Stamico kuwashika mkono wachimbaji wadogo

Ofisa Uhusiano wa Stamico Bibiana Ndumbaro akitoa mada kwenye Mkutano Mkuu wa saba wa Jukwaa la Wahari Tanzania (TEF).

Muktasari:

  • Lengo la utoaji wa mikopo hiyo ni kuwawezesha wachimbaji kununua vifaa vya kisasa na kukuza biashara zao, ajira na uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa.

Lindi. Shirika la Madini la Taifa (Stamico) limesema kilio cha wachimbaji wadogo kukosa fursa ya mikopo hivi sasa kimepata suluhisho baada ya kuingia makubaliano na taasisi tano za kifedha kwa ajili ya kuwapa mikopo.

 Lengo la utoaji wa mikopo hiyo ni kuwawezesha wachimbaji kununua vifaa vya kisasa na kukuza biashara zao, ajira na uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne, Novemba 14, 2023 na Ofisa Uhusiano wa shirika hilo, Bibiana Ndumbaro alipokuwa akiwasiliana mada katika Mkutano Mkuu wa saba wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) unaofanyika mkoani Lindi.

Amesema makubaliano waliyoingia na benki hizo tano yatawawezesha wachimbaji wadogo kuomba mikopo kwenye taasisi hizo na wao (Stamico) wanapoombwa taarifa wachimbaji hao huzitoa ili kuwezesha upatikanaji wa kile kinachotakiwa.

“Kimsingi hapa tunazungumzia benki za NMB, KCB CRDB na Azania ambazo zipo kusaidia wachimbaji wadogo kufikia malengo yao, rasilimali zetu ni vema zitakatusaidia kupiga hatua kiuchumi” amesema 

Bibiana amesema Stamico imedhamiria kuleta suluhisho la kudumu la upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo kwa kuhakikisha inasimamia kuanzishwa kwa Benki ya Wachimbaji ambapo taratibu za uanzishwaje wake umeanza.

Amesema kuwa Stamico imeboresha uendeshaji wa miradi yake na kuifanya kuwa sehemu ya kukusanya mapato na sio matumizi jambo lililosababisha kuongezeka kwa mapato yake.

“Tumeboresha mradi wetu wa kuzalisha nishati mbadala ya kupikia  kwa kuleta mitambo mikubwa miwili yenye uwezo wa kuzalisha  tani 20 kwa saa kila mmoja ili kuongeza uzalishaji  wa nishati hiyo kuweza kuwafiki wananchi wengi. Mitambo hii itafungwa mkoani Pwani na Songwe” amesema

Bibiana amesema kuwa Stamico imechagiza kuanzishwa kwa kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza ambacho kimechochea ongezeko la thamani ya madini hivyo kuchochea ukuaji wa ajira na teknolojia kwa Watanzania.

Ameongeza kuwa kupitia miradi ya ubia Stamico inahakikisha miradi hiyo inarithisha teknolojia na kutoa ajira kwa Watanzania.

Amebainisha kuwa wameendelea kutoa elimu ya teknolojia kwa vitendo kwa wachimbaji wadogo na kuongeza  kituo cha mfano  kwa ajili  ya wachimbaji  wa chumvi  mkoani  Lindi ili kuhakikisha  wanazalisha chumvi yenye ubora kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.

Naye mchimbaji mdogo, Abdul Jamal amesema kuwa utoaji mikopo unapaswa kutolewa bila upendeleo au kuangalia ukubwa wa biashara ya wahusika.

“Wachimbaji wodogo wengi hawana dhamana za kuwawezesha kupata mikopo, kama Stamico na benki hizo zitaangalia vigezo vya ukopeshaji kama wanavyofanya kwa makundi mengine sisi hatutaweza kupenya” amesema.

Cristina Peter amesema anaamini ujio wa Benki ya Uchimbaji ndiyo itakuwa mkombozi wa masuala ya kifedha kuliko kutegemea taasisi nje ya mfumo huo.

“Wenzetu walimu wana benki yao, wakulima wanayo hivyo ninaona ni wakati mwafaka kwetu wachimbaji kuwa na benki yetu” amesema.