwananchi kuanzia ngazi ya chini.

“Huu ni mradi unaowagusa wananchi wa chini kabisa, maana uzalishaji huu unatumia majani ya mkarafuu, kwa hiyo kila mwananchi anaweza kuokota majani hayo na kuuza bila shida yoyote akapata kipato,” alisema Amed.

Advertisement

“Lengo letu Serikali, tunataka viongezeke viwanda vifike 20, tutakuwa na uhakika wa kuzalisha tani 100 kwa mwaka.”

Waziri wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Amina Salim Ali alisema Indesso wamekamata soko la dunia na wanashika namba tatu hivyo iwapo watachangamkia fursa hiyo, wataipaisha Zanzibar kimataifa.

“Serikali haikubahatisha kuanzisha mradi huu, Zanzibar itapata maendeleo makubwa na kuimarisha uchumi wake kupitia mradi huu (uchumi wa bluu),” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC), Said Mzee alisema mradi huo utazalisha ajira nyingi na utaleta kipato si tu kwa Taifa bali kwa wananchi wa rika zote.

Aliwataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo ya kukusanya majani hayo yanayodondoka na kuliuzia shirika hilo kwa Sh150 kwa kilo moja.

“Ukiangalia hii (majani) ni malighafi iliyokuwa inapotea bure, lakini kwa sasa hatupotezi tena, karafuu na majani yake kwa sasa vyote imekuwa mali, huu ndio mpango hadi kufikia mwaka 2025 tunataka kuwa na vinu 25,” alisema Mzee.

Advertisement