Mbeya Cement yatoa gawio baada ya miaka 10
Muktasari:
- Kampuni hiyo imetangaza mgao wa Sh4,259 kwa kila hisa ambayo ni faida iliyosubiriwa kwa muda mrefu kutokana na mafanikio yaliyofikiwa mwaka 2023.
Dar es Salaam. Kampuni ya saruji ya Mbeya Cement Company Limited (MCCL) imetangaza malipo ya gawio ikiwa ni miaka 10 tangu malipo ya mwisho yalipofanyika.
Kampuni hiyo imetangaza mgao wa Sh4,259 kwa kila hisa, ikiwa ni sehemu ya faida iliyosubiriwa kwa muda mrefu inayoakisi utendaji wa kampuni uliorekodiwa mwaka wa 2023.
Kutokana na faida hiyo, Serikali ambayo inamiliki asilimia 25 ya hisa kupitia Msajili wa Hazina, inatarajiwa kupata gawio la Sh3 bilioni.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Juni 1, 2024, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambalo lilikuwa na asilimia 10 ya hisa, litapata gawio la Sh1.2 bilioni.
"Gawio hili kubwa linakuja kama nyongeza ya kukaribishwa, inayoonyesha afya dhabiti ya kifedha ya kampuni na uwezo wa siku zijazo," inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, malipo hayo yanaashiria mabadiliko tangu mgao wa mwisho ulipotolewa mwaka wa 2014 na kuwa hilo limetokana na mikakati iliyotekelezwa chini ya umiliki mpya.
Kampuni hiyo, hivi karibuni imekuwa mwanachama wa Kundi la Amsons, ambalo lilipata asilimia 65 ya hisa kutoka kwa Kundi la Holcim lenye makao yake makuu Uswizi.
Mikakati iliyowezesha mafanikio hayo ni pamoja na kupunguza utegemezi wa klinka iliyonunuliwa na kuongeza uzalishaji wa malighafi hiyo kutoka kwenye migodi yake.
Akiba ya kina ya migodi ya kampuni na uwezekano wa kuongezeka kwa uzalishaji wa klinka yalikuwa mambo muhimu, "na mkutano ukisisitiza haja ya uwekezaji wa kimkakati ili kuongeza rasilimali hizi."
Uboreshaji wa hivi majuzi wa kifedha ulisaidiwa zaidi na makubaliano muhimu ya msamaha yaliyofikiwa Novemba 2023, ambayo yalibadilisha mkopo uliokuwepo kutoka kwa Cemasco Limited, kurahisisha mzigo wa deni la kampuni na kuruhusu kuwekeza tena katika maeneo ya ukuaji.
"Kwa sasa MCCL ina hisa ya asilimia sita ya soko nchini na iko tayari kupanuka. Wasimamizi wa kampuni wanalenga katika kuimarisha mikakati ya uuzaji ili kuhifadhi wateja waliopo na kuvutia wapya,” inasomeka sehemu nyingine ya taarifa hiyo.