Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yataka umakini uwekezaji teknolojia ya fedha

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Sauda Msemo akizungumza wakati wa kufungua Mkutano wa Jukwaa la Uwekezaji la Afrika Mashariki,unaoendelea kufanyika jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Serikali yasisitiza mapambano ya utakatishaji fedha na ugaidi.

Dar es Salaam. Wakati kupata fedha za uendelezaji mawazo bunifu ikiwa moja ya changamoto kwa wabunifu wengi, Serikali imetaka umakini uwepo katika uwekezaji wa teknolojia ya fedha (FinTech).

Umakini huo unalenga kupambana na utakatishaji fedha kwa kuweka njia zitakazozuia hayo kufanyika.

Pia, imetaka FinTech kuhakikisha uthabiti wa hali ya juu kupitia uaminifu wa mifumo ya kifedha kwa ujumla.

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Sauda Msemwa amesema hayo alipofungua Jukwaa la Uwekezaji Afrika Mashariki (EAIF) 2024 lililolenga kutafuta fursa za uwekezaji kwa wavumbuzi wa teknolojia za fedha likibebwa na kaulimbiu isemayo ‘Uwekezaji na ubia bila kumuacha mwingine nyuma.’

Sauda amesema FinTech zitakazoruhusiwa kufanya kazi nchini lazima zihakikishe zinafuata sheria za kifedha zilizowekwa na kuhakikisha ulinzi kwa watumuaji wa bidhaa zake.

“Umakini unapaswa kuwapo kupambana na utakatishaji fedha na ugaidi kwa kuweka hatua za kupunguza haya na kuhakikisha kunakuwa na udhibiti wa hali ya juu kupitia uaminifu wa mifumo ya kifedha kwa ujumla,” amesema.

Sauda amesema ni muhimu kuhakikisha ubora katika utoaji wa huduma za kifedha hasa unaozingatia uwazi katika vipengele vya bidhaa na huduma ili kumwezesha mtumiaji kufanya maamuzi sahihi na kupata taarifa mpya za huduma hizo.

Amesema BoT tayari imeweka kanuni zinazohitaji kuwekwa wazi kwa masharti na gharama za huduma hizo na miongozo kuhusu ada na malipo.

Amesema kama watumiaji hawana imani na huduma zinazotolewa ni ngumu kufanikiwa katika kile walichokibuni na watumiaji hawatapata faida kutokana na huduma hizo.

Amesema Serikali inafahamu changamoto zinazowakabili wabunifu, ikiwemo upatikanaji mdogo wa fedha na mitaji, ugumu wa kuvutia uwekezaji mkubwa na kushindwa kuelewa mazingira ya udhibiti na ushindani.

“Benki Kuu ya Tanzania (BoT) itaendelea kuunga mkono FinTech, ubunifu na hivi karibuni tutaanza kuwaalika wabunifu kuja na mawazo yao,” amesema.

Mbali ya hayo, matumizi ya fedha za mifuko ya hifadhi ya jamii yametajwa kuwa moja ya njia inayoweza kusaidia mawazo bunifu kuendelezwa.

Hilo litawezekana kupitia ubia wa uwekezaji wa pamoja kati ya mashirika hayo na wawekezaji wa kigeni.

Akitoa mada, Christine Maina ambaye ni Mkurugenzi Africa Private Equity & Venture Capital Association (EAVCA) amesema nchi za Afrika  Mashariki zimeshuhudia kupungua kwa fedha za kigeni zinazoingia kwa ajili ya uwekezaji kutokana na sababu mbalimbali kama vile uchumi wa dunia na uchaguzi katika nchi nyingine.

“Afrika inahitaji kuanza kuangalia rasilimali zake za ndani. Hivyo, tulifanya utafiti kwa nini mifuko ya pensheni haitazami uwekezaji huu kama sehemu ya kupata fedha na kwa nini mara nyingi wanawekeza kwenye dhamana za serikali, hatifungani, na mali isiyohamishika pekee,” amesema.

Amesema waligundua hawana uelewa wa kutosha kuhusu uwekezaji huo, hivyo hatua ya kwanza iliyofanyika ni kutoa elimu na kuonyesha mifano ya uwekezaji uliofanikiwa na faida zake.

“Tunatambua changamoto zinazokuwepo, kuna uwezekano mkubwa wa mtu kutorudisha fedha zake lakini tunatafuta njia za kupunguza hili,” amesema.

Amesema moja ya njia ni kuwezesha taasisi kuwekeza pamoja na watu kutoka nje kusaidia wavumbuzi, biashara ndogo na za kati.

Magdi Amin, mshirika wa African Renaissance Ventures amesisitiza umuhimu wa kujumuisha huduma za kifedha hasa kwa watu wasio na akaunti za benki.

"Ni muhimu kutoa msaada kwa waanzilishi wa vumbuzi hizi sahihi kwa kuhakikisha wanapata motisha inayofaa na mwelekeo wake ni kuhakikisha wajasiriamali wa Afrika Mashariki wanafanikiwa katika masoko kama vile Rwanda, Kenya, Tanzania, Uganda, na Ethiopia ili kanda hii isichelewe katika mazingira ya kifedha ya kimataifa,” amesema.