Tanzania, Singapore zahuisha ushirikiano kiuchumi, EAC kushirikishwa
Muktasari:
- Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, aliwasili nchini jana Juni 8, 2026 kwa ziara ya kitaifa kwa mwaliko wa Rais Samia na alipofika Ikulu leo, alipata heshima ya kupigiwa mizinga 21 pamoja na gwaride maalumu lililoandaliwa kwa ajili ya mapokezi yake.
Dar es Salaam. Serikali za Tanzania na Singapore zimetiliana saini mikataba mitano ya ushirikiano huku viongozi wa mataifa hayo wakijadiliana kuhusu masuala mbalimbali, ikiwamo uwezeshaji wa vijana nchini ili kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Pia, wamejadiliana kuhusu azma ya Singapore kutaka kushirikiana kibiashara na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupitia Makubaliano ya Biashara Huria (FTA) ili kupanua wigo wa biashara baina yao huku Singapore ikiahidi kuwa lango katika soko la Asia.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekutana na mgeni wake, Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, leo Jumanne, Juni 9, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo wawili hao walifanya mazungumzo ya faragha, baadaye wakafanya mazungumzo ya pande mbili.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo na ujumbe wa Singapore uliongozwa na Rais Tharman Shanmugaratnam.
Rais Shanmugaratnam aliwasili nchini jana Juni 8, 2026 kwa ziara ya kitaifa kwa mwaliko wa Rais Samia na alipofika Ikulu leo, alipata heshima ya kupigiwa mizinga 21 pamoja na gwaride maalumu lililoandaliwa kwa ajili ya mapokezi yake.
Kwa takwimu za mwaka 2025, Singapore ina pato ghafi la taifa (GDP) la dola za Marekani 606.23 bilioni (Sh1,579 trilioni), huku kwa mwaka 2026 likikadiriwa kuwa dola bilioni 659.576 (Sh1,716 trilioni). Uchumi wa Singapore unategemea zaidi biashara za kimataifa katika sekta za huduma za fedha, uzalishaji, bidhaa za kielektroniki, uchumi wa kidijitali na usafiri wa anga.
Akizungumza na vyombo vya habari, Rais Samia amesema ziara ya kiongozi huyo ni ya kwanza kwa Rais wa Singapore kuitembelea Tanzania na inafanyika wakati nchi hizo zikitimiza miaka 45 ya uhusiano na ushirikiano wa kidiplomasia.
Rais Samia amesema pia wamejadili kuhusu uwezeshaji wa vijana na alimweleza kuhusu Dira ya 2050, ambayo imeweka kipaumbele zaidi kwa vijana kwa kuwa ndio watakaoongoza na kushika nafasi mbalimbali.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Jumanne Juni 9, 2026 kwa ziara ya Kitaifa.
Amesema amemweleza dhamira ya Serikali kuwawezesha vijana katika elimu, hasa ya ujasiriamali, ukuzaji wa ujuzi na ubunifu, na kwamba Serikali imejielekeza zaidi katika uchumi wa kidijitali na kutekeleza mkakati wa uchumi wa kidijitali wa 2024/2034.
“Pakubwa tulipojielekeza ni mambo ya Digital Economy (uchumi wa kidijitali), kuwaingiza vijana wetu sana kwenye utekelezaji wa mkakati wetu wa uchumi wa kidijitali ambao tumepanga kuutekeleza ndani ya miaka 10 ijayo kuanzia mwaka 2024 hadi 2034,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema kwamba amemweleza mgeni wake utayari wa Tanzania kushirikiana na Singapore katika mpango wao wa kuimarisha usalama wa chakula kwa nchi zote.
Ameikaribisha kuwekeza katika kilimo cha uzalishaji kupitia utaratibu wa kuzalisha nje ya nchi, kama ambavyo Tanzania imekubaliana na Russia.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam kwenye mkutano na waandishi wa habari leo Juni 9, 2026, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Amesema wamezungumzia ushirikiano wa kikanda na wamekaribisha wazo la Singapore kuzungumza na Umoja wa Afrika kuhusu masuala ya Soko Huru la Afrika.
