Uelewe mfumo wa fedha wa Kiislamu
Katika miaka ya hivi karibuni, huduma za fedha za Kiislamu zimekuwa mojawapo ya uvumbuzi muhimu katika sekta ya kifedha nchini.
Taasisi mbalimbali za kifedha kama benki zimeanza kutoa huduma hizi kwa kuzingatia kanuni za fedha za Kiislamu. Kwa mfano, akaunti za akiba na utoaji mikopo ambayo inakidhi matakwa ya Sharia. Hali kadhalika, huduma za bima ya Takaful zimeanza kupata umaarufu.
Mfumo wa fedha za Kiislamu ni njia ya kupanga na kutoa huduma za kifedha kwa kufuata mafundisho ya Kiislamu kuhusu fedha na uchumi. Kanuni hizi, zinazoitwa Sharia Muamalat, zinatoa mwongozo kuhusu jinsi ya kufanya shughuli za kifedha na biashara kwa waamini katika maisha yao ya kila siku.
Inajumuisha namna ya kutekeleza mambo mbalimbali kama kukopa au kukopesha, kununua na kuuza, kukodisha, kupanga bei, kupima bidhaa, kutoa zaka na sadaka, kutoa msaada, kuingia mkataba, kuanzisha ubia, kuweka amana na kadhalika.
Katika utoaji huduma za kifedha rasmi mfano kibenki au bima, kuna misingi sita muhimu inayotumiwa kikanuni ambayo ni kuepuka riba, kuepuka hatari zisizotabirika kibiashara, kuepuka kamari, kuwekeza katika shughuli halali, kugawana faida au hasara na usawa na haki. Kufuata misingi hiyo inafanya huduma hizo kuwa adilifu na zenye kufaa kulingana na mafundisho.
Kwa mfano, katika mfumo wa ukopeshaji wa Kiislamu, benki inaweza kuingia ubia na mteja (musharaka). Hapa, benki na mteja wanaweza kuwekeza pamoja katika biashara na kugawana faida na hasara. Au, benki inaweza kukopesha kwa njia ambayo inakuwa mshirika katika biashara ya mteja, hivyo kuchangia katika faida na hasara zake.
Pia mikopo inaweza kutolewa kwa njia ya mkataba wa Murabaha. Kwa mfano, mteja anayetaka mkopo wa gari, benki itanunua gari kwa niaba yake, kisha baadaye kuiuza kwa mteja kwa bei iliyokubaliwa, ambayo inajumuisha faida ya benki. Mteja atalipa gharama ya gari pamoja na faida ya benki kwa awamu au kwa wakati uliopangwa.
Mfumo huu unatumika kwa kuzingatia misingi ya Sharia, kwa kuwa unalenga kuepuka riba kwenye mkopo. Faida ya benki inategemea tofauti kati ya bei ya kununua na bei ya kuuza gari, na sio kiwango cha riba kilichowekwa kwenye mkopo (fixed interest). Kwa hivyo, faida hiyo inahusishwa na gharama ya biashara (markup) na inaungwa mkono na mali halisi ya mteja (asset-backed).
Kwa mfano, wavumbuzi huduma za kifedha Kiislamu wanapendekeza bima ya Takaful ambayo muundo wake unahimiza kuwa na mfuko wa uwekezaji (Takaful Fund) ambao michango iliyopokelewa kutoka kwa wateja waliokata bima baadaye itawekezwa katika biashara mbalimbali zinazokubalika kuwa ni shughuli halali kisheria.
Kufanya hivyo kunaleta tija kubwa nne, kwanza, mteja aliyekata bima hatapoteza kabisa michango yake ikiwa janga halitatokea, inaondoa mazingira ambayo kanuni za fedha za Kiislamu zinataja kuwa ni “gharar au maysir”, kubahatisha au kuotea kama ilivyo katika bima ya kawaida janga lisipotokea michango “premiums” zimepotea.
Pili, kwa kuanzisha mfuko wa uwekezaji, mteja na kampuni ya bima, wanakuwa amefungua ushirikiano wa kibiashara (Mudaraba).
Tatu, inaleta usawa kupitia kugawana faida au hasara inayopatikana kutokana na uwekezaji wa michango hiyo (profit&risk sharing). Na nne, inaleta uwazi, mteja anaweza kujua michango yake imewekezwa wapi na katika shughuli gani.
Huduma za fedha za Kiislamu ni kwa yeyote anayehitaji, uanzishwaji wake ulikusudia kutanua wigo kwa kuwapa fursa wengine ambao katika huduma za kawaida zinawaacha nje ya uwanja.
Baadhi ya benki kubwa maarufu kimataifa zinazotoa huduma hizo ni kama Citibank ya Marekani, HSBC ya Hong Kong, PNB Paribas ya Ufaransa, na Standard Chartered ya Uingereza.