Mji wa Himo watajwa kitovu biashara haramu

Mji wa Himo watajwa kitovu biashara haramu

Muktasari:

  • Mji wa Himo uliopo kilometa 27 kutoka mji wa Moshi ambao ndio makao makuu ya Mkoa wa Kilimanjaro, unatajwa kuwa kitovu cha biashara haramu nne, huku baadhi ya viongozi wa vitongoji na vijiji wakitajwa kuwa sehemu ya tatizo.

  Mji wa Himo uliopo kilometa 27 kutoka mji wa Moshi ambao ndio makao makuu ya Mkoa wa Kilimanjaro, unatajwa kuwa kitovu cha biashara haramu nne, huku baadhi ya viongozi wa vitongoji na vijiji wakitajwa kuwa sehemu ya tatizo.

Licha ya Jeshi la Polisi, Jeshi la Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuonyesha mafanikio katika mapambano na mitandao hiyo ya kihalifu, lakini uwepo wa njia za panya zaidi ya 200, unaathiri kazi nzuri ya vyombo hivyo.

Mbali na uwepo wa njia hizo, jiografia ya mji huo kuwa jirani na mpaka wa Tanzania na Kenya, unachangia kuwapo kwa mwingiliano mkubwa, huku baadhi ya polisi kituo cha Himo na mgambo wakitajwa kuwa sehemu ya mitandao hiyo.

Biashara za kihalifu zinazoufanya mji huo kuwa kitovu ni biashara ya magendo ya bidhaa, biashara ya dawa za kulevya aina ya mirungi, biashara ya wahamiaji haramu, biashara ya gongo na mji huo kuwa njia ya usafirishaji wa bangi.

Kati ya mwaka 1995 hadi mwaka 2006, kulikuwapo kikosi maalumu cha polisi cha kupambana na magendo kilichokuwa chini ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, ambacho hata hivyo kilivunjwa kwa kushindwa kudhibiti magendo.

Lakini kwa sasa, mfumo unaowahusisha maofisa wa TRA na polisi kwa wakati mmoja, umesaidia kwa kiasi fulani kufanikisha doria na operesheni za kukabili magendo, ingawa bado wapo wafanyabiashara wanaofanikiwa kuwakwepa.


Biashara ya magendo ya bidhaa

Mji huo unatajwa kuwa kitovu cha uingizaji bidhaa za magendo na taarifa kutoka kwa vyanzo mbalimbali zinaeleza bidhaa zinazoingizwa kimagendo kwa wingi kwa sasa ni mafuta ya taa, mafuta ya kula, sabuni na steel wire.

“Unajua biashara ya magendo ya bidhaa ni ya kihistoria na ilishika kasi miaka ile ya 90 hasa bia kutoka Kenya, lakini kwa sasa ni mafuta ya taa, mafuta ya kula, sabuni na bidhaa nyingine ndogo ndogo zinazozika zaidi,” ilidokezwa.

Chanzo kingine kimedokeza bidhaa nyingine inayoingizwa kwa wingi na kwa usiri ni simu za kiganjani ambazo huwekwa kwenye mifuko ya sandarusi au viroba na kuingizwa kutoka Kenya kwa kutumia pikipiki na kusambazwa miji mbalimbali.

“Kuna simu mpya zinaingizwa na hazilipiwi kodi zinaingizwa kwa njia za magendo kupitia hapa Himo. Simu zinazoibwa Kenya zinapitia hapa na kwenda kuuzwa Moshi hasa kituo kikuu cha mabasi,” Gazeti hili limedokezwa.


Biashara ya gongo

Pombe haramu ya gongo inatajwa kuwa biashara inayolipa na maeneo sita ya mji wa Himo yanatajwa kuwa kinara wa upikaji na uuzaji wa pombe hiyo ambayo baadhi husafirishwa kwenda nchini Kenya kupitia Wilaya ya Rombo.

Vyanzo mbalimbali kutoka mji huo vimeyataja maeneo hayo yaliyopo pembezoni kwa mto Ghona unaopita katika mji huo mdogo kuwa ni Nganyoni, Makuyuni, Kilema Njiapanda, Kilototoni na eneo la Himo Kosovo.

“Gongo inauzwa waziwazi na inashamiri kwa sababu baadhi ya polisi wetu hapa Himo wamegeuza kama ni mradi. Huwa wanachukua return (mgawo) kila mwisho wa mwezi. Kwa ufupi gongo hapa ni uchumi,” chanzo chetu kimedokeza. Chanzo kingine kimedokeza kuwa biashara hiyo inazidi kushamiri kwa kuwa kisheria kosa la uzalishaji, uuzaji na unywaji wa gongo lina faini kwa hiyo wakipigwa faini wanachangishana wanailipa chapchap,” kilieleza chanzo hicho.


Wahamiaji kutoka Kenya

Uchunguzi umebaini kuwa Jeshi la Uhamiaji kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limefanikiwa kudhibiti kwa kiasi kikubwa biashara ya wahamiaji haramu kutoka Ethiopia na Somalia wanaoingia kupitia Kenya.

Biashara hiyo inahusisha fedha nyingi na mhamiaji mmoja anatozwa zaidi ya Dola 3,000 Marekani (sawa na Sh6.6milioni za Tanzania), kwa ajili ya kutoka Somalia au Ethiopia kupitia Kenya, hadi mpaka wa Tunduma ili kuingia Kusini mwa Afrika.

Vyanzo mbalimbali vimedokeza kuwa wahamiaji kutoka Ethiopia na Somalia huingia nchini kwa kutumia njia za panya zaidi ya 200 zilizopo maeneo ya mpakani ya Kitobo, Madarasani, Mariatabu na Riata wakisaidiwa na bodaboda.

Hata hivyo, Jeshi la Uhamiaji kwa sehemu kubwa limefanikiwa kudhibiti biashara hiyo, lakini sasa tatizo kubwa ni uwepo wa wahamiaji kutoka Kenya ambao wapo maeneo mengi ya mji wa Himo wakifanya kazi na wengine kuwa wahamiaji.

“Wakenya wamejaa tele huku tunaishi nao na wengine wanaingia kama wapenzi baadae wanaishi kabisa humu. Huwezi kuamini kuna wengine hadi wanaomba vitambulisho vya Taifa wakisaidiwa na wenyeji,” kilieleza chanzo chetu.


Biashara ya mirungi

Usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya mirungi kutoka Kenya huanzia katika vijiji vya mpakani mwa Tanzania na Kenya katika Wilaya za Rombo na Moshi, kupitia barabara kuu ya Himo-Moshi hadi kwa wauzaji wa jumla.

Maeneo ambayo yamekithiri kwa upitishaji, uhifadhi na uuzaji wa mirungi ni vijiji vya mpakani wa Tanzania na Kenya ya Madarasani, Kitobo, Lotima, mto Ghona, Chekereni hadi Njiapanda na kitovu cha biashara hiyo ni mji wa Himo.

Wengine hupitia vijiji vya Kilototoni na Kyomu hadi barabara kuu ya Mwanga-Moshi na wengine hupitia barabara za kuelekea vijiji vya Kahe na Mabogini na baadaye kuingia katikati ya mji, lakini wasafirishaji wakuu wako Himo.

Kwa Moshi mjini, maeneo ambayo hutumika kupokea na kuuza mirungi hiyo ni eneo la Matindigani, Bomambuzi, Pasua, Njoro, Bondeni, Majengo, Kiborlon, Mnazi, Soweto, Uru na Rau na bodaboda ndio hutumika.

Imendikwa na Daniel Mjema na Florah Temba