Mavunde: Sheria zilichelewesha Tanzania kuvuna sekta ya madini
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akizungumza mara baada ya kuzindua maadhimisho ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), leo Jumanne June 9, 2026.
Muktasari:
- Sekta ya madini imeendelea kuwa mhimili wa uchumi wa Tanzania, ikichangia asilimia 11 ya Pato la Taifa, huku Serikali ikitekeleza mageuzi ya sheria, utafiti na uchakataji ili kuongeza manufaa kwa wananchi.
Dar es Salaam. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema baadhi ya vikwazo vya kisheria na mifumo ya usimamizi vimechangia kuchelewesha Tanzania kunufaika kikamilifu na utajiri wake wa madini.
Hayo ameyasema alipozindua maadhimisho ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), leo Jumanne Juni 9, 2026, ambapo amebainisha kuwa mageuzi yaliyofanyika sasa yameanza kuleta matokeo katika mapato ya Serikali, akiba ya dhahabu na ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo.
Mavunde anafafanua kuwa moja ya hatua muhimu ni mabadiliko ya kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini yaliyowezesha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wakubwa na wadogo.
"Tuliingia humo kwa kubadili kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini, ambacho sasa kinaipa nafasi BOT kununua madini kwa wauzaji wakubwa na wadogo. Oktoba 2024 hadi leo tayari tumeingia tano bora Afrika kwa akiba ya dhahabu katika benki kuu," amesema.
Amesema Tanzania sasa ina zaidi ya tani 24 za dhahabu katika akiba ya BoT, hatua anayoitaja kuwa ushahidi wa namna marekebisho ya sheria yanavyoweza kuongeza manufaa ya rasilimali za Taifa.
Mavunde amesema sekta ya madini imeendelea kuimarika kiuchumi, ikichangia asilimia 11 ya Pato la Taifa na asilimia 15 ya mapato yote ya kodi nchini.
"Mwaka 2025 tuliingiza Sh1.07 trilioni sawa na asilimia 103 ya lengo. Mwaka huu tayari tumefikia Sh1.3 trilioni, sawa na asilimia 107 ya lengo la kipindi hiki," amesema.
Hata hivyo, amesema changamoto kubwa iliyobaki ni kiwango kidogo cha utafiti wa kina wa madini nchini.
"Nchi yetu ina eneo la kilomita za mraba 945,000. Tumefanya utafiti wa madini kwa asilimia 97, lakini utafiti wa kina umefanyika kwa asilimia 16 tu," amesema.
Amesema Serikali imejiwekea lengo la kuongeza kiwango hicho hadi asilimia 50 kupitia miradi ya uchunguzi wa anga katika mikoa ya Kigoma, Katavi, Kusini mwa Tanzania pamoja na mradi wa pamoja na China katika mikoa ya Tabora na Shinyanga.
Hoja ya umuhimu wa utafiti imeungwa mkono na Naibu Makamu Mkuu wa UDSM anayeshughulikia utafiti, Profesa Nelson Boniface, ambaye amesema maendeleo ya sekta yoyote yanategemea uwekezaji katika tafiti na ubunifu.
Profesa Boniface amesema tafiti na ubunifu ni hatua muhimu katika kukuza teknolojia na kuwezesha Taifa kunufaika na rasilimali zake.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Anangisye amesema Tanzania inapaswa kutumia teknolojia na maarifa kuongeza thamani ya madini badala ya kuyachukulia kama rasilimali za kawaida.
"Tunapaswa kujiuliza tunatumiaje teknolojia katika kuongeza thamani ya sekta ya madini, tunatumiaje rasilimali hizi kuboresha maisha ya wananchi," amesema.
Amesema vyuo vikuu vina nafasi ya kusaidia Serikali kupata majawabu ya changamoto za maendeleo kupitia tafiti za ndani, akitoa wito kwa viongozi wa Serikali kutumia vyuo vikuu kupata majawabu ya changamoto za sekta zao ili kuibua maendeleo.
Mipango endelevu
Mavunde amesema Serikali imefanya maboresho ya Kanuni ya 13 ya "Local Content" akisema ni hatua muhimu katika kuongeza ushiriki wa Watanzania katika manunuzi yanayofanywa migodini.
"Sekta ya madini hutumia zaidi ya Sh5 trilioni kwa manunuzi ya bidhaa na huduma. Maboresho haya yanalenga kuhakikisha sehemu kubwa ya fedha hizo inanufaisha Watanzania," amesema.
Amesema Serikali pia inaandaa mfumo wa dhamana za mikopo kwa wachimbaji wadogo ili kupunguza utegemezi wa mitaji ya nje, huku ikiendelea kutekeleza programu maalumu za kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki katika sekta hiyo.
Katika eneo la kuongeza thamani ya madini, amesema Serikali imezuia usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi na kwa sasa kuna viwanda nane vya kusafisha madini (refineries), huku Smelter kubwa inayojengwa Songwe ikitarajiwa kuimarisha uwezo wa ndani wa uchenjuaji.
Hata hivyo, Profesa Agnes Mwakaje amesema mafanikio ya mageuzi hayo yatategemea uwezo wa kuyageuza kuwa mabadiliko ya kimfumo yanayogusa wananchi.
"Kushughulikia changamoto za sekta ya madini ni suala la kimfumo. Lazima mabadiliko yashuke hadi ngazi za chini. Ni suala la kisera pia," amesema.
Naye Rais wa Chama cha Wahandisi Tanzania, Mhandisi Asa Mwaipopo amesema pamoja na utajiri mkubwa wa madini uliopo nchini, bado Tanzania inahitaji uwekezaji mkubwa katika teknolojia, maarifa na viwanda vya kuongeza thamani.
"Ghana sasa inaongoza uzalishaji wa dhahabu, Tanzania imeshuka hadi nafasi ya tatu. Swali la kujiuliza ni kama migodi yetu ya dhahabu tumeitumia ipasavyo," amesema.
Kwa mtazamo wa wadau mafanikio ya sekta ya madini inaelezwa kutegemea uwezo wa Tanzania kuunganisha sheria bora, tafiti, teknolojia na ushiriki wa wananchi ili utajiri wa madini ugeuke kuwa maendeleo halisi ya Taifa, badala ya kubaki kwenye karatasi huku jamii ikikosa kuyaona matunda yake.