Maonyesho ya Sabasaba kuja na ‘Expo Village’

Kaimu Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara wa Tantrade, Fortunatus Mhambe akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Mei 19, 2023, kuhusu maandalizi ya maonyesho ya biashara ya kimataifa ya Sabasaba. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), yatangaza uwepo wa jukwaa maalum (Expo village) litakalowawezesha wafanyabiashara kushiriki na kuonyesha bidhaa zao, katika Sabasaba mwaka huu.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), yatangaza uwepo wa jukwaa maalum (Expo village), litakalowawezesha wafanyabiashara kushiriki na kuonyesha bidhaa zao, katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) mwaka huu.

Taarifa zinaonyesha kuwa jumla ya mataifa 14 yamethibitisha kushiriki maonyesho hayo yanayokusudiwa kuanza Juni 28 hadi Julai 14 mwaka huu, ambapo kampuni 112 kutoka nje ya nchi na 1188 za ndani yamethibitisha kushiriki.

Kaimu Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara wa Tantrade, Fortunatus Mhambe amesema jukwaa hilo litatoa fursa kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kwa kuonyesha ubunifu na kushirikiana na wadau wengine wa sekta mbalimbali.

Mhambwe ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Mei 19, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maonyesho ya Sabasaba ya mwaka 2023 yatakayoanza Juni 28 hadi Julai 14.

"Kupitia jukwaa hili tunatarajia kuona ukuaji wa biashara, mauzo na kuimarisha uchumi wa nchi. Pia kutakuwa na Sabasaba Expo village itakayo toa jukwaa la kujenga mtandao kwa wafanyabiashara na kupata fursa ya kuanzisha mawasiliano na wenzao.

"Eneo hili litawavutia wageni kutoka nje ya nchi wakiwemo wa ndani ya nje ya wakiwemo wafanyabiashara na wawekezaji kuonyesha ubora wa bidhaa zetu. Katika Expo village kutakuwa na waonyeshaji kutoka sekta za madini, ujenzi, mazingira, vijana na wanawake," amesema Mhambe.

TanTrade ni taasisi ya umma yenye majukumu ya kuishauri Serikali kwenye masuala ya kuunda, kuendeleza, kusimamia na kutekeleza sera na mikakati za biashara nchini, kudhibiti na kutangamanisha maendeleo ya soko la ndani ya nchi na nje ya nchi.

Kwa upande mwingine, taasisi hiyo in majukumu ya kuzijengea uwezo jumuiya za wafanyabiashara juu ya namna bora ya kusimamia shughuli za biashara ya ndani na nje ya Nchi, kuanzisha.

Majukumu mengine ni kutunza na kuendeleza Kanzidata ya taarifa za biashara nchini pamoja na kuandaa na kuratibu maonesho ya Sabasaba, Maonesho ya Viwanda, misafara na mikutano ya Wafanyabiashara.