Pwani kuanza kuzalisha mihogo kibiashara

Pwani kuanza kuzalisha mihogo kibiashara

Muktasari:

  • Ili kuwaongezea tija wakulima, mkakati wa kulima mihogo kibiashara umeandaliwa mkoani Pwani.

Pwani. Baada ya miaka mingi ya mihogo kuliwa mibichi, Mkoa wa Pwani unajipanga kulifanya zao hilo kuwa la biashara.

Mkakati huo unatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Wakulima na Wasindikaji Mihogo Tanzania (Tacappa).

Mkuu wa mkoa huo, Evarist Ndikilo amebainisha alipofungua mkutano wa Tacappa uliolenga kujitambulisha mkoani humo na kuweka mikakati ya kuongeza uzaishaji wa mihogo nchini.

Ndikilo amesema kiasi kikubwa cha mihogo inayozalishwa mkoani Pwani, kati ya asilimia 60 mpaka 70, inaliwa ikiwa mibichi na kidogo kinachobaki kukaushwa kama makopa.

"Wananchi wanalima lakini bado zao hili halijachangia vilivyo katika uchumi wetu kwa hiyo tutoke na azimio la kuwezesha kufanya uzakishaji mkubwa. Tuifanye mihogo kuwa zao la kimkakati. Watu walime kwa kutumia mbegu bora na kiutalaam kwani Tacappa wametuonyesha soko sasa," amesema Ndikilo.

Kwa miaka mitano iliyopita, wastani wa tani 6.5 hadi 7.6 zilizalishwa kwa hekta moja ingawa yapo maeneo machache  hasa wilayani Kibiti na Rufiji ambako walipata kati ya tani tisa hadi 18 kwa hekta ingawa uzalishaji wa dunia ni tani 20 kwa hekta.

Awali, mwenyekiti wa Tacappa Taifa, Mwantumu Mahiza aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na soko la uhakika la mihogo nchini endapo tu mkoa huo utakuwa na uhakika wa kuzalisha tani 300 za mihogo mibichi kwa siku kigezo cha wawekezaji wengi.

"Maofisa kilimo wakatoe elimu kwa wakulima ili walime kitaalamu. Tukijipanga vizuri tutazalisha zaidi mihogo, wawekezaji wanaojenga viwanda huangalia  kwenye uzalishaji wa kutosha,” alisema Mwantumu.

Mihogo ni zao kuu la chakula mkoani Pwani ambako hekta 60,703 zinatumika kuzalisha zao hilo. Kwa mwaka, Pwani inavuna kati ya tani 500,000 hadi 650,000.

Hata hivyo, eneo linalotumika ni sawa na asilimia 3.1 kwani mkoa huo una hekta 1,933,224 zinazofaa kwa kilimo hicho.