Mrajisi: Acheni kuweka takataka kwenye tumbaku

Muktasari:

  • Wakulima wa Tumbaku nchini waonywa kuweka takataka kwenye bidhaa hiyo.

Morogoro. Onyo limetolewa kwa wakulima wa zao la Tumbaku nchini, kuacha tabia ya kuweka takataka kwenye bidhaa hiyo yakiwemi mawe kwa lengo la kuongeza uzito, kwani kufanya hivyo kumekuwa kukitishia kuua soko.

 Naibu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Collins Bnyakunga amesema hayo wakati wa kikao na wadau mbalimbali bidhaa za tumbaku wakiwemo warajisi wa vyama vya ushirika, mameneja  wa vyama vikuu ushirika pamoja na wakulima wa zao la tumbaku.

Mrajisi huyo amesema wapo baadhi ya wakulima wamekuwa wakiharibu soko la tumbaku kwa makusudi kwa kuweka takataka zenye kidhoofisha na wengine kuweka mawe kwenye tumbaku yao ili kuongeza uzito kwamba hiyo sio sawa kabisa.

"Niseme tu wanunuzi wamekuwa wakitumia kigezo cha ubora wa tumbaku katika kufanya uamuzi wa kununua zao hilo katika soko lakini uwaminifu umekuwa mdogo kwa baadhi ya wakulima tubadilike," amesema.

Pia amewasisitiza viongozi wa vyama vya ushirika kuondoa hati chafu na zile zenye mashaka.

Mwenyekiti wa Mradi wa Pamoja wa Wakulima Tanzania (TCJE), Ntelizyo John amesema moja ya changamoto wanayokumbana nayo ni kampuni za tumbaku kutolipa fedha kwa wakulima  kwa wakati.

Aidha amesema wakulima wa tumbaku hawanufaiki na ruzuku za mbolea na hivyo kuomba waweze kupata fursa hiyo muhimu kama ilivyo kwa  wakulima wa mazao mengine.

Mkurugenzi wa Bodi yaTumbaku, Tanzania Stanley Mnozya amesema msimu ujao tumbaku  umeongezeka kutoka kilogramu 60 milioni hadi kufikia 125 milioni msimu huu.

Mnozya amesema lengo la serikali ni kilogramu 200 milioni ifikapo mwaka 2025 huku mahitaji yakiwa kilogramu 231 milioni.