Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia ataja maeneo matano ya kipaumbele, Rais wa Singapore asema…

Muktasari:

  • Tanzania na Singapore zimekubaliana kuongeza ushirikiano katika biashara na uchumi.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametaja sekta tano za kipaumbele kwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Singapore, huku nchi hizo mbili zikilenga kubadili uhusiano wao wa kidiplomasia wa zaidi ya miaka 45 kuwa wa biashara na uwekezaji.

Ameeleza hayo leo Jumanne, Juni 9, 2026, katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji la Tanzania na Singapore lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Kupitia kongamano hilo, Rais Samia amewaalika wawekezaji wa Singapore kutumia fursa zilizopo katika sekta za bandari na usafirishaji, uongezaji thamani wa mazao ya kilimo na madini, nishati jadidifu, utalii pamoja na huduma za kifedha.

Kongamano hilo lilifanyika baada ya mazungumzo ya viongozi wa nchi hizo mbili, Rais Samia na Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo walishuhudia kusainiwa kwa makubaliano matano yanayohusu masuala ya kodi, urahisishaji wa biashara, maendeleo ya ujuzi, ushirikiano wa tabianchi na mashauriano ya kidiplomasia.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Singapore, lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

Rais Samia amesema Tanzania na Singapore zimekuwa na uhusiano mzuri kwa zaidi ya miaka 45, lakini ushirikiano wa kiuchumi bado haujafikia kiwango kinachostahili.

"Ingawa uhusiano wetu wa kidiplomasia umeendelea kuwa imara na wa kirafiki, bado kuna fursa nyingi ambazo hazijatumika kikamilifu katika kuimarisha na kupanua ushirikiano wetu wa kiuchumi," amesema.

Amebainisha kuwa biashara kati ya nchi hizo iliongezeka kutoka dola milioni 74 mwaka 2020 hadi kufikia dola milioni 299 mwaka 2023, kabla ya kushuka tena hadi dola milioni 74 mwaka 2024, hali aliyoeleza kuwa inaonyesha umuhimu wa kujenga mahusiano ya kiuchumi yenye uimara zaidi.

"Mifumo yetu ya biashara bado haina uimara wa kutosha, hivyo tunapaswa kuchukua hatua mahsusi kushughulikia tofauti hizi," amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Singapore, lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

Rais Samia amesema Tanzania inalenga kunufaika na uzoefu wa Singapore katika usafirishaji na ugavi, maendeleo ya viwanda, upangaji wa miji na uhamasishaji wa uwekezaji, wakati nchi ikiendelea kutekeleza azma ya kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

Eneo la kwanza la kipaumbele alilotaja ni bandari na usafirishaji, akisema Tanzania ina faida ya kipekee kutokana na nafasi yake ya kijiografia kama lango la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

"Bandari ya Dar es Salaam inahudumia sehemu kubwa ya biashara hii ya usafirishaji. Ushirikiano na waendeshaji wa kiwango cha kimataifa kutoka Singapore utaongeza tija ya bandari yetu na kuifanya Singapore kuwa kitovu kinachounganisha Afrika na Asia," amesema.

Ametaja miradi ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mradi wa Bandari na Eneo Maalumu la Viwanda la Bagamoyo pamoja na maendeleo ya bandari za Zanzibar kuwa maeneo yanayoweza kunufaika na utaalamu wa Singapore.

Sekta ya pili ni uongezaji thamani katika kilimo na madini. Rais Samia amesema Tanzania inataka kuondokana na utegemezi wa kuuza malighafi na badala yake kuanzisha viwanda vya uchakataji vitakavyohudumia masoko ya Asia na dunia kwa ujumla.

"Sehemu kubwa ya dhahabu na vito vyetu bado huondoka nchini bila kuongezewa thamani. Vikichakatwa hapa nchini, vitatusaidia kuhamia kutoka kuuza malighafi hadi kuuza bidhaa zilizochakatwa na zenye chapa zinazohitajika katika masoko ya kimataifa," amesema.

Pia amependekeza kuwepo kwa mikataba ya muda mrefu ya biashara ya mazao ya kilimo ili Tanzania iweze kusambaza bidhaa kama kahawa, chai, korosho na viungo nchini Singapore, wakati taifa hilo likitafuta vyanzo vipya vya chakula.

Kipaumbele cha tatu ni nishati jadidifu na miundombinu ya kisasa. Kutokana na ongezeko la mahitaji ya nishati kwa ajili ya viwanda na uwepo wa rasilimali za nishati ya jua, upepo, jotoardhi na gesi asilia, Tanzania inaiona Singapore kama mshirika muhimu katika maendeleo ya teknolojia za kijani na miundombinu endelevu.

Eneo la nne ni utalii, ukarimu na uchumi wa buluu. Rais Samia amesema Tanzania ilipokea watalii wa kimataifa takribani milioni 2.3 mwaka jana, lakini soko la Asia bado halijatumika kikamilifu.

"Kuna fursa kubwa katika miundombinu ya utalii, utangazaji wa vivutio vya utalii na kuimarisha usafiri kati ya nchi zetu. Tushirikiane kuongeza idadi ya watalii kati ya Tanzania na Singapore," amesema.

Huduma za kifedha na utatuzi wa migogoro ya kibiashara vilikuwa eneo la tano la kipaumbele. Rais Samia amesema Tanzania inaweza kunufaika na uzoefu wa Singapore katika masoko ya mitaji, ufadhili wa miradi mikubwa na mifumo ya usuluhishi wa migogoro inayotambulika kimataifa.

"Tunakaribisha ushirikiano katika kuendeleza kituo cha kimataifa cha huduma za kifedha na kuanzisha kituo cha usuluhishi wa migogoro ya kibiashara chenye ithibati ya kimataifa ili kuongeza imani ya wawekezaji," amesema.


Alichokisema Rais wa Singapore

Kwa upande wake, Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, akisema mabadiliko yanayoendelea katika mfumo wa biashara duniani yanahitaji mataifa kujenga ushirikiano mpya na kupanua minyororo ya ugavi.

Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam akizungumza katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Singapore, lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

"Katika dunia ya namna hii, jibu ni kupanua ushirikiano, kujenga njia mpya za fursa na kuimarisha minyororo ya ugavi yenye ustahimilivu mkubwa zaidi," amesema.

Akielezea Tanzania kuwa nchi yenye matarajio makubwa, Rais huyo amesema idadi kubwa ya vijana, nafasi yake ya kijiografia, utajiri wa rasilimali na fursa zinazoongezeka za uwekezaji vinaendelea kuvutia wafanyabiashara wengi wa Singapore.

"Tukitumia vizuri nguvu zinazokamilishana za uchumi wa nchi zetu mbili, tunaweza kuzalisha ajira bora, kuongeza uwezo wa watu wetu na kufanikisha ukuaji jumuishi wa uchumi," amesema.

Pia amekaribisha mpango wa kuanza mazungumzo ya makubaliano ya biashara huria kati ya Singapore na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), akisema hatua hiyo inaweza kuleta mageuzi makubwa katika biashara kati ya Afrika Mashariki na Kusini Mashariki mwa Asia.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema mafanikio ya kiuchumi ya Singapore yana funzo muhimu kwa Tanzania katika jitihada zake za kuharakisha maendeleo ya viwanda na kuvutia uwekezaji.

"Mwelekeo wa uchumi wa Rais Samia uko wazi kabisa. Ni wa vitendo. Tunazunguka dunia kutafuta si misaada, bali biashara na fursa za uwekezaji," amesema.

Profesa Mkumbo amesema safari ya Singapore kutoka nchi maskini hadi kuwa moja ya uchumi mkubwa duniani ni mfano ambao Tanzania inaweza kujifunza wakati ikitekeleza malengo yake ya maendeleo.

"Hadithi ya Singapore inaheshimika duniani kote. Ni safari ambayo Tanzania inaweza kujifunza mengi tunapoendelea kutimiza ndoto zetu za maendeleo," amesema.