Rais Samia asema haikuwa sawa kuchoma vifaranga kutoka Kenya

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekumbushia namna ugumu wa ufanyaji wa biashara kati ya Tanzania na Kenya ulivyokuwa ngumu kabla hajaingia madarakani huku akifurahishwa na hatua zinazofanyika sasa.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema wakati hajaingia madarakani biashara kati ya Tanzania na Kenya ilikuwa ngumu sana huku akikumbusha vifaranga vilivyochomwa moto mpakani akisema haikuwa sawa kuchoma vifaranga kutoka Kenya.

Ameyasema hayo Alhamisi, Novemba 24, 2022 katika ufunguzi wa mkutano wa 27 wa wanasheria wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki unaofanyika jijini Arusha.

"Watu wamefika mipakani pale makaratasi hayasomi vizuri na vifaranga vyako haisemi vimetoka wapi, kunapitishwa vifungu vya sheria kama vile sheria ndiyo kila kitu, mwisho wa siku sheria hairuhusu, suluhisho choma hivyo vifaranga hata hatuogopi dhambi," amesema

"Tumejisahau kuwa vifaranga ni viumbe wa Mungu walikuwa na uhai tukachoma, roli za mahindi zinakaa mipakani miezi mitatu, mahindi ya Tanzania yana sumukuvu tunategeana tegeana hivi," amesema

Amesema kwa sababu yeye ni Suluhu alinyanyuka na kwenda kwa Rais wa Kenya wa wakati huo, Uhuru Kenyatta na kumuambia yanayoendelea hayafai huku.


"Tukakusanya na jumuiya ya wafanyabiashara tukaenda Nairobi, tukaongea sisi wawili ndani (na Rais wa Kenya) nikamuambia sasa twende kwa wafanyabiashara, tukaenda tukaongea nao tukamaliza wakaanza vikao vyao wafanyabiashara.

Amesema katika vikwazo visivyokuwa vya kikodi 64 vilivyokuwepo 55 kati yake vimeondolewa na wakati mazungumzo yakiendelea biashara unekuwa kwa kiasi kikubwa kupitia mazungumzo pekee.

"Vivyo hivyo tumefanya na nchi nyingi na shughuli zinakwenda. Na nyie katika katika shughuli zenu za kisheria za kuvuka mipaka, kajipangeni ili biashara yenu iende vizuri mtuletee nini mnaweza kufanya nini nchi zenu zinaweza kufanya ili biashara yenu ivuke mikapa kwa malengo ya kusaidia jamii,” amesema na kuongeza:

"Pamoja na kuwa huduma yenu ina malipo sawa lakini lazima mtu alipie ili apate huduma bora.”