Tanzania yaingiza tani 52,000 nyama ya nguruwe kutoka nje

Muktasari:

  • Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limefanya mkutano na wafugaji na wafanyabishara wanyama hao kutoka Mikoa ya Mbeya, Iringa, Katavi na Rukwa kujadili namna ya kukabiliana na magonjwa yanayowakabili wanyama hao na kuongeza uzalishaji.

Mbeya. Chama cha Wafugaji Nguruwe Tanzania (TAFIPA) kimesema wastani wa tani 52,000 za nyama ya nguruwe huingizwa nchini kila mwaka kutoka nje ya nchi, huku Tanzania ikizalisha tani 27,000 pekee.

 Katibu wa chama hicho, Collins Ritenga amesema leo Jumamosi Mei 6, 2023 kwenye mkutano ulioratibiwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ukihusisha wafugaji na wafanyabishara wanyama hao kutoka Mikoa ya Mbeya, Iringa, Katavi na Rukwa.

Kikao hicho kimelenga kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kuthibiti na kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mafuta ya nguruwe ambao umekuwa ni changamoto katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

“Licha ya jitihada kubwa za wananchi kujihusisha na ufugaji wa nguruwe, bado kuna changamoto ya kutofikia malengo ya uzalishaji wa kibiashara kama mataifa mengine, ikiwepo ufugaji wa mazoea unaochangia kupata changamoto za ugonjwa wa homa ya mafuta ya nguruwe,” amesema.

Katibu wa  Chama cha Wafugaji Nguruwe Tanzania (TAFIPA), Collins Ritenga akiwasilisha mada ya hali ya ufugaji mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Picha na Hawa Mathias.

Ameongeza kuwa ujio wa FAO huenda ukawa mwarobaini kwa wafugaji kuondokana na ufugaji wa mazoea ikiwepo changamoto za kukabiliana na ugonjwa hho ambao umekuwa ukiathiri sana sekta ndogo ya ufugaji nguruwe nchini

Akizungumza katika mkutano huo, mratibu wa mradi huo kutoka FAO, Dk Raphael Sallu amesema wamelenga kuweka mikakati ya pamoja kukabiliana na tatizo la homa ya nguruwe.

Ametaja mikakati hiyo kuwa pamoja na kuboreshwa kwa maabara ya Wakala wa Veterinari Tanzania (TVLA) Kanda ya Iringa sambamba na kuweka vifaa vya kisasa vya kupima sampuli ili kutoa elimu kwa wataalam wa maabara na wanasayansi ili  kudhibiti ugonjwa huo.

“Ili kuweza kubaini ukubwa wa tatizo tumeona ni vyema kutokutegemea maabara katika Mikoa ya Morogoro na Rukwa ambazo zimekuwa ni changamoto uchelewashi wa majibu na kusababisha kuenea haraka kwa ugonjwa huo,” amesema.

Kwa upande wake Ofisa ufuatiliaji magonjwa ya mifugo Wizara ya Kilimo na Mifugo, Dk Makungu Seleman amesema kama Wizara wametoa maelekezo kwa maofisa mifugo nchini kuwa karibu na wafugaji kwa lengo la kutoa elimu ya namna ya kukabiliana na ugonjwa ambao ni hatari.

 “Tumekutana mkoani Mbeya  na wadau kutokamikoa mwingine lengo ni kujadiliana na kwa pamoja na kutoka na maadhimio ya pamoja ya kukabiliana na ugonjwa wa mafua ya homa ya nguruwe kutokana na mikoa ya nyanda za Juu Kusini kuathirika kwa kiwango kikubwa,” amesema.