Mbunge alia wakulima wa korosho kuchelewesha malipo

Muktasari:
- Mbunge Nanyumbu, Yahya Mhata ameibuka mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas akilalamika kucheleweshwa kwa malipo ya korosho walizouza wakulima katika minada mitatu kati ya mitano iliyofanyika.
Mtwara. Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, Yahya Mhata amelalamikia ucheleweshaji wa malipo ya korosho kwa wakulima, huku akimwomba Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas kuwachukulia hatua anunuzi walioshindwa kuwalipa wakulima.
Kauli hiyo ameitoa leo Novemba 18 wakati wa uzinduzi wa maandalizi ya msimu wa kilimo katika Kijiji cha Nanyumbu, Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu, mkoani Mtwara, sanjari na uzinduzi wakilimo cha pamoja (Block Farming), ugawaji wa mbegu za ufuta na mbaazi, pamoja na matumizi ya kipima udongo.
Amesema kuwa licha ya wakulima kupeleka korosho zao katika utaratibu wa mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani, lakini wmalipo yao yamekuwa yakicheleweshwa.
Aidha mbunge huyo amesema, wapo wanunuzi korosho huzichukua kutoka mnada mmoja kwenda mwingine bila kuwalipa wakulima.
“Tuko katika msimu wa korosho na leo ni mnada wa tano lakini fedha ambazo wakulima wameishalipwa ni za minada miwili tu, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu kwani inatakiwa ndani ya siku nne, mnunuzi awe amelipa.
“Sisi tunafanya mnada Ijumaa, lakini inachukua zaidi ya wiki mbili bila kulipwa, zipo kampuni zinazoomba kununua na kuruhusiwa, jambo la kusikitisha zinashindwa kuwalipa wakulima,” amesema.
Akijibu malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanal Ahmed Abbas ameagiza vyama vikuu, taasisi za fedha na wanunuzi wa korosho kukutana ili kuweza kutatua changamoto hizo.
Katika utatuzi huo, amewataka Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (Tanecu) na Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi na Mtwara (Mamcu), taasisi za fedha pamoja na wanunuzi kukutana na Katibu Tawala wa Mkoa Novemba 21, 2023.
“Haitokuwa na maana tunasimama hapa tunajisifia mafanikio yote haya alafu kuna wananchi wanaendelea kusikitika na wengine wanaendelea kulia pengine kutokana na uzembe wa watu wachache,” amesema RC huyo.
Pia amewataka wakulima kufanya maenedeleo na kubadilisha maisha yao kwa kuzalisha mazao yenye tija kama vile korosho, mbaazi, ufuta, karanga na choroko.
“Tari (Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania) wametupatia mbegu za ufuta tani 10, hivyo nawaagiza viongozi na maofisa ugani kuhakiikisha kuwa mbegu za hizo zinatolewa kwa wakulima walioandaa mashamba na waliotayari kufuata kanuni taratibu na masharti ya kilimo bora,” amesema Kanal Abbas.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji) Mkoa wa Mtwara, Nanjiva Nzunda amesema kuwa sekta ya kilimo imekuwa ikikua, ambapo mazao yaliyokuwa hayafanyi vizuri kwa sasa yanalimwa.
“Katika msimu wa 2023 tumeshuhudia ongezeko kwa mauzo ya zao la mbaazi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na tumeuza zaidi ya tani 17, zilizowapatia wakulima zaidi ya Sh35 milioni ikiwa ni mara ya kwanza kuuzwa kwa mfumo huo,” amesema.
Kwa upande wa zao la ufuta, Nzunda amesema: “Zao la ufuta limeongezeka kutoka tani 9 hadi 17, 843 na kuuzwa kwa zaidi ya Sh66.7 bilioni.”
Kwa mantiki hiyo, mkoa huo kwa mujibu wa Nzunda, umeongeza nguvu katika mazao ya korosho, ufuta, karanga, alizeti, choroko na mbaazi kwa kuimarisha huduma za kilimo kwa kuwawezesha maofisa ugani kwa kutumia tozo ya Sh2 ya kila korosho inayoenda halmashauri.
“Kupitia tozo hii, maafisa ugani watawafikia wakulima na kuhakikisha kuwa kalenda ya mazao inafuatwa,” amesema Nzunda.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Tari, Joseph Nzunda amesema kuwa endapo wakulima watafuata maelekezo ya watalaamu na kutumia mbegu bora, watalima kwa tija na kuongeza uzalishaji na hivyo kukidhi mahitaji wa soko.
“Tunajua soko linahitaji nini ndio maana tumegawa tani 10 za mbegu za ufuta kwa wakulima wa Mkoa wa Mtwara, kwakuwa wanunuzi wanangalia sana suala la kiafya ambapo wamehimiza tuwasisitize wakulima wetu nchini kuzingatia ubora tukifanya uzembe tunaweza kupoteza wateja,” amesema Joseph.