Serikali, watoa huduma kupeleka mawasiliano vijijini

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashibaa (kulia) akisaini mkataba na Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Basiimire (kushoto)  huku utiaji saini ukishuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan leo Jumamosi Mei 13, 2023 jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo

Dar es Salaam. Serikali imeingia mikataba na watoa huduma za mawasiliano nchini kwenda kujenga minara ya simu katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na kuiongezea nguvu minara inayotoa teknolojia ya 2G kwenda 3G.

Mikataba hiyo imesainiwa leo Mei 13, 2023 jijini Dodoma katika hafla iliyoshuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ikihusisha Kampuni za Airtel Tanzania, TTCL, Vodacom Tanzania, Mic Tanzania (Tigo) na Vietel (Halotel).

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema walitangaza zabuni ya kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo 763 lakini baada ya mchakato wa zabuni, wamepata maeneo katika kata 713 ambayo minara ya mawasiliano 758 itakwenda kujengwa.

“Hii ni historia kwa taasisi yetu, hata ushiriki wa watoa huduma katika zabuni hii, wameweza kushiriki kwa asilimia 93. Hii ni historia katika ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali,” amesema Mashiba.

Mtendaji huyo amesema baada ya kutangaza zabuni hiyo, wamepata watoa huduma watakaokwenda kujenga minara ambao ni TTCL wanaokwenda kujenga minara 104 katika kata 104, Vodacom Tanzania ameshinda kata 190 ambapo atakwenda kujenga minara 190.

Wengine ni Airtel Tanzania ambayo imepata kata 161 ambapo itajenga minara 168, Tigo (MIC Tanzania) imeshinda katika maeneo 244 ambapo itajenga minara 262, Halotel (Vietel) imeshinda katika kata 34 na itakwenda kujenga minara 34 katika maeneo mbalimbali nchini.

“Mbali na kwenda kujenga minara, tunakwqenda pia kuongeza nguvu ya minara mingine 304 ambayo ilikuwa inatoa teknolojia ya 2G lakini sasa itakwenda kutoa teknolojia ya 3G na baadhi ya maeneo mengine itatoa teknolojia ya 4G,” amesema mtendaji huyo.

Ameongeza kwamba Tigo itakwenda kuongeza nguvu ya minara 148, TTCL minara 55, Airtel minara 32, Vidacom minara 69 na jumla itakuwa minara 304.