Prime
Sekta binafsi, wasafishaji wataja maeneo muhimu bajeti 2026/27
Muktasari:
- Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27 inatarajiwa kuwa Sh 61.93 trilioni, huku ikilenga kuongeza makusanyo ya ndani hadi kufikia Sh46.69 trilioni ili kupunguza utegemezi wa misaada na mikopo kutoka nje
Dar es Salaam. Wakati Serikali kesho Alhamisi, Juni 11, 2026 ikitarajiwa kuwasilisha bajeti ya mwaka 2026/27 inayokadiriwa kufikia Sh61.93 trilioni, sekta binafsi imeainisha maeneo matano muhimu inayotaka yawekwe mbele ili kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuimarisha ushindani wa biashara nchini.
Aidha, Chama cha Wamiliki wa Malori ya Kati na Madogo Tanzania (Tamstoa) na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) wanatamani bajeti ipunguze mamlaka za udhibiti pamoja na kuboresha miundombinu ili kuwezesha usafirishaji kuwa rafiki.
Mapendekezo hayo yanakuja wakati bajeti hiyo ikitarajiwa kuwa ya kwanza katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku sekta binafsi ikisisitiza ukuaji wa mapato ya Serikali unapaswa kwenda sambamba na ukuaji wa shughuli za uzalishaji na uwekezaji.
Akizungumzia bajeti hiyo jana Jumanne Juni 9, 2026, Meneja wa Uchambuzi wa Sera kutoka Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Mercy Philipo amesema ni vyema kuhamasisha uwekezaji kupitia sera thabiti na zinazotabirika.
“Kuwepo kwa mazingira yenye uhakika wa sera yataongeza imani kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuvutia mitaji ya muda mrefu na kuchochea uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi,” amesema.
Pia, amesema bajeti hiyo ielekeze nguvu katika kukuza uchumi wa viwanda kwa kuimarisha ushindani wa viwanda vya ndani, kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini na kupanua mauzo katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Amesema kwa kufanya hivyo kutaongeza nafasi katika kuongeza ajira na mapato ya kigeni.
“Pia, ni vyema kuimarisha urasimishaji wa biashara ndogo na za kati (MSMEs) ambazo zinaendelea kuwa mhimili wa uchumi wa Taifa kupitia sheria rahisi hasa kwa wafanyabiashara wasiowasilisha ritani,” amesema.
Katika upande wa kuweka mazingira wezeshi ya biashara ametaka kuwapo kwa sheria za usimamizi wa kodi, kuondoa tozo, kero, ada na shuru mbalimbali zinazoongeza gharama ya kufanya biashara hapa nchini.
“Pia ni vyema kuhakikisha uwepo wa sera za kodi na zisizo za kodi zinazochochea ukuaji wa sekta ya fedha pamoja na uchumi wa kidijitali kama nyenzo kuu ya kuongeza uwekezaji, kuimarisha ubunif na kupanua ushiriki wa sekta binafsi kwenye uchumi wa kisasa,” amesema Philipo.
Mbali na hayo, sekta binafsi imependekeza bajeti hiyo kutoa kipaumbele kwa sekta za kilimo, viwanda, madini, utalii, ujenzi, usafirishaji, huduma na uchumi wa kidijitali ambazo zinaendelea kuwa nguzo kuu za ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
“Ni muhimu kutambua, Serikali na sekta binafsi zina lengo moja la kujenga uchumi imara, shindani na wenye kuleta ustawi kwa Watanzania wote.
“Taifa linapojiandaa kusikiliza bajeti hii, sekta binafsi ina matumaini kuwa itaweka msingi imara wa ukuaji endelevu wa uchumi unaochagizwa na sekta binafsi kwa asilimia 70 ili kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema.
Amesema kadri Serikali inavyolenga kugharamia bajeti kubwa zaidi huku ikiendelea kudumisha uhimilivu wa kifedha, ni muhimu kutambua kwamba sekta binafsi inaunga mkono jitihada za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Amesema ili kufikia lengo hilo, ongezeko la mapato ya Serikali linapaswa kujengwa juu ya msingi wa kukuza uchumi, kuongeza tija ya uzalishaji nakupanua shughuli za kiuchumi, badala ya kuongeza mzigo kwa walipakodi ambao tayari wanatimiza wajibu wao ipasavyo.
“Kwa lugha rahisi, ukuaji endelevu wa mapato ya Serikali unategemea uwepo wa sekta binafsi imara, inayokua na inayoweza kushindana. Bajeti ya mwaka 2026/27 inatarajiwa kutoa fursa muhimu ya kuweka uwiano sahihi kati ya malengo ya ukusanyaji wa mapato na kuimarisha ushindani wa sekta binafsi,” amesema Philipo.
Matamanio ya Taboa
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Priscus Joseph amesema katika bajeti hiyo ni vyema kuangalia namna ya kupunguza mamlaka za udhibiti ambazo zimeweka tozo nyingi katika mauzo ghafi yakichukuliwa kidogo kidogo yanapunguza faida Serikali itakosa faida.
Amesema wakati asilimia 30 ya faida ikipaswa kwenda serikalini, uwepo wa tozo nyingi katika mapato ghafi unaifanya Mamlaka ya Mapato (TRA) kukosa kodi.
“Pia, mamlaka zinapochukua kwenye mauzo kuna mitaji. Ni vyema hizi mamlaka kabla hazijaanzishwa ziwe zinapita kwa waziri wa fedha ziangaliwe muundo wake, kwani mara zote wanatunga vyanzo vingi vya mapato lakini si kwenye biashara mpya ni zilezile wanaongeza tozo,” amesema.
Amesema katika dunia ya sasa ili upate zaidi ni vyema kuwa na faida ndogo kupitia kuuza sana lakini kuchukua mauzo ya mtu ili utoze kodi ni kumuumiza.
“Katika upande wa tozo zipo mamlaka nyingi za udhibiti ambazo kwa pamoja zinaweza kubeba hadi asilimia nne hali hiyo inafanya Serikali na mfanyabiashara wanakosa hela kwa sababu tozo zinaishia kwenye halmashauri,” amesema.
Wakati haya yanafanyika, sheria nyingi zilizowekwa za usimamizi katika utozaji wa tozo hizi zinatajwa kuwa ngumu katika mchakato wake na mazingira huku urahisi unaoonekana ni kumpa mfanyakazi rushwa.
“Matokeo yake mamlaka inamnufaisha mfanyakazi wakati ambao mamlaka hiyo, mwanachi na wafanyabiashara wanafilisika. Ila suala la tozo liangaliwe zaidi kwa kuwa, sasa tunalipa Latra, TRCA, halmashauri kila unayoingia inataka tozo wakati huo halmashauri inakupa leseni na latra wamekupa leseni, bandubandu humaliza gogo,” amesema.
Ukarabati miundombinu
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori ya Kati na Madogo Tanzania (Tamstoa), Chuki Shabani amesema ni vyema bajeti hii ikatoa kipaumbele katika utengenezaji wa ukarabati wa miundombinu ili kusaidia kuchochea ukuaji wa uchumi.
Amesema barabara ambazo ndiyo nyenzo kuu ya kutoa bidhaa sehemu moja kwenda nyingine ni vyema zikaongezwa kulingana na mahitaji yaliyopo sasa hasa wakati huu ambao bandari inashuhudia ufanisi mkubwa.
“Bandari ni sehemu tunayoitegemea sasa, ni vyema kuhakikisha maboresho yaliyofanyika yanaendana na kasi ya uwezeshaji wa mizigo kutoka haraka bandarini kwa kuwezesha watendaji kuwa na weledi katika kutejeleza majukumu yao ipasavyo,” amesema.
Amesema ni wakati sasa wa kuhakikisha kipaumbele kinakuwa katika kuliwezesha Jiji la Dar es Salaam kupumua kwa kupeleka bandari kavu nje ya mji ili malori yachukulie mzigo huko huku akitolea mfano wa Kwala.
“Kwala inaweza kusaidia sana kufanikisha hili, tulifanye Jiji la Dar es Salaam lipumue kwa kutoa vibali vya ujenzi wa hizi bandari kavu kule badala ya kuendelea kuziweka ndani ya jiji hali inayofanya kuendelea kuwapo kwa malori,” amesema.
“Hilo liende sambamba na ujenzi wa barabara za njia nane kutoka Kibaha hadi Chalinze na Chalinze hadi Morogoro ili kuweka urahisi katika usafirishaji wa biashara.
“Pia, katika ujenzi wa hizi barabara, tunapojenga ni vyema kuhakikisha kuwa maeneo ya hifadhi ya barabara yanawekwa katikati; tutapanda miti na matunda badala ya kuweka pembeni, ikitokea unataka kufanya upanuzi inakulazimu kuanza kulipa watu fidia, utamaliza fedha kwa kulipa fidia wakati ingekuwa katikati unatoa miti na kujenga,” amesema.
Athari za tozo na ada
Mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi jijini Dar es Salaam, Hamisi Mussa amesema ongezeko la tozo na ada kutoka taasisi mbalimbali limekuwa likipunguza mtaji wa biashara na kuathiri uwezo wa wafanyabiashara kupanua shughuli zao.
Amesema changamoto kubwa si kulipa kodi, bali wingi wa malipo yanayotozwa na taasisi tofauti tofauti kabla biashara haijaanza kupata faida.
“Mfanyabiashara yuko tayari kulipa kodi, lakini tatizo ni hizi tozo nyingi zinazokuja kutoka kila upande. Unalipa leseni, unalipa ada mbalimbali na wakati mwingine unatozwa kabla hata hujauza au kupata faida. Hali hii inapunguza mtaji unaotakiwa kutumika kukuza biashara,” amesema.
Mussa amesema mazingira hayo yanawaathiri zaidi wafanyabiashara wadogo na wa kati ambao uwezo wao wa kifedha ni mdogo ikilinganishwa na kampuni kubwa.
“Wafanyabiashara wengi wangependa kupanua biashara zao na kuajiri watu zaidi, lakini sehemu kubwa ya fedha inaishia kwenye gharama za uendeshaji. Serikali ikiangalia namna ya kupunguza tozo zisizo za lazima na kurahisisha taratibu za biashara, itasaidia biashara nyingi kukua na kuongeza mapato ya Serikali kwa muda mrefu,” amesema.
Ameongeza kuwa, mfumo unaowezesha biashara kukua na kupata faida ndio unaoweza kuongeza mapato ya kodi kwa Serikali badala ya utegemezi wa tozo nyingi zinazobebwa na wafanyabiashara wachache waliopo kwenye mfumo rasmi.