Nape: Sekta ya fedha imebeba ukuaji uchumi

Muktasari:

Serikali imesema sekta ya fedha imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa pamoja na kujenga uchumi jumuishi.

Dar es Salaam. Serikali imesema sekta ya fedha imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa pamoja na kujenga uchumi jumuishi.


Imesema kuwa hatua hiyo imekuwa chachu ya kupunguza umasikini na ndio sababu na kwamba, mataifa mengi kwa sasa yamekuwa yakitilia mkazo ujumuishi kwenye sekta ya fedha.


Hayo yameelezwa leo Jumatano Novemba 16, 2022 na Waziri Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akizindua progamu ya CRDB Wakala App ambayo inakwenda kurahisisha zaidi utoaji wa huduma za kifedha.


"Hapa nchini Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisera ili kukuza ujumuishi wa kifedha kwa wananchi.


“Baadhi ya jitihada za kisera na kimkakati ambazo zimefanyika ni pamoja na kuanzishwa kwa Mpango wa Elimu ya Kifedha (Financial Education Program 2021/22 – 2025/26) na mwaka 2020, ilizindua Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (Financial Sector Development Master plan - 2020/21 -2029/30)," amesema Nape.


Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo Nape amesema bado idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za benki ni ndogo na hamasa na elimu inahitaji kuendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali.


Nape amekwenda mbali zaidi akikumbushia utafiti wa kwanza wa Finscope wa mwaka 2006 ambao ulionyesha kuwa ni asilimia 46 tu ya watu wazima walijumuishwa kifedha, ambapo asilimia 11 tu walikuwa wakitumia huduma rasmi za kifedha.


Hatua hiyo imeelezwa kuwa inatokana na idadi kubwa ya watu kuwa nje ya mfumo wa fedha kutokana na ufikiaji mdogo wa huduma za benki kupitia matawi katika maeneo ya vijijini na gharama za ufikiaji wa huduma za kifedha ikiwemo hitaji la kusafiri umbali mrefu.


Kwa kutambua mchango wa teknolojia kutatua changamoto hiyo, Nape amesema Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Februari 2013 ilitoa mwongozo wa huduma za benki kupitia mawakala na sasa CRDB ina zaidi ya mawakala 25,000 nchi nzima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema benki hiyo imekuwa ya kwanza kuanzisha huduma za kifedha kupitia mawakala mwaka 2013 ambapo, ilianza na mawakala 500 na sasa wapo zaidi ya 25,000 nchini kote.


"Mfumo wa CRDB wakala umekuwa na mchango mkubwa katika kufikisha huduma za fedha kwa wananchi, taarifa zetu za utendaji zinaonyesha zaidi ya miamala milioni 100 yenye thamani ya Sh50 trilioni imefanyika kupitia CRDB wakala kwa mwaka. Mfumo huu pia unasaidia ukusanyaji wa mapato ya Serikali na takribani Sh1.3 trilioni hukusanywa kwa mwaka," amesema Nsekela.


Nsekela ameongeza kuwa mfumo huo unahudumia zaidi ya wateja milioni tatu na umetoa ajira kwa vijana 35,000 wanaolipwa kamisheni kwa kila muamala wanaoufanya.


"Huu ni mwendelezo wa juhudi za benki yetu katika kutambua umuhimu wa huduma za kidigitali ili kuleta ufanisi wa huduma jumuishi za fedha na maendeleo kwa ujumla.


Kupitia huduma hii tunaamini tutawafikia Watanzania wanaoishi vijijini na sehemu za pembezoni ili kuhakikisha makundi hayo hayaachwi nyuma," amesema.