Mbunge ataka nguvu kwenye uzalishaji si kupanga bei

Muktasari:

  • Mbunge wa Sumve Kasalali Mageni, ameiomba Serikali kuwekeza zaidi  kwenye uzalishaji badala ya kutumia nguvu kuwapangia wakulima namna nzuri ya kuuza mazao yao.

Dar es Salaam. Mbunge wa Sumve Kasalali Mageni, ameiomba Serikali kuwekeza zaidi  kwenye uzalishaji badala ya kutumia nguvu kuwapangia wakulima namna nzuri ya kuuza mazao yao.

Mageni ametoa kauli hiyo jana Ijumaa April 9,2021 bungeni  Jijini Dodoma alipokuwa akichangia mjadala wa mpango wa tatu wa maendeleo wa kitaifa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2021/22 - 2025/26.

Amesema wakulima wanapoanza kuzalisha Serikali inakuwa kimya lakini wakishaanza kuvuna mazao yao wanaanza kuona masharti mara stakabadhi ghalani, uanzishwaji na usimamizi usio rafiki kwa wakulima.

“Mimi kwenye Jimbo langu la Sumve tunalima mazao jamii  ya kunde,  choroko na dengu ni mazao ambayo wakulima  tunayalima kwa nguvu zetu hatujawahi kuona dawa, mbegu  kutoka serikalini lakini tunapoanza kuvuna tunaanza kuona watu wanaitwa Amcos, ushirika wanakuja kusimamia bei za mazao yetu na mbaya zaidi wanaleta utaratibu wa ovyo zaidi, naomba sana Serikali iwekeze zaidi kwenye uzalishaji kabla ya kuanza kuwapangia wakulima bei ya kuuza mazao yao”amesema

Amesema Serikali inapaswa kuliangalia kwa undani kwakuwa  hawawezi kuweka mazao yote kwenye kapu moja  kwasababu kufanya hivyo kunachangia kuua bei ya masoko ya mazao tofauti.

“Wilaya ya Kwimba inaongoza kwa uzalishaji wa zao la Pamba  lakini linasimamiwa na watu ambao hawajui na limeingiliwa, kuna mabeberu yanayowadidimiza wakulima na Serikali imeshiriki kuliiua soko lake, wakulima wengi nchini hawajui kama wanalima wanapata faida au hasara  huwa tunalima tu  lakini ukifanya mahesabu tunapata hasara,”amesema