NMB yatunukiwa kimataifa

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna akimkabidhi Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB, Dkt. George Mulamula, Tuzo ya umahiri ya Euromoney kama Benki Bora Tanzania 2021 na Benki bora huduma kwa wateja binafsi na Biashara (Best Retail Bank) wakati wa hafla iliyofanyika katika Makao Makuu ya NMB -  Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi Benki ya NMB, Filbert Mponzi na Kushoto ni Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya NMB, Juma Kimori.


Muktasari:

  • Licha ya kuwa benki kubwa zaidi nchini, NMB ni bora na inayowahudumia vizuri zaidi wateja wake. Majarida mawili ya nchini Uingereza yamelitambua hilo na kuipa tuzo NMB yenye matawi katika halmashauri karibu zote nchini. 


  


Dar es Salaam. Kutokana na umaahiri wake sokoni, Benki ya NMB imetunukiwa tuzo ya benki bora Tanzania na benki bora kwa wateja binafsi na  biashara za kati.

Tuzo hizo zimetolewa na taasisi mbili tofauti za kimataifa. Wakati Jarida la Euromoney likiitangaza NMB kuwa benki bora Tanzania kwa mwaka wa tisa mfululizo, lile la Global Banking and Finance limeitunuku kuwa benki bora ya huduma kwa wateja binafsi na biashara za kati nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo hizo kwa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, Ofisa Mtendaji Mkuu, Ruth Zaipuna amesema wanajivunia juhudi zilizoongeza ufanisi uliozaa tuzo hizo.

Akimkabidhi tuzo hizo Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, George Mulamula, Zaipuna amesema ubunifu wa bidhaa, uwekezaji katika teknolojia na huduma za kidigitali ni kati ya mambo yaliyochangia kuifanya NMB kuwa benki bora.

“Ni heshima na mafanikio makubwa kwa NMB kupata tuzo hizi. Tunajivunia kuona juhudi zetu zinatambulika kimataifa na tunajiona tuna deni la kuendelea kujituma zaidi ili kubaki kwenye viwango vya kimataifa,” amesema.

Marida ya Euromoney na Global Banking and Finance yana makaomakuu yao jijini London, Uingereza na hufanya tathmini ya huduma za benki duniani kote.

Akipokea tuzo hizo, Mulamula aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Bodi, Dk Edwin Mhede ameipongeza menejimenti na wafanyakazi wa benki kwa mafanikio hayo na kuwataka kutobweteka.

“Ningependa ieleweke kwa jamii na wateja wetu kuwa tuzo hizi zina maana kwamba NMB ni benki bora Tanzania na tumejikita kutoa huduma bora kwa Watanzania mahali popote walipo, iwe mjini au kijijini,” amesema Mulamula.