Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpango wa miaka mitano ulivyoiimarisha NMB

Muktasari:

  • Benki ya NMB imetangaza kuingia katika awamu mpya ya ukuaji baada ya kukamilisha mpango wake wa muda wa kati wa mwaka 2021 hadi 2025, uliowezesha benki hiyo kurekodi faida kabla ya kodi ya zaidi ya Sh1 trilioni, kutoa gawio kubwa kwa wanahisa na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

Dar es Salaam. Utekelezaji wa Mpango wa Muda wa Kati wa Benki ya NMB wa mwaka 2021 hadi 2025 umeiwezesha taasisi hiyo kuimarisha nafasi yake katika sekta ya fedha, baada ya kurekodi faida kabla ya kodi ya zaidi ya Sh1 trilioni, kuelekeza zaidi ya Sh28 trilioni katika sekta mbalimbali za uchumi na kuchangia Sh2.7 trilioni kama kodi kwa Serikali.

Katika kipindi hicho, benki hiyo pia ililipa zaidi ya Sh700 bilioni kama gawio kwa wanahisa na kuwekeza Sh24 bilioni katika miradi ya maendeleo ya jamii.

Mafanikio hayo yamewasilishwa leo Juni 9, 2026 jijini Dar es Salaam katika mkutano wa wawekezaji uliofanyika kuelekea Mkutano Mkuu wa 26 wa Wanahisa wa NMB unaotarajiwa kufanyika kesho.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, amesema kipindi cha miaka mitano iliyopita kimekuwa miongoni mwa hatua muhimu zaidi katika historia ya benki hiyo kutokana na mageuzi yaliyoifanya kuwa taasisi imara zaidi na yenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na mabadiliko ya mazingira ya biashara.

“Hii imekuwa sura muhimu katika historia ya NMB. Mageuzi tuliyoyatekeleza katika kipindi cha miaka mitano yamejenga taasisi imara zaidi, mtindo wa biashara wenye ustahimilivu na msingi thabiti wa kuingia katika awamu mpya ya ukuaji,” amesema Zaipuna.

Amesema katika kipindi hicho NMB iliongeza kiwango cha mali, amana za wateja, mikopo na matumizi ya huduma za kidijitali, huku ikiendelea kupanua huduma zake kwa makundi mbalimbali ya wananchi na sekta za uzalishaji.

Kwa mujibu wa benki hiyo, zaidi ya Sh28 trilioni zilizoelekezwa katika uchumi zilichangia kugharamia shughuli za biashara, kilimo, viwanda, huduma na miradi mingine ya maendeleo, hatua iliyoifanya NMB kuwa miongoni mwa taasisi zenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema mchango wa taasisi za fedha katika uchumi wa Tanzania ni mkubwa na umechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi kwa wastani wa takribani asilimia sita kwa miaka mingi.

“Historia ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania haiwezi kutenganishwa na mchango wa taasisi kama NMB,” amesema Profesa Kitila.

Amesema pamoja na maendeleo yaliyopatikana, sehemu kubwa ya shughuli za kiuchumi nchini bado ipo nje ya mfumo rasmi, hivyo benki na taasisi za fedha zina wajibu mkubwa wa kusaidia biashara ndogo na za kati kupata mitaji, huduma za kifedha na mazingira bora ya kukua.

“Taasisi za fedha kama NMB zinasaidia kuleta biashara nyingi zaidi katika mfumo rasmi, kupanua upatikanaji wa mitaji na kuongeza uwezo wa Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa,” amesema Profesa Kitila.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uhusiano na Wawekezaji, Uendelevu na Mawasiliano wa NMB, Innocent Yonazi, amesema awamu inayofuata ya ukuaji wa benki hiyo itaweka mkazo katika teknolojia, uendelevu, biashara ndogo na za kati pamoja na sekta zinazochochea uwekezaji na ajira.

“Kadiri nchi inavyokua na kubadilika, wajibu wetu ni kuhakikisha tunaendelea kutoa suluhisho za kifedha, uwekezaji na ubia unaohitajika kuunga mkono mageuzi hayo,” amesema.