“Anatufungulia na sisi njia, lakini tunakuza mawasiliano. Singapore ni nchi ndogo lakini nzito sana kiuchumi, kwa hiyo tukionekana tukakuza mawasiliano na nchi kama hiyo, tunakuza dhamira yetu katika uchumi pia,” amesema.
Rais Samia ameeleza kwamba wamezungumza kuhusu uhusiano na ushirikiano ili uwe thabiti kwa maslahi ya pande zote, na wamejadili kuhusu ushirikiano katika biashara na uwekezaji na kukubaliana kuuimarisha zaidi.
“Nimeikaribisha Singapore kufungua ubalozi wake hapa nchini. Ni wazi nimewapa wazo, watakwenda kujadili na kuamua,” amesema.
Ameongeza kuwa katika kikao chao wamekubaliana kuangalia njia za kukuza biashara na uwekezaji. Amesema kwa sasa kiwango cha biashara kati ya mataifa hayo ni dola za Marekani milioni 299 huku Singapore ikiwa na miradi 36 nchini, idadi ambayo amesema ni ndogo.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Juni 9, 2026 kwa ziara ya Kitaifa.
Rais Samia amesema kiwango cha biashara kati ya mataifa hayo hakiakisi uhalisia wa urafiki wao, ndiyo maana wamesaini mikataba ya kuimarisha ushirikiano zaidi.
Kwa upande wake, Rais wa Singapore, Shanmugaratnam, amesema sasa ni wakati wa kuhuisha uhusiano wa mataifa hayo ili kuupa nguvu mpya na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano.
Amesema wanakutana katika kipindi ambacho siasa za ulimwengu zinabadilika, huku msukumo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ukiongezeka, na nchi zinazoendelea ziko katika hatari ya kubaki nyuma katika kunufaika na fursa.
Amesema mwitikio wa hali hiyo ni kujenga kanda, ikiwemo Afrika na Asia, miongoni mwa nchi zinazoamini katika ushirikiano unaotoa njia ya kwenda mbele. Amesema Singapore na Tanzania zimepiga hatua katika mwelekeo huo.
“Nilitaka hakikisho la Rais Samia kuhusu dhamira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya Makubaliano ya Biashara Huria (FTA) na Singapore. Hili ni muhimu, linaiunganisha Singapore siyo tu na Tanzania, bali pia na nchi nyingine za Afrika Mashariki (EAC).
Rais Shanmugaratnam amesema FTA hiyo itasaidia usafirishaji wa bidhaa kati ya EAC na Singapore na kwamba nchi yake itawapatia wasafirishaji wa EAC njia za kuingia katika soko kubwa la Asia.
Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam akikagua gwaride la heshima la mapokezi mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa ziara ya Kitaifa.
“Tumeibua maeneo mengine ya ushirikiano kama vile digital economy (uchumi wa kidijitali), ambao utasaidia kubadilisha mtandao wa biashara zetu ukizingatia mabadiliko ya siasa za dunia,” amesema Rais huyo wa Singapore.
Mikataba mitano yasainiwa
Wakati huohuo, Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Singapore zimetiliana saini rasimu tano za hati za makubaliano ya ushirikiano zinazolenga kuimarisha uhusiano, kukuza biashara na uwekezaji baina yao.
Mikataba iliyosainiwa ni wa kuondoa utozaji kodi mara mbili na zuio la ukwepaji na uhepaji wa kodi, pamoja na rasimu ya hati ya makubaliano kati ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Wizara ya Mambo ya Nje ya Singapore katika masuala ya uendelezaji wa ujuzi.
Pia, wametiliana saini rasimu ya hati ya makubaliano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na Wizara ya Viwanda na Biashara ya Singapore katika biashara za kaboni chini ya Ibara ya 6 ya Mkataba wa Paris.
Makubaliano mengine yaliyosainiwa ni rasimu ya hati ya makubaliano ya mashauriano ya uwili kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Mambo ya Nje ya Singapore.
Kadhalika, imesainiwa rasimu ya hati ya makubaliano kati ya Wizara ya Viwanda na Biashara na Taasisi ya Singapore katika masuala ya uwezeshaji wa biashara.