Samia atekeleza ‘mradi’ wa Magufuli Mbeya
Muktasari:
- Mradi huo wenye lengo la kuwezesha wafanyabishara wadogo kuondokana na changamoto za kupanga bidhaa maeneo yasiyo rasmi ikiwepo pembezoni mwa miundombinu ya barabara, ni utekelezaji wa agizo la aliyekuwa Rais awamu ya tano.
Mbeya. Serikali imetoa zaidi ya Sh500 milioni kwa ajili ya kuboreshwa miundombinu ya Soko la Kimataifa ka Wafanyabishara wadogo maarufu ‘Machinga’ katika eneo ulipokuwa uwanja wa ndege wa zamani Kata ya Iyela Jijini Mbeya.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano, Mei 10, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa, amesema leo Jumatano, Mei 10,2023 mara baada ya kukagua utekelezaji wa ujenzi huo katika soko hilo ambapo 2020, aliyekuwa Rais Hayati John Magufuli, alitoa maagizo kwa uongozi wa Mkoa, kuboresha miundombinu hiyo.
Malisa amesema licha ya Serikali kuwekeza fedha hizo, halmashauri ya Jiji la Mbeya kwa kushirikiana na Serikali Kuu, inasimamia utelezaji wa mradi huo hatua kwa hatua kwa lengo la kuhakikisha wafanyabishara wadogo wanafanya shughuli zao katika mazingira rafiki.
“Fedha hizo zimetolewa na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu kutokana na kuwepo kwa changamoto mbalimbali za mazingira yasiyo rafiki kwa wafanyabishara hali iliyokuwa ikiwalazimu kupanga bidhaa maeneo yasiyo rasmi,” amesema.
Malisa amesema kuwa uwepo wa mradi huu utawesha halmashauri kuongeza mapato sambamba na wafanyabishara wote kulazimika kuingia kuendesha shughuli zao za kiuchumi ndani ya soko na sio maeneo yasiyo rasmi hususan pembezoni mwa miundombinu ya barabara.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Mbeya Dk Jonas Lulandala, amesema tayari wametoa maelekezo kwa watendaji kusimamia miongozo yote iliyotolewa katika kuboresha soko hilo inatekelezwa na kumalizika kwa wakati.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo Jiji la Mbeya, Waziri Hamisi ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kuwatupia macho wamachinga kwa kuboresha miundombinu ambayo ilikuwa ni changamoto kubwa kwa kipindi kirefu.
“Sasa tunaiona Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kitupia jicho wananchi wa kipato cha chini kwani mbali ya kutoa fedha ujenzi wa soko pia tumepokea zaidi ya Sh 10 milioni kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Shirikisho la Machinga Jiji la Mbeya ambao uko katika hatua za awali”amesema.
Mfanyabishara wa mitumba soko la Sido, Ephraim Joel amesema kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo itakuwa mwarobaini wa kuwaondoa kwenye mazingira magumu ya utafutaji hususan katika msimu wa masika.
Naye Diwani wa Kata ya Iyela Mussa Ismaily, amesema watasimamia utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya ubadhirifu hususan upotevu wa vifaa vya ujenzi